Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utalii wa Wizara ya Maliasili, Paskasi Mwiru (wapili kushoto) akizungumza kumkaribisha mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza kufunga mafunzo hayo.
Picha ya pamoja.
................................................................
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeandaa kanuni ambayo itavibana vyuo vinavyofundisha utalii na ukarimu ili viweze kuzalisha wataalamu wenye ubora.
Kanuni hiyo itasaidia kuthibiti utitiri wa vyuo vilivyoanzishwa nchini huku vikiwa vimejikita kupata faida wakati wahitimu wanaozalishwa kupitia vyuo hivyo wakiwa ni wa viwango vya chini.
Kufuatia hali hiyo hata wataalamu watakaozalishwa kupitia vyuo hivyo watasimamiwa lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa kwa watalii zinakidhi viwango vinavyokubalika.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza aliyasema hayo jana mjini Iringa wakati akifunga mafunzo ya ukarimu na utalii yaliyofanyika kwa muda wa siku tatu kwa wahudumu wa hoteli na migahawa kwa kuratibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Mradi wa SPANEST.
‘’Wale wamiliki wa hoteli wenye tabia ya kuajiri ndugu zao wasio kuwa na ujuzi wowote huu ndo utakuwa mwisho wao,kama kuna yeyote anayetaka kufanya kazi katika tasnia hii ni lazima aende shule’’. Alisisitiza Masenza.
Akitaja sababu ya Nyanda za juu kusini kutembelewa na watalii wachache licha ya kuwa na vivutio lukuki, alisema wahudumu nao wamekuwa kikwazo kwani baadhi yao hawana elimu kabisa.
Akitoa takwimu za mwaka 2015, Mkuu wa Mkoa alisema ni asilimia nne tu ya watalii 764,837 toka nje ya nchi na asilimia nane tu ya watalii 641, 114 wa ndani waliotembelea vivutio vya mikoa ya kusini huku idadi kubwa iliyobaki wakitembelea vya kaskazini.
Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utalii wa Wizara ya Maliasili, Paskasi Mwiru alisema serikali imeamua kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa watoa huduma baada ya kubaini baadhi ya vyuo vinavyotoa mafunzo ya ukarimu na utalii nchini, vinayatoa chini ya kiwango.
Kwa kupitia mafunzo hayo, alisema watoa huduma wanapewa mafunzo katika maeneo ya mapokezi, utoaji wa huduma ya chakula na vinywaji, upishi na namna ya kukuza huduma ya malazi ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa katika sekta ya ukarimu na utalii katika mikoa ya kusini ambayo ipo chini.
Kwa kupitia mafunzo hayo, jumla ya wahitimu 80 kati ya zaidi ya 100 waliojitokeza wamefanikiwa kuhitimu na kutunukiwa vyeti walivyokabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Mradi wa SPANEST umechangia zaidi ya asilimia 75 ya gharama zote za kuendesha mafunzo hayo lengo likiwa ni kushirikiana na Serikali katika kukuza na kuendeleza utalii katika Kanda ya Kusin.
No comments:
Post a Comment