slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Wednesday, May 18, 2016

KATIBU MKUU WIZARA YA MALIASILI NA UTALII MAJ. GEN. GAUDENCE MILANZI AONGOZA MKUTANO WA 23 CHA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA WIZARA HIYO

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (katikati),  Naibu Katibu Mkuu Angelina Madete (kulia) na Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Maliasili na Utalii Wilfred Msemo (kushoto) wakiimba wimbo wa wafanyakazi wa "Solidarity Forever" wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 23 wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Maliasili na Utalii uliofanyika jana tarehe 17 Mei, 2016 katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii, tawi la Bustani, Jijini Dar es Salaam. 
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi akizungumza wakati akifungua Mkutano wa 23 wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Maliasili na Utalii uliofanyika jana katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Jijini Dar es Salaam. 

Katika salamu zake amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuhakikisha kuwa wanatimiza wajibu wao katika kutekeleza lengo kuu la Wizara ambalo ni kuendeleza uhifadhi wa Maliasili, Malikale na Kukuza Utalii nchini. 

Amewataka watumishi wote wa Wizara kuwa waadilifu, wabunifu, kufanya kazi kwa ushirikiano, kuepuka vitendo vya rushwa na makundi yasiyokuwa na tija kwa Wizara na Serikali kwa ujumla. 

Alionya kuwa, Mtumishi yeyote atakeenda kinyume cha sheria na taratibu hatosita kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kuachishwa kazi ili kwenda sambamba na kauli mbiu ya Serikali ya awamu ya tano ya "HAPA KAZI TU"

Maj. Gen. Milanzi alimuwakilisha Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe ambaye yupo Mkoani Dodoma kwa ajili ya majukumu mengine ya Kiserikali (Bunge la bajeti).
Sehemu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Maliasili na Utalii wakiimba wimbo wa kuashiria umoja wa wafanyakazi (Solidarity Forever). 
Sehemu ya wajumbe wa Mkutano huo.
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano huo wakiimba wimbo wa umoja wa wafanyakazi "Solidarity Forever"

Saturday, April 2, 2016

SERIKALI YA UJERUMANI YATOA MSAADA WA NDEGE MAALUM AINA YA HUSKY A-1C KUSAIDIA DORIA YA KUPAMBANA NA VITENDO VYA UJANGILI KATIKA PORI LA AKIBA LA SELOUS

Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd Muller alipowasili katika uwanja mdogo wa ndege wa Matambwe uliopo ndani ya Hifadhi ya akiba ya Selous Mkoani Morogoro kwa ajili ya hafla ya makabidhiano ya ndege maalum aina ya Husky A-1C kutoka Serikali ya Ujerumani itakayosaidia kufanya doria za kupambana na ujangili katika hifadhi hiyo.
Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe (katikati) akizungumza na Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd Muller (kushoto) katika hafla fupi ya makabidhiano ya msaada wa ndege maalum aina ya Husky A-1C kutoka Serikali ya Ujerumani itakayosaidia kufanya doria za kupambana na ujangili katika Hifadhi ya Akiba ya Selous. Wengine ni Meneja wa Hifadhi ya Selous Bw. Mabula Misungwi (wa pili kushoto), Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania Bw. Martin Laibooki (wa pili kulia) na Bw. David Kanyatta Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Wanyamapori.
Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe (katikati) akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa ndege maalum kutoka Serikali ya Ujerumani aina ya Husky A-1C kwa ajili ya kufanya doria za kupambana na ujangili katika Hifadhi ya Akiba ya Selous. Kutoka kushoto ni Balozi wa Ujerumani hapa nchini Mhe. Egon Konchanke, Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd Muller, Dkt. Christof Schenck Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uhifadhi la Kimataifa la FZS na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania Bw. Martin Laibooki.

Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd Muller akizungumza katika hafla hiyo.
Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd Muller (wa pili kushoto) akimkabidhi Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe msaada wa ndege maalum aina ya Husky A-1C kwa ajili ya kufanya doria za kupambana ujangili katika Hifadhi ya Akiba ya Selous. Wanaoshuhudia Kulia ni Rubani wa Ndege hiyo Capt. Bernard Shayo, Dkt. Christof Schenck Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uhifadhi la Kimataifa la FZS (wa pili kulia) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) Bw. Martin Laibooki.

Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kulia) akifanya majaribio ya kupanda ndege maalum aina ya Husky A-1C iliyotolewa na Serikali ya Ujerumani kwa ajili ya kufanya doria za kupambana na ujangili katika Hifadhi ya Akiba ya Selous. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd Muller (wa pili kushoto), Capt. Bernard Shayo (kulia), Bw. David Kanyatta Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Wanyamapori (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania Bw. Martin Laibooki (wa tatu kushoto). 
Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd Muller akiwa na baadhi ya askari wa Wanyamapori katika Hifadhi ya Akiba ya Selous.
Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akiwasalimia askari wa Wanyamapori katika Hifadhi ya Akiba ya Selous. Kulia anayeshuhudia ni Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd Muller ambaye amemkabidhi Prof. Maghembe msaada wa ndege maalum aina ya Husky A-1C ya kufanya doria za kupambana na ujangili katika Hifadhi ya Akiba ya Selous.
 Sehemu ya kundi la Swala katika hifadhi ya akiba ya Selous.
Moja ya Twiga akiwa anakimbia katika hifadhi ya akiba ya Selous.
Sehemu ya wajumbe wa msafara wa Waziri Maghembe na Waziri wa Muller wakibadilishana mawazo katika hifadhi ya akiba ya Selous.
..............................................................

Serikali ya Ujerumani imetoa msaada wa ndege maalum aina ya “Husky A-1C Aircraft” kwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Malisili na Utalii kwa ajili ya kusaidia katika doria za kupambana na Ujangili katika Pori la Akiba la Selous.

Msaada huo wenye thamani ya Euro 200,000 sawa na Tsh. 498,292,000, umekabidhiwa kwa Mhe. Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe na Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd Muller katika hafla fupi iliyofanyika Matambwe ndani ya pori la Akiba la Selous.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Maafisa wa Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini wakiongozwa na Balozi Mhe. Egon Konchanke, viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii,          Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mashirika ya Maendeleo ya Kimataifa ya FZS, WWF, GIZ na KFW.

Akizungumza katika hafla hiyo Waziri Maghembe amesema ndege hiyo itasaidia jitihada za Serikali za kupambana na Ujangili kwa kufanya doria katika anga ya hifadhi ya Akiba ya Selous na kusaidia kutoa taarifa za kiuhalifu pale itakapobainika na kuchukuliwa hatua stahiki za kukabiliana na uhalifu huo.

“Ndege hii tunayoshuhudia mapokezi yake leo ni ukombozi kwa Wanyamapori katika Pori hili la Akiba la Selous kwani itasaidia na kuimarisha doria za kupambana na ujangili ndani na kuzunguka eneo zima la hifadhi”. Alisema Prof. Maghembe.

Waziri Maghembe ameishukuru Serikali ya Ujerumani kupitia kwa Waziri Muller kwa msaada huo na mingine ambayo wamekuwa wakiitoa kusaidia uhifadhi wa Wanamapori hapa nchini, Amebainisha kuwa misaada hiyo imekuwa na tija kubwa katika kuendeleza uhifadhi wa Wanyamapori ikilinganishwa na kipindi cha nyuma kabla ya kuwepo kwa misaada hiyo.

Waziri Maghembe alieleza kuwa sera ya Wanyamapori Tanzania inatambua ushirikiano wa wahisani na watu binafsi katika kuisaidia Serikali Kifedha na Kitaaluma kwenye eneo la uhifadhi, hivyo amewaomba wadau mbalimbali kuendelea kuipa ushirikiano Serikali katika jitihada zake za kuendeleza Uhifadhi wa Wanyamapori nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Ujerumani Dkt. Gerd Muller alimueleza Prof. Maghembe kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza uhifadhi hapa nchini. Waziri huyo pia aliwapongeza Askari wa Wanyamapori kwa kazi nzuri wanayofanya ya kulinda Wanyamapori katika mazingira magumu ya porini.

Akizungumza kwa lugha ya Kijerumani huku ikitafsiriwa kwa Kiingereza na Mkalimani wake Dkt. Muller alisema ipo haja kubwa ya kuendelea kuwalinda Wanyamapori kwa nguvu zote kwa kuwa hawana hatia na kwamba walikuwepo katika mazingira yao ya asili kabla hata ya binadamu kuwepo hapo.

“Hawa viumbe hai wanaowindwa walikuwepo katika mazingira haya kabla ya sisi binadamu kuja hapa, Sote tunahitaji kuwalinda na kuishi kwa amani na viumbe hawa ndio kutakuwa na amani duniani kote” Alieleza Dkt. Muller.

Mapema akizungumza kabla ya tukio la kukabidhiwa ndege, Meneja wa Pori hilo la Akiba la Selous Bw. Mabula Misungwi alieleza baadhi ya changamoto kuu zinazoikabili hifadhi hiyo kuwa ni ujangili, miundombinu mibovu ya barabara kwa ajili ya doria na vifaa ikiwemo magari ya doria.

Msafara wa Waziri Maghembe na ugeni wake kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya hifadhi ya Selous ikiwemo Matambwe na Behobeho ambayo inajulikana kama Serengeti ndogo na kujionea Wanyamapori mbalimbali wakiwemo Tembo, Twiga, Pundamilia, Swala, Nyani, Ngiri, Nyumbu na mandhari mazuri ya mto behobeho.

Pori la Akiba la Selous ni moja ya Pori kubwa duniani ikiwa na ukubwa wa zaidi ya Kilomita za mraba 50,000. Pori hili lipo ndani ya Mikoa mitano ya Tanzania ambayo ni Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na Songea. Pori hili limeathiriwa kwa kiasi kikubwa na ujangili kwani katika Sensa ya mwaka 2013 ilionesha idadi ya tembo katika pori hilo kuwa 13,000 idadi ambayo ni ndogo sana ikilinganishwa na ile ya mwaka 2003 ambayo ilikuwa 70,000.

Saturday, March 26, 2016

WAZIRI MAGHEMBE AWASIMAMISHA KAZI WATENDAJI TFS NA KAIMU MKURUGENZI IDARA YA WANYAMAPORI

Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Machi, 2016. Kulia ni Naibu Waziri Eng. Ramo Makani.
Sehemu ya waandishi wa habari na wajumbe mbalimbali walioshiriki Mkutano huo.
........................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Mghembe amemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu nchini, (TFS) Bw. Juma Mgoo pamoja na Wakurugenzi wawili wa Taasisi hiyo ili kupisha uchunguzi kutokana na mwenendo usioridhisha wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali na usimamizi mbovu wa rasilimali za misitu nchini.

Prof. Maghembe ametaja majina ya Wakurugenzi hao aliowasimamisha kazi kuwa ni Mkurugenzi Rasilimali Misitu, Bw. Zawadi Mbwambo pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi endelevu ya Misitu, Bw. Nurdin Chamuya

Baada ya kuwasimamisha hao amewateua watu wengine kushika nafasi zao wakati mchakato wa kuwapata watendaji wapya ukifanyika na walioteuliwa kukaimu nafasi hizo ni Kaimu Mtendaji Mkuu TFS, Gerald Kamwendo, Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Misitu, Mwanaidi Kijazi, na Kaimu Mkurugenzi wa Matumizi Rasilimali Misitu, Haji Mpya.

Wengine waliosimamishwa kazi na kanda zao katika mabano ni Hubert Haule (Kusini), Bakari Rashid (Mashariki), Cuthbert Mafipa (Kaskazini), Emmanuel Minja (Magharibi), Haji Khatibu (Ziwa) na Bruno Mallya (Nyanda za Juu Kusini).

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Prof. Maghembe amesema hatua hiyo imekuja baada ya kubaini mapungufu mbalimbali katika ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali na usimamizi usioridhisha wa rasilimali za misitu.

Alisema kuwa hivi karibuni walibaini shehena kubwa za magogo aina ya mninga katika Mkoa wa Rukwa wilayani Kalambo yakiwa yamekatwa na kuwekwa ndani ya makontena ndani ya msitu pamoja na kutengenezewa nyaraka feki zinazoonesha magogo hayo yanatoka nchini Zambia tayari kwa kusafirishwa kupelekwa nchini China.

Amesema kuwa baada ya kubaini tukio hilo na kulitolea maamuzi alipata taarifa kuwa shehena ya Magogo hayo yenye thamani ya shilingi milioni 500 za Kitanzania yaliyotakiwa kupelekwa Makao makuu ya Wilaya ya Kalambo yamemwagiwa petroli na kuchomwa moto wakati wiki mbili kabla alishatoa agizo la magogo hayo kusafirishwa kupelekwa Matai ambapo ni Makao Makuu ya Wilaya ya Kalambo.

Aliongeza kuwa kumekuwa na ubadhilifu unaofanywa na Maofisa wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika Mikoa na Wilaya kwa kutowasilishwa katika mfuko Mkuu wa Serikali.

“Pesa zitokanazo na makusanyo hayo zimekuwa hazipelekwi benki kwa wakati na hata zikipelekwa benki zimekuwa zikipelekwa pungufu na muda mwingine pesa hizo zimekuwa hazipelekwi kabisa”. Alisema Prof. Maghembe.

Katika tukio lingine, Waziri Maghembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori wa Matumizi Endelevu, Dkt. Charles Mulokozi kwa kosa la kukaidi agizo la kusaini vibali vya kusafirisha Wanyamapori nje ya nchi.

Hatua hiyo imekuja baada ya kukamatwa watu katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro wakitaka kusafirisha nyani 61 “velvety monkeys” na kubaini kuwa Idara ya Wanyamapori ndio iliyotoa vibali vya kusafirisha nyani hao na vibali hivyo kusainiwa na Mkurugenzi huyo.

Alisema watu hao kutoka Ulaya Mashariki na washirika wao wa hapa nchini, walikodisha ndege ili kuwaondoa tumbili hao kwenda Ulaya Mashariki. Alisema harakati za kukamata tumbili hao porini zilianza wiki iliyopita na jumla ya idadi yao ni 450 ilhali kuna taasisi zinazolinda hayo mapori bila walinzi wa mapori hayo kujua

Prof. Maghembe alisema nyani hao walikamatwa maeneo ya Upareni, Hanang Manyara na Kiliamanjaro ambapo aliwaita wasimamizi na kuwapa taarifa juu ya watu hao na kuwakataza kutotoa kibali chochote cha kusafirisha wanyama hao.

“Nikiwa Moshi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa nilimuita Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Wanyamapori Matumizi Endelevu, Dk Charles Mulokozi na kumuarifu juu ya kamata kamata hiyo na kumuagiza kutotoa kibali cha kusafirisha wanyama ili tuwakamate watu hao, lakini baadaye tukagundua yeye ndio amesaini kibali hicho kutoka Dar es Salaam,” alisema Maghembe.


Ameongeza kuwa ndege iliyokamatwa ilikuwa imekodiwa kutoka Afrika ya Kusini kwa ajili ya kusafirisha nyani hao kwenda Ulaya ya Mashariki, Ndege hiyo imeshikiliwa pamoja na rubani wake kwa mahojiano zaidi.

Prof. Maghembe ametoa onyo kali kwa wale wote wanaohujumu rasilimali za nchi na kusema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali.

“Hatutasita kumfukuza kazi mtu yeyote ambaye atashiriki katika suala hili la kuiibia nchi mali zake au anakaa anaangalia kando wakati fedha za nchi, mali za nchi zinaporwa” Alisema Prof. Maghembe kwa ukali.

SERIKALI YA TANZANIA HAINA MPANGO KWA KUTEKETEZA MENO YA TEMBO YALIYOHIFADHIWA

Serikali ya Tanzania imetoa tamko kuwa kwa sasa haina mpango wowote wa kuteketeza meno ya tembo yaliyohifadhiwa ambayo yametokana na vitendo vya ujangili na vifo asilia vya tembo.

Tamko hilo limetolewa hivi karibuni na Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Balozi wa Marekani hapa nchini Bw. Mark Childress alipotembelewa na balozi huyo ofisini kwake kujadili maendeleo ya sekta ya Maliasili mchini.

Prof. Maghembe alisema hayo baada Balozi huyo wa Marekani hapa nchini kutoa pendekezo kwa Serikali ya Tanzania kuchoma sehemu meno ya tembo yaliyohifadhiwa ili kutoa ujumbe mzito duniani juu ya dhamira ya Serikali kukomesha biashara hiyo haramu.

"Naomba niweke wazi kuwa kwa sasa hatupo tayari kuteketeza meno haya, tunaweza kuyatumia kwenye tafiti za kisayansi au vielelezo kwa ajili ya kesi za ujangili ambazo zipo mahakamani na nyingine ambazo bado zinafanyiwa uchunguzi" Alisema Prof. Maghembe.

Zipo nchi mbalimbali duniani ambazo zimechukua hatua ya kuteketeza meno yake ya tembo yaliyohifadhiwa ikiwemo nchi jirani ya Kenya na Malawi ambapo inaaminika kuwa kufanya hivyo ni njia mojawapo ya kushawishi Ulimwengu kukomesha biashara hii haramu ya meno ya tembo.

Nchi nyingine ni Chad, Ubelgiji, Ufaransa, China, India, Marekani na Ureno. Kwa upande wa nchi ambazo zina msimamo sawa na Tanzania katika kuendelea kuhifadhi meno yake ya Tembo ni pamoja na Afrika ya Kusini, Botswana na Zimbabwe.

Akizungumzia kuhusu kuendeleza sekta ya Maliasili nchini, Prof.Maghembe amemuomba Balozi wa Marekani Bw. Mark Childress kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukuza sekta hiyo kwa kuleta wawekezaji mbalimbali kutoka Marekani kuja kuwekeza Tanzania pamoja na kusaidia kwenye mapambano dhidi ya Ujangili.

Aliongeza kuwa Tanzania ina fursa nyingi ambazo zinahitaji uwekezaji mkubwa ikiwemo hoteli za kitalii, fukwe za kisasa na kuendeleza vivutio mbalimbali vilivyomo hapa nchini.

Prof. Maghembe amemshukuru balozi huyo kwa misaada mbalimbali kutoka Serikali ya Marekani ya kuendeleza sekta ya Maliasili nchini ukiwemo wa hivi karibuni wa mbwa maalum (Snifer Dogs) kwa ajili ya kusaidia utambuzi wa rasilimali za Maliasili zinazoweza kutoroshwa nje ya nchi kupitia bandari na viwanja vya ndege.

Katika taarifa iliyowasilishwa kwenye kikao baina ya Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe na Balozi wa Marekani hapa nchini Bw. Mark Childress imeonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali ya Marekani imetoa misaada mbalimbali ambayo jumla yake ni dola za kimarekani Milioni 41.35 katika kusaidia eneo la uhifadhi hapa nchini.



Akizungumzia mahusiano baina ya Tanzania na Marekani Balozi Mark Childress alimueleza Prof. maghembe kuwa Serikali ya Marekani itaendeleza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi hizi mbili ambapo pia ofisi yake ya ubalozi imeshatafuta wadau mbalimbali ambao wapo tayari kusaidia fedha, vifaa na mafunzo kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi na mapambano dhidi ya ujangili. 

Wednesday, March 23, 2016

WAZIRI WA MALIASILI PROF. JUMANNE MAGHEMBE AONANA NA BALOZI WA MAREKANI HAPA NCHINI MHE. MARK CHILDRESS KUJADILI MAENDELEO YA SEKTA YA MALIASILI NCHINI

Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akizungumza katika kikao na Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Mark Childress (kulia) na Ujumbe wake katika ukumbi wa Selous Makao Makuu ya Wizara hiyo Mpingo House leo tarehe 23 Machi, 2016. Waziri Maghembe amemuomba Balozi huyo wa Marekani kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukuza sekta ya utalii nchini kwa kuwakaribisha wawekezaji kutoka Marekani kuwekeza katika sekta hiyo.
Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Mark Childress (kulia) akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (kushoto). Balozi huyo wa Marekani ameahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Marekani katika kuendeleza sekta ya uhifadhi hapa nchini. Ameahidi pia kusaidia katika vita dhidi ya ujangili.
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akisisitiza jambo kwa  Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Mark Childress (wa pili kushoto). Mhe. Maghembe alimueleza balozi huyo kuwa Tanzania haiko tayari kuteketeza meno ya Tembo yaliyohifadhiwa mpaka hapo itakapoona namna bora zaidi ya kufanya kwani kwa sasa Meno hayo yanaweza kutumika kwa ajili ya tafiti mbalimbali za kisayansi na kusaidia pia katika utambuzi na vielelezo vya mashtaka ya ujangili. Mhe Maghembe alisema hayo baada ya Balozi Childress kutoa pendekezo kwa Serikali kuona uwezekano wa kuteketeza sehemu ya meno ya Tembo yaliyohifadhiwa ili kutoa ujumbe duniani wa namna Serikali ya Tanzania ilivyodhamiria katika vita dhidi ya Ujangili.
Sehemu ya wajumbe kutoka ubalozi wa Marekani walioongozana na Mhe. Balozi Mark Childress wakifuatilia mada katika kikao hicho. Wajumbe hawa kila mmoja aliwasilisha mada ikionyesha ushirikiano wa Serikali ya Marekani na Tanzania katika sekta ya uhifadhi hapa nchini.  
Baadhi ya wajumbe kutoka ubalozi wa Marekani na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kikao hicho.
Wajumbe kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii walioshiriki katika kikao hicho. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Bi. Angelina Madete.