SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imepiga marufuku kusafirisha mkaa kutoka wilaya moja kwenda wilaya nyingine, kwa lengo la kukabiliana na tatizo kubwa la ukataji wa miti unaendelea hali inayochangia kukosekana kwa mvua katika maeneo mengi nchini.
Waziri wa wizara hiyo, Profesa Jumanne Maghembe amewaagiza maofisa misitu wa wilaya zote nchini, wasitoe vibali vinavyoruhusu mkaa kusafirishwa kutoka nje za wilaya zao na pia wakamate mfanyabiashara yoyote yule atakayethubutu kusafirisha mkaa kwenda wilaya nyingine.
Akizungumza jana katika siku ya kilele cha maadhimisho ya miaka 110 ya Vita vya Maji Maji na uzinduzi wa Makumbusho ya hayati Rashidi Kawawa, yaliyofanyika wilayani Songea mkoani Ruvuma, Profesa Maghembe alisema mkaa utakaozalishwa katika wilaya utumike ndani ya wilaya hiyo hiyo hakuna kusafirishwa kwenda nje.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara yake kwa vyombo vya habari, Profesa Maghembe alisema kutokana na matumizi makubwa ya mkaa ndani na nje ya nchi, akitolea mfano Mkoa wa Tanga ambako mkaa wake umekuwa ukisafirishwa Zanzibar na hatimaye kupelekwa nchi za Uarabuni, ambako kumekuwa na soko kubwa la mkaa kutoka Tanzania, umechangia idadi kubwa ya miti kukatwa kutokana na hali hiyo athari zimeanza kujitokeza katika mikoa ya kaskazini.
“Kama serikali hatuwezi kukaa kimya huku tukiacha hali hii ikiendelea, ni lazima tuchukue hatua madhara ya kutopata mvua ya kutosha yanayotokea kwa sasa katika mikoa hiyo na baadhi ya maeneo ya mengi nchini yanasababishwa na miti mingi kukatwa bila kufuata utaratibu,” alibainisha Profesa Maghembe.
Aidha, alisema licha ya biashara hiyo ya uuzaji mkaa kufanywa ndani na nje ya nchi, watu wanaojihusisha na uchomaji wa mkaa wamezidi kuwa watu maskini kwa vile wafanyabiashara wamekuwa wakiwalangua kwa bei ndogo huku wao wakiuuza kwa bei kubwa sokoni halafu wahusika wakizidi kutumbukia kwenye hali umaskini na ndio waathirika wakubwa ukame na pale mvua inapokuwa hainyeshi.
Miongoni mwa mikoa ambayo itaathirika na uamuzi huo wa serikali ni Jiji la Dar es Salaam, ambalo limekuwa likitegemea mkaa kutoka nje ya mkoa huo.
Nchini Tanzania zaidi ya ekari 370,000 za misitu huharibiwa kila mwaka, kiwango kikubwa kwa matumizi ya nishati, kwa mujibu wa Wakala wa Misitu yenye mamlaka ya kuangalia matumizi mbalimbali ya misitu.
Mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam inaongoza kwa matumizi ya mkaa kama chanzo kikuu cha nishati kwa matumizi ya majumbani, huku Mkoa wa Simiyu ukiwa na idadi ndogo zaidi ya matumizi ya nishati hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya mgawanyo wa kijamii na kiuchumi iliyotolewa mwaka jana na Ofisi ya Takwimu Nchini (NBS), Dar es Salaam ndiyo inayoongoza kwa matumizi ya mkaa, japokuwa mkoa huu una vyanzo mbalimbali ambavyo ni rafiki wa mazingira.
Matumizi makubwa ya mkaa katika mikoa hiyo, umesababisha kichocheo cha ukataji wa miti katika mikoa mingine na inakadiriwa kuwa karibu hekta 300,000 hadi 400,000 za misitu ya asili huharibiwa kila mwaka kutokana na utengenezaji mkaa.
Ripoti hiyo iliyochapishwa na NBS imeonesha kwamba zaidi ya asilimia 73 (familia nane kati ya 10) wanatumia mkaa kama chanzo cha nishati kwa ajili ya kupikia.
Katika hatua nyingine, Profesa Maghembe ameiomba Serikali ya Ujerumani irudishe kichwa cha aliyekuwa Kaimu Nduna, Songea Mbano aliyenyongwa na kisha kukatwa kichwa katika vita vya Majimaji na baadaye kuzikwa kwenye kaburi la pekee yake katika eneo ambalo mashujaa wenzake wapatao 66 walinyonyongwa na kuzikwa katika kaburi moja.
Amemwambia Balozi wa Ujerumani, Egon Kochanke katika maadhimisho hayo kuwa ni muda muafaka sasa kukirudisha kichwa hicho kwa kuwa shujaa huyo hakuwa raia wa Ujerumani alikuwa Mwafrika hivyo ni vyema kichwa chake kikarudishwa katika ardhi yake.
Awali, wakati akizindua nyumba ya Makumbusho ya Rashidi Mfaume Kawawa (Simba wa Vita), aliishukuru familia yake kwa kukubali kukabidhi nyumba ya Bombambili Songea kwa Wizara ya Maliasili na Utalii itakayotumika kuhifadhi historia ya maisha yake, kumbukumbu za kazi na mchango wake katika kulitumikia Taifa.
Pia aliwataka Watanzania kumuenzi Mzee Kawawa kwa kuwa maisha yake yote aliyatoa kwa kuwatumikia Watanzania bila kujali itikadi zozote.