slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Wednesday, December 14, 2016

RAIS DKT. JOHN POMBE MAGUFULI AWAAPISHA VIONGOZI MBALIMBALI AKIWEMO NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

4.Aloyce
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Dkt. Aloyce Kashindye Nzuki kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Ikulu jijini Dar es Salaam.
5
 Viongozi walioapishwa wakila kiapo cha Maadili mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam. Wakwanza kutoka kushoto ni Mkuu wa Itifaki Balozi Grace Alfred Martin, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Kashindye Nzuki, Katibu Mkuu Mawasiliano Dkt. Maria Sasabo, Katibu Mkuu Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe pamoja na Mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Olonyokie Ole-Sendeka
7.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi pamoja na viongozi walioapishwa Ikulu jijini Dar es Salaam Wakwanza kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Kashindye Nzuki, Katibu Mkuu Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe, Mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Olonyokie Ole Sendeka, Wakwanza kutoka kulia ni Mkuu wa Itifaki Balozi Grace Alfred Martin pamoja na Katibu Mkuu wa Mawasiliano Dkt. Maria Sasabo.
6
 Viongozi walioapishwa waki weka saini katika viapo vya maadili Ikulu jijini Dar es Salaam. Wakwanza kutoka kushoto ni Mkuu wa Itifaki Balozi Grace Alfred Martin, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mali asili na utalii Dkt. Aloyce Kashindye Nzuki, Katibu Mkuu Mawasiliano Dkt. Maria Sasabo, Katibu Mkuu Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe pamoja na Mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Olonyokie Ole Sendeka.

Monday, December 12, 2016

WAZIRI MKUU APOKEA TAARIFA YA FARU JOHN NA PEMBE ZAKE



...............................................

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti.


Akizungumza katika kikao kilichofanyika nyumbani kwake Oysterbay leo mchana (Ijumaa, Desemba 9, 2016) na kuhudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe na baadhi ya watendaji wa wizara yake, Waziri Mkuu amesema taarifa hiyo itafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi yake. 

"Nilipokea taarifa yenu jana saa 7 usiku lakini nikaahidi kuwa leo tukimaliza sherehe za 
maadhimisho ya Uhuru tukutane na kujadiliana kuhusu taarifa yenu,”amesema. 

Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Maghembe alisema hadi kufikia Desemba 
2015 wakati faru John anahamishwa alikuwa na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2) 
ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.

“Kati ya faru 37 waliokuwepo ndani ya kreta, watoto wake walikuwa 26 sawa na asilimia 70.2. Uamuzi wa kumuondoa John ulikuwa ni muhimu ili kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Waziri Maghembe.

Baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri Maghembe alisema Julai 10, 2016 afya ya faru John 
ilianza kudorora na alikufa tarehe 18 Agosti, mwaka huu. Taarifa hiyo 
iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na Faru. Kamati hiyo inaundwa 
na Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Mkurugenzi Mkuu wa 
NCAA na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.

Akikabidhi pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo
cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Bw. Robert Mande alimweleza kwamba 
pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na 
uzito wa kilo 2.3.

Watendaji wa wizara waliohudhuria kikao hicho ni Kaimu Katibu Mkuu, Bw. Iddi Mfunda; 
Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Bw. Freddy Manongi; 
Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Bw. Simon Mduma; Kaimu Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori, 
Bw. Alexander Songorwa na Mkuu wa Pori la Akiba la Ikorongo/Grumeti, Bw. 
Nollasco Ngowe. 

Desemba 6, mwaka huu, akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa 
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika 
kumhamisha faru maarufu kwa jina la ‘John’ kutoka kwenye hifadhi hiyo ifikapo 
Alhamisi, Desemba 8.

Alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani 
Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na 
Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani 
humo.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU

IJUMAA, DESEMBA 9, 2016.


Wednesday, December 7, 2016

RAIS MAGUFULI AFANYA MABADILIKO YA MAKATIBU WAKUU, NAIBU KATIBU WAKUU NA WAKUU WA MIKOA - MABADILIKO HAYO YAIGUSA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 07 Desemba, 2016 
amefanya uteuzi wa Katibu Mkuu mmoja na Mkuu wa Mkoa mmoja na pia amefanya 
mabadiliko madogo katika Wizara na Mikoa kama ifuatavyo;

Dkt. Magufuli amemteua 
Prof. Faustin Kamuzora kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais.Kabla ya uteuzi 
huo, Prof. Kamuzora alikuwa Katibu Mkuu Mawasiliano.

Rais Magufuli 
amemteua Mhandisi Mathew Mtigumwe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Uvuvi 
na Mifugo anayeshughulikia Kilimo. Mhandisi Mathew Mtigumwe anachukua nafasi ya 
Dkt. Frolence Turuka ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na 
Jeshi la Kujenga Taifa.

Kabla ya uteuzi 
huo Dkt. Frolence Turuka alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na 
Uvuvi aliyekuwa akishughulikia Kilimo. Anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. 
Job Masima ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.

Rais Magufuli 
amemteua Dkt. Maria Sasabo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na 
Mawasiliano na atakuwa akishughulikia Mawasiliano. Dkt. Maria Sasabo anachukua 
nafasi iliyoachwa wazi na Prof. Faustin Kamuzora ambaye ameteuliwa Katibu Mkuu 
Ofisi ya Makamu wa Rais.

Pia Rais Magufuli 
amemteua Mhandisi Angelina Madete kuwa Naibu Katibu Mkuu Katika Wizara ya 
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Mhandisi Angelina Madete anachukua nafasi 
iliyoachwa wazi na Dkt. Maria Sasabo aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya 
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano.

Aidha, Rais 
Magufuli amemteua Dkt. Aloyce K. Nzuki kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya 
Maliasili na Utalii.

Wakati 
huo huo, Rais Magufuli amemteua Bw. Christopher Ole 
Sendeka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe.Bw. Christopher 
Ole Sendeka anachukua nafasi ya Dkt. Rehema Nchimbi ambaye amehamishwa kituo 
cha kazi na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Dkt. Rehema 
Nchimbi anajaza nafasi iliyoachwa na Mhandisi Mathew Mtigumwe ambaye ameteuliwa 
kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo anayeshughulikia Kilimo.Katika 
hatua nyingine, Rais Magufuli amemteua Dkt. Osward
J. Mashindano kuwa Msajili wa Hazina. 

Dkt. Osward J. 
Mashindano anachukuwa nafasi ya 
Bw. Lawrence Mafuru ambaye atapangiwa kazi 
nyingine

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasilino ya Rais,
IKULU

Dar es Salaam

07 Desemba, 2016

JARIDA LA WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU TANZANIA (TFS) - ONLINE EDITION



Thursday, November 24, 2016

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AZUGUMZA NA VIONGOZI NA WATENDAJI WAKUU WA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao alichokiitisha kati yake na  Watendaji Wakuu wa  Wizara ya Maliasili na Utalii na Wakuu wa Mapori  ya Hifadhi za Mistitu, Ofisini kwake mjini Dodoma Novemba 21, 2016.  Kulia kwake ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kushoto kwake) na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe akizungumza katika Mkutano ulioitishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  Ofisini kwake mjiniDodoma Novemba 21, 2016.
  Baadhi ya Watendaji Wakuu  wa Wizara ya Maliasili na Utalii  wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao Ofisini kwake mjini Dodoma, Novemba 21, 2016.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe (kulia) na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (katikati) baada ya kuongoza kikao kati yake na Viongozi na Watendaji Wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisini kwake mjini Dodoma Novemba 21, 2016.
____________________________

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa miezi na siku tisa kwa Wakuu wa Mapori ya Hifadhi za Misitu kuhakikisha wanaweka mawe ya alama (beacons) kwenye mipaka yao ili kuepusha migogoro na wanavijiji wanaowazunguka.

Ametoa agizo hilo leo jioni (Jumatatu, Novemba 21, 2016) wakati akizungumza na Watendaji Wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Wakuu wa Mapori ya Hifadhi za Misitu nchini katika kikao alichokiitisha kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma.

“Tatizo la migogoro baina ya wafugaji, wakulima na kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya ni lazima lifanyiwe kazi. Mkitoka hapa rudini katika maeneo yenu mkawaambie wananchi mipaka yenu iko wapi. Ninyi mnatambua mipaka yenu iko wapi kwa hiyo waelewesheni wananchi kwa kuweka alama,” amesema.

“Wakati Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli akizindua bunge tarehe 20 Novemba, 2015 aliwapa maeneo makuu matatu ambayo ni kuanisha mipaka, kupambana na ujangili na kukusanya mapato. Alizungumzia suala la mipaka kwa sababu iliyopo haieleweki, mkiulizwa mnajibu kuna buffer zone. Hivi mwananchi wa kawaida anajua buffer zone ni nini?,” alihoji.

“Sasa ninawapa muda hadi Januari 31, 2017 kazi ya kuweka beacons kwenye hifadhi zote za misitu iwe imekamilika. Kila pori nenda mkatengeneze alama zenu kama TANROADS walivyofanya. Kaeni mpige hesabu ni kiasi gani cha saruji na kokoto kinahitajika. Tutarudi hapa Dodoma kupeana taarifa ya utekelezaji. Katibu Mkuu niletee taarifa ya kila mkoa na wilaya kuna mapori mangapi tutakutana hapahapa kupeana mrejesho,” alisisitiza.

Alisema kama TANROADS waliweza kuweka alama za barabarani kwa nchi nzima ni kwa nini Wizara ya Maliasili na Utalii imeshindwa kuchukua hatua kama hizo. “Ni lazima tuweke hizo alama kila katika pori lake, tusipofanya hivyo, migogoro hii itaendelea,” alisema.

“Nendeni mkaweke alama za mipaka mkishamaliza sasa muwaeleze wananchi ni umbali wanapaswa waache kutoka kwenye hizo alama zenu na muwaelimishe kwamba hiyo ndiyo buffer zone. Suala la beacons ni serious na ninatarajia nikute hizo beacons kwenye maeneo yenu”

“Kila mmoja anayo fursa ya kuitisha mkutano na wananchi na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kuwa na mapori ya akiba. Pandeni kwenye majukwaa, muelezee mipaka hiyo mipya na wananchi watawaelewa kwa sababu mwenye dhamana ya kwanza katika kutoa elimu hii ni wewe Mkuu wa Pori,” alisistiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuanzia leo Ofisi ya Rais TAMISEMI haina budi kusitisha usajili wa vijiji hadi zoezi la kuweka alama kwenye mipaka mapori ya hifadhi za misitu litakapokalimika.

“Kuanzia leo ninasimamisha zoezi la usajili wa vijiji unaofanywa na TAMISEMI hadi wizara ya Maliasili na Utalii ikamilikshe zoezi la kuainisha na kuweka alama kwenye mipaka mapori ya hifadhi za misitu. Tusipofanya hivyo tutaendelea kuwa na Taifa la walalamikaji,” alisema huku akishangiliwa na watendaji hao.

“Wakuu wa mapori tambueni ni vijiji vingapi ambavyo Serikali ilifanya makosa na kuvisajili wakati viko ndani ya hifadhi na vijiji vingapi bado havijasajiliwa. Pia onyesheni ni vijiji vingapi ambavyo ni hatarishi,” alisema.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemtaka Mkurugenzi wa Idara ya Utalii katika wizara hiyo, Bw. Zahoro Kimwaga pamoja na Bodi ya Utalii nchini wabadilike na kuanza kufanya kazi kibiashara zaidi.

“Mkurugenzi wa Utalii na Bodi yako ya Utalii bado hamjajitangaza vya kutosha. Promosheni ya utalii hapa nchini bado haitoshi na mgeweza kuoata mapato makubwa zaidi kwa kujitangaza. Mabango ya barabarani yamejaa matangazo ya Vodacom na Airtel badala ya kuwa na picha za wanyama ili kila mtu akiona atamani kwenda mbugani,” alisema.

“Tumieni mabango ya kieletroniki (electronic screens) kurusha picha za wanyama. Mfano pale nje ya uwanja wa Taifa, au uwanja wa ndege hata kwenye njia kuu  za mikoani wekeni mabango ya iana hiyo. Ombeni vipindi kwenye televisheni nyingine, kile cha TBC1 peke yake hakitoshi,” alisisitiza.

KUKUZA UCHUMI KUPITIA SEKTA YA UTALII KUNAHITAJI WAFANYAKAZI WENYE SIFA - MAGHEMBE

Waziri wa Maliasili na utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kulia) akisikiliza maelezo ya mmoja wa wahitimu wa mafuzo ya upishi katika hoteli za kitalii wakati wa mahafali ya sita ya Chuo cha Hoteli na Utalii Njuweni kilichopo Kibaha, mkoani Pwani hivi karibuni. 
_______________________________

Waziri wa Maliasili na utalii, Prof. Jumanne Maghembe amesema  ili Tanzania iendelelee kukuza uchumi kupitia sekta ya utalii inahitaji wafanyakazi wa kada hiyo  wawe na sifa zinazostahili ikiwemo nidhamu na uaminifu.


Ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya  6 ya Chuo cha Hotel na Utalii  cha Njuweni kilichoko  Kibaha mkoani Pwani ambayo yalifanyika kwenye viwanja vya Chuo hicho.

Alisema kuwa  pamoja na vyanzo mbalimbali vya mapato vinavyokuza uchumi wa taifa taifa,  Wizara ya Maliasili na Utalii ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi huo hivyo kinachotakiwa ni kuhakikisha watu wanaopewa dhamana ya kufanyakazi kwenye Wizara hiyo wanafanya kazi kwa weledi.

"Napenda kuwakumbusha kuwa nidhamu na uaminifu ndiyo siri itakayowawezesha ninyi kufika mbali katika utendaji wenu wa kazi, lakini mkiingiza tamaa na udokozi hamtafika mbali na badala yake mtalitia taifa kwenye sifa mbaya" alisema

Alisema kuwa Serikali imekuwa ikikuza uchumi wa nchi kila mwaka kupitia Sekta ya utalii ambapo idadi ya  watalii  imekuwa ikiongezeka kwa asilimia 23.7 kutoka watalii 867,994 mwaka 2011 hadi kufikia watalii 1,137,182 mwaka 2015. Aidha sekta hiyo inachangia asilimia 17 ya pato la taifa.

"Mapato yatokanayo na  shughuli za utalii yaliongezeka  kwa asilimia 28.8 kutoka dola za Marekani mil. 1,353.29 mwaka 2011 hadi kufikia dola za Marekani mil. 1,901.1 mwaka 2015" alisema

kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Nditi Rashid alisema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana kwa miaka kadhaa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho lakini bado kuna changamoto kadhaa zinazowakabili ikiwemo upungufu wa vifaa vya kisasa vya kuendeshea masomo ya TEHAMA

"kutokana na ufinyu wa bajeti tulionao tunakuomba mheshimiwa mgeni rasmi utusaidie kupata msaada wa vifaa vipya vitakavyotusaidia kuendesha masomo ya TEHAMA kwa ufanisi zaidi" alisema

Mahafari hayo ambayo ni ya sita tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 200o  yalihusisha jumla ya wanafunzi 350 waliohitimu kwa ngazi ya stashahada ambao walipata vyeti na zawadi mbalimbali .