slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Tuesday, January 17, 2017

KAMATI YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YATEMBELEA MAKAO MAKUU YA TTSA, TAWA NA TAFORI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizaya hiyo, Meja Generali Gaudence Milanzi (kushoto) wakiwakaribisha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii walipowasili katika ofisi za Wakala ya Miti za Mbegu Tanzania (TTSA) mjini Morogoro jana kwa ajili ya kuona kazi na miradi ya wakala huyo. Kushoto ni wajumbe wa kamati hiyo, Silafi Maufi ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa na Godwin Molel (wa pili kushoto), Mbunge wa jimbo la Siha.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta Nditiye (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Mohammed Kilongo alipowasili na kamati yake katika ofisi za Wakala wa Miti za Mbegu Tanzania mkoani Morogoro jana. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Wizara ya Maliasili na Utalii, Marry Faini na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Dkt. Ezekiel Mwakalukwa (wa pili kulia).
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akiwakaribisha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii katika ofisi za makao makuu ya Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA). Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhandisi Atashasta Nditiye.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA), Edigar Masunga (wa pili kulia) akiwasilisha taarifa ya wakala huyo kwa Kamati ya Bunge ya Ardhi ya Maliasili na Utalii mkoani Morogoro jana. Alisema wakala huyo huzalisha aina 195 za mbegu, kati ya hizo asilimia 60 ni miti ya kienyeji na asilimia 40 ni miti ya kigeni. Kushoto ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe na kulia kwake ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta Nditiye.
Katibu Mkuu wa Wizaya ya Maliasili na Utalii, Meja Generali Gaudence Milanzi (kulia) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Aloyce Nzuki wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA), Edigar Masunga kwa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii mkoani Morogoro jana. Meja Generali Milanzi alisema Ujangili nchini kwa sasa umepungua kutokana na kasi ya udhibiti wa vitendo hivyo inayofanywa na askari wa wanyamapori kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama. Alisema nyara nyingi zinazokamatwa kwas sasa ni zile za zamani na kwamba uamuzi wa China kuzuia biashara ya meno ya tembo utasaidia kupunguza zaidi ujangili nchini.
Mtaalam wa Baiolojia ya mbegu wa Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania, Fandey Mashimba (kulia) akitoa ufafanuzi wa namna ya uaandaaji wa mbegu na miche ya miti kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii walipotembelea wakala huyo jana Mkoani Morogoro kwa ajili ya kuona shughuli na miradi ya wakala huyo. Kushoto ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe.
Meneja wa Kanda ya Mashariki na Kati wa Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania, Frida Mngulwi (kulia) akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii namna mashine za kuandaa mbegu za miti zinavyofanya kazi. Wa pili kushoto ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe.
 Wajumbe wa Kamati ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii wakikagua vitalu vya miche ya miti vya wakala wa mbegu za miti Tanzania (TTSA) walipotembelea makao makuu ya wakala huyo mkoani Morogoro jana.
 Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA), Edigar Masunga (mbele kushoto) akiongoza wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kukaga shamba la miti la wakala huyo mkoani Morogoro jana. 
Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Mohammed Kilongo (kulia) akifafanua jambo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kulia) wakati wa kukagua shamba la miti la Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA) mkoani Morogoro jana.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Laurence Mbwambo (kushoto) akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii namna taasisi hiyo ilivyojipanga kuendesha tafiti zake na kuhifadhi taarifa za utafiti kwa njia ya mtandao.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akisistiza jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii walipotembelea ofisi za Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) mkoani Morogoro jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wanne kushoto) akitoa maelezo ya mtandao (kulia) wa kugundua matukio ya moto kwenye maeneo ya misitu nchini unavyofanya kazi kwa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Mtambo huo upo chini ya usimamizi na utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI).
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Martin Laibooki akiwasilisha taarifa ya mamlaka hiyo kwa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilipotembelea makao makuu ya mamlaka hiyo mkoani Morogoro jana. Katika taarifa yake ameeleza kuwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Agosti 2016 mamlaka hiyo ilitoa jumla ya shilingi bilioni 2.2 kama faida ya mgao wa mapato ya utalii kwa Halmashauri za Wilaya, vijiji pamoja na Jumuiya za Uhifadhi wa Wanyamapori nchini (WMAs). Hata hivyo alisema changamoto kubwa ya mamlaka hiyo kwenye uhifadhi kwa sasa ni uvamizi wa mifugo ndani ya maeneo ya hifadhi.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utali, Dkt. Aloyce Nzuki (kulia) akiteta jambo na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara hiyo, Dkt. Ezekiel Mwakalukwa wakati kamati ya bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii ilipotembelea makao makuu ya TAFORI NA TAWA mkoani Morogoro jana.

Picha ya pamoja ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania na Taasisi ya Utafiri wa Misitu Tanzania (TAFORI).
Mtaalamu wa maabara wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) akieleza namna tafiti za misitu zinavyofanywa kwenye maabara ya taasisi hiyo kwa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) wakiwa kwenye mkutano wa kamati hiyo ya bunge.

Friday, January 13, 2017

NAIBU WAZIRI MAKANI ALIVYOPANIA KUMALIZA MGOGORO ULIODUMU ZAIDI YA MIAKA 25 LOLIONDO

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kushoto) akioneshwa Ramani ya Kijiji cha Ololosokwan na Diwani wa Kata hiyo, Yanick Ndoinyo alipotembelea kijiji hicho hivi karibuni kuona changamoto za uhifadhi. Kulia ni Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Ololosokwan, Emmanuel Salteimoi. 
Kundi la mifugo likiwa ndani ya Pori Tengefu la Loliondo, karibu kabisa na mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akizungumza katika kikao cha wadau wa mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo alichokiitisha katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Tarafa ya Loliondo mkoani Arusha hivi karibuni.

NA HAMZA TEMBA - WMU
............................................................................

Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli mara tu ilipoingia madarakani mwezi Oktoba mwaka juzi ilitoa vipaombele vyake kadhaa vya kutelezwa na wizara zake mbalimbali huku Wizara ya Maliasili na Utalii ikikabidhiwa majukumu mazito matatu ya kutekeleza katika kipindi cha uongozi wake. 


Majukumu hayo yaliyotolewa na Rais Magufuli wakati wa hotuba yake ya kwanza ya kulihutubia bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, ni yale ya kuhakikisha kuwa wizara hiyo inakomesha vitendo vya ujangili, kuongeza mapato ya serikali na kushuulikia utatuzi wa migogoro ya mipaka kwenye maeneo ya hifadhi nchini. 

Wizara ya Maliasili na Utalii, imesema kuwa imejipanga kuhakikisha kuwa malengo yake ya uhifadhi wa Maliasili, Malikale na Kuendeleza Utalii pamoja na utekelezaji wa vipaombele ilivyopewa na Serikali ya awamu ya tano kuwezesha kufikia malengo hayo yanatimia kwa wakati.

Kwa upande wa utatauzi wa migogoro kwenye maeneo ya hifadhi nchini, Wizara hiyo imejipanga kuwashirikisha wadau wote wanaohusika na migogoro hiyo kwa kukaa nao pamoja kwenye vikao vya majadiliano na kuweka mikakati ya pamoja ya kufikia suluhu ya migogoro hiyo kwa faida ya Serikali na wadau wote wanaohusika.

Hivi karibuni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani alifanya ziara ya kiutafiti katika Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Pori Tengefu la Liliondo, lengo kuu la ziara hiyo ikiwa ni kuona uhalisia wa changamoto zilizopo pamoja na kupata taarifa sahihi kutoka kwa wadau husika, alifanya hivyo bila ya kujitambulisha kwa lengo la kupata taarifa sahihi kuhusiana na migogoro hiyo.

Akiwa katika Tarafa ya Loliondo alitembelea kijiji cha Ololosokwan, Pori Tengefu la Liliondo, sehemu ya mpaka wake na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na eneo la muwekezaji, kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC) na kampuni ya &Beyond (Kleins Camp).


Akiwa katika eneo hilo alizungumza na viongozi wa kijiji cha Ololosokwan ambao waliwasilisha changamoto kadhaa ikiwemo ongezeko la mifugo kutoka nchini Kenya na vijiji jirani hususani wakati wa kiangazi kwa ajili ya kutafuta malisho na uelewa tofauti wa mpaka baina ya vijiji na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Diwani wa Ololososkwan, Yanick Ndoinyo alisema uhifadhi umekuwa ukiwanufaisha kwa kiasi kikubwa kwa kuwa kupitia utalii kijiji hicho hupata fedha taslim zaidi ya shilingi milioni 300 kwa mwaka kupitia mikataba ya wawekezaji na mgao kutoka Serikalini.

Pamoja na mchango huo amesema “wawekezaji wa eneo hili wamekuwa wakitekeleza miradi ya jamii ambapo wamechimba visima vinne, wamejenga madarasa mawili na kisima kingine kinajengwa jirani na kata hii, lakini kampuni zote kwa ujumla zinatoa ajira kwa wanavijiji, kwahiyo kwakweli sisi ni kijiji ambacho tumeona manufaa ya utalii “

Ndoinyo alisema fedha hizo zimekuwa zikisaidia kusomesha watoto masikini kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu, kusaidia ujenzi wa zahanati na huduma nyingine za jamii.

Kwa upande wa kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC) ambao wamewekeza katika pori hilo kupitia Afisa Mahusiano wao, William Parmat walisema changamoto kubwa inayowakabili ni ya wananchi kuingiza mifugo katika eneo la uwekezaji jambo linalosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo wanyamapori kutoweka.

Muwekezaji huyo alisema wapo tayari kuweka makubaliano ya uhifadhi na wananchi pamoja na kusaidia kujenga miundombinu ya huduma za jamii. Alisema changamoto ya mifugo imesababishwa na msukumo wa baadhi ya asasi za kiraia kwa wananchi kwamba Serikali inataka kuchukua pori hilo hivyo waingize mifugo yao kwa ajili ya kulilinda.

Naibu Waziri Makani aliuahidi uongozi wa kijiji cha Ololosokwan pamoja na wawekezaji hao kuwakutanisha wadau wote wanaohusika na mgogoro wa pori hilo kwa ajili kujadili changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.


Akiwa kwenye Pori Tengefu la Loliondo na kwenye mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti alishuhudia makundi ya mifugo ikiwa ndani ya pori hilo na mingine ikizagaa maeneo ya mpakani na Hifadhi hiyo. Alielezwa na Viongozi wa Wilaya ya Ngorongoro kuwa, mifugo hiyo huingizwa kwa ajili ya malisho wakati wa usiku kwenye hifadhi ya Serengeti. 

Inaelezwa kuwa eneo la Pori Tengefu la Loliondo lina umuhimu wa pekee katika uhifadhi kwa sababu ni sehemu ya mazalia ya wanyamapori, mapito ya wanyamapori na vyanzo vya maji. Kutokana na sababu hizo, eneo hilo linapaswa kuendelea kuhifadhiwa ipasavyo, kwa kuwa linachangia kwa kiwango kikubwa kuimarisha mfumo wa ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti.

Siku chache baada ya ziara hiyo ya kiutafiti, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara ya kikazi mkoani Arusha na kuwaagiza viongozi wa Serikali kukaa pamoja na wadau wanaohusika na migogoro ya ardhi katika Tarafa ya Loliondo na kuitafutia suluhu ya kudumu.

Baada ziara hiyo ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri Makani aliendelea na ziara yake katika tarafa ya Loliondo ambayo aliikatisha kupisha ziara Waziri Mkuu. Mara hii ziara hiyo ikihusisha pia ufuatiliaji wa maagizo ya Waziri Mkuu aliyoyatoa kwenye ziara yake mkoani Arusha.

Aliwasili Loliondo kwa ajili ya kuweka mkakati wa kumaliza changamoto ya mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 25 kati ya mwekezaji, wanavijiji, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), suala la mifugo, uharibifu wa mazingira na utata wa mpaka wa Hifadhi ya Serengeti na Loliondo.  

Tarehe 29 Desemba, 2016 alifanya mkutano na wadau wanaohusika moja kwa moja na mgogoro wa Loliondo, mkutano huo ulifanyika katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Tarafa ya Loliondo, Kupitia mkutano huo aliunda kamati maalum ya kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro huo.

Kamati hiyo inahusisha taasisi za serikali, asasi za kiraia, viongozi wa dini, wazee wa kimila (Leigwanan), viongozi wa vijiji, wajumbe wa kamati teule ya vijiji 15 ya mpango bora wa matumizi ya ardhi na uendelezaji wa uhifadhi na wawakilishi wa wanawake na vijana. Aliunda pia kamati ya kuandaa kanuni za kundesha vikao vya kamati hiyo.

Naibu Waziri huyo aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Rashid Mfaume Taka akateuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.  

“Kamati ya kanuni itumie muda wa wiki mbili hadi kufikia tarehe 17 Januari, 2017 iwe imeshakamilisha rasimu ya kanuni ili tarehe 18 Januari, 2017 tuzipitie, tuzijadili na kuzipitisha. Hatua itakayofuata ni mawasilisho ya taarifa mbalimbali kutoka kwa wadau pamoja na majadiliano”, alisema Makani.

Aliagiza pia taarifa mbalimbali za kamati zilizowahi kushuulikia mgogoro huo miaka ya nyuma na mapendekezo yake pamoja na taarifa mbalimbali za sheria za uhifadhi na vijiji kwa ajili ya kusaidia majadiliano hayo ziwasilishwe.

Kikao hicho kilikubaliana kazi hiyo ifanyike ndani ya miezi mitatu hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2017 iwe imekamilika na muafaka upatikane kwa ajili ya kuishauri Serikali namna bora ya kumaliza mgogoro huo.

Wadau wote walikubaliana kushiriki vikao vya majadiliano huku wengine wakipongeza hatua iliyofikiwa na Serikali ya kutaka kumaliza mgogoro huo, hata hivyo Naibu Waziri Makani alitoa angalizo kwa wadau hao; "Kuna watu humu ndani na hata nje ambao hawataki tumalize migogoro Loliondo, nitoe rai kwao, waache chokochoko.

“Wafikishiwe salamu, tutawabaini, tutawakamata na kuwashitaki kwa kosa la kukwamisha jitihada za Serikali kuwaletea wananchi maendeleo yao, Wananchi muone umuhimu wa jitihada za Serikali kumaliza changamoto hii na kutuunga mkono”, alisema Makani.

Akizungumza katika mkutano huo, mchangiaji mmoja ambaye hakutambulisha jina lake alisema “Eneo hili Loliondo lenye kata saba na vijiji 15 lilikosekana dawati la pamoja, kwa mfumo huu tutaenda mbele, Taasisi nyingi zimekuwa zikipotosha umma kuhusiana na taarifa za Loliondo, tutashukuru kuona tunapata muafaka kupitia kamati hii iliyoundwa leo”

Changamoto ya Mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo ni mkwamo kwa maendeleo ya wananchi wa Loliondo na Taifa kwa ujumla, Kila mwananchi wa Loliondo ana nafasi kubwa  ya kuhakikisha mgogoro huu unafikia tamati kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine. Kila mmoja atimize wajibu wake mgogoro huu utakuwa historia na Loliondo itakua salama na kupiga hatua kimaendeleo. 

Thursday, January 12, 2017

TO SEE THIS, VISIT OUR NATIONAL PARKS..........

Image may contain: outdoor
Ushawahi kuona vita ya swala dume? Ona hapa namna wanavyokung'utana kisa majike! "An epic clash between two rams"
Image may contain: outdoor and nature
Image may contain: grass, outdoor and nature
Image may contain: outdoor and nature

UJANGILI NCHINI UMEPUNGUA - MEJA JENERALI MILANZI

Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akihutubia kikao cha mafunzo ya siku tano kwa watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) na wakuu wa mapori ya akiba kilichofanyika Morogoro hivi karibuni.
 Picha ya pamoja.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (Kushoto) akiteta jambo na Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP), Biswalo Mganga (wa pili kushoto) mara baada ya kufungua mkutano wa siku tano wa watendaji wakuu wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) na wakuu wa mapori ya akiba kilichofanyika Morogoro hivi karibuni. Kulia ni Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki.

..........................................................
WIZARA ya Maliasili na Utalii, imesema vitendo vya ujangili nchini vimepungua kwa mwaka uliopita ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Hali hiyo imetokana na kuwapo kwa ushirikiano wa vyombo vya ulinzi na usalama, mamlaka husika na wananchi katika kutoa taarifa na kufanikisha kukamatwa wahalifu wa ujangili wa tembo.
Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Gaudence Milanzi hivi karibuni mjini Morogoro, alipotoa hotuba yake ya kufungua kikao cha mafunzo ya siku tano kwa watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) na wakuu wa mapori ya akiba.
Alisema, ujangili umepungua na ukamataji wa meno ya tembo unaofanyika kwa hivi sasa unatokana na ujangili wa zamani ambayo baadhi ya wahalifu huo walikuwa wameyahifadhi kwa ajili ya usafirishaji kwenda katika masoko.
“Watu watasema, mbona ukamataji wa meno ya tembo unaendelea endapo ujangili umepungua? Meno haya ni yaliyokuwa yamehifadhiwa kwa kitambo na yanakuwa katika njia ya usafirishaji kwenda nje ya nchi na si meno mapya ya tembo,” alifafanua Milanzi.
Hata hivyo, alisema licha ya kupungua kwa ujangili tofauti na miaka ya nyuma, lakini bado unaendelea kufanyika kwa kiwango kidogo na kutokana na hali hiyo juhudi za pamoja zinahitajika katika suala la ukamataji na udhibiti kwenye maeneo ya hifadhi za taifa.
Alisema, “kazi ya sasa kwa mamlaka kwa kushirikiana na nyingine ni kazi ya kuhakikisha majangili hawawezi tena kuingia ndani ya mapori ya hifadhi kwa ajili ya kuua wanyamapori hasa tembo. Na hii itasaidia kukomesha biashara hii haramu,” alisema Milanzi.
Katibu Mkuu huyo aliwataka watendaji wa mamlaka hiyo na nyingine zinazosimamia rasilimali za hifadhi za wanyamapori kuongeza nguvu katika vita dhidi ya ujangili kwani mafanikio ya serikali yameanza kuonekana katika suala zima la mapambano ya vita vya ujangili.
Katika hatua nyingine ameipongeza Serikali ya China kwa kufunga biashara ya meno ya tembo nchini humo na kusema kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza na kumaliza kabisa vitendo vya ujangili nchini.
Kwa upande wake Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP), Biswalo Mganga amesema watuhmiwa 200 walikamatwa katika kipindi cha mwaka jana kutokana makosa ya kukutwa na nyara mbali mbali za Serikali na kushtakiwa.
Alisema zaidi ya shilingi milioni 800 hadi 900 zilipatikana kutokana na faini walizotozwa na walioshindwa kulipa faini walifungwa kifungo cha miaka 20 hadi 25. "Endapo wote wangefanikiwa kulipa faini kiasi cha shilingi bililioni 164 zingekusanywa" .
Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Hamis Semfuko, kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu alisema kuwa ujangili, uharibifu wa mazingira na uvamizi wa mifugo na kujenga makazi ndani ya mapori ya hifadhi ya akiba ni mkubwa na mifugo mingi inatoka nje ya Tanzania.

Thursday, January 5, 2017

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAOKOA WAFUGAJI 50 WALIOKUWA WAKIPITISHA MIFUGO YAO NDANI YA PORI LA AKIBA LA SELOUS

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence  Milanzi (katikati) akipata taarifa kutoka kwa  Meneja wa Pori la Akiba la Selous,  Enock Msocha (wa tatu kushoto)  mara baada ya  kuwasili kwa ajili ya kuwatembelea  Wafugaji 50 waliokolewa na Askari wanyamapori baada ya kutelekezwa  na mtu mmoja waliyemtaja kwa  jina la Mzigua. ( Picha na Lusungu Helela-Wizara ya Maliasili na Utalii)
lus1
  Baadhi wa Wafugaji wakiwa wanakunywa maji na juisi walizopelekewa kama msaada baada ya kuokolewa na Askari wanyamapori wa Pori la Akiba la Selous,  Kanda ya Kaskazini Mashariki  Kingupira  baada ya kutelekezwa kwa muda wa  siku tano na mtu mmoja waliyemtaja kwa  jina maarufu la Mzigua aliyewarubuni kwa kuwaonyesha njia za mkato ndani ya Pori hilo ( Picha na Lusungu Helela-Wizara ya Maliasili na Utalii) 

NA LUSUNGU HELELA - WMU
.................................................................
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Askari wa Wanyamapori wa Pori la Akiba la Selous, Kanda ya Kaskazini Mashariki  Kingupira imewaokoa wafugaji 50 waliokuwa wakiwapitisha jumla ya ng’ombe 1780, kondoo  200 na punda 6  baada ya kutelekezwa kwa muda wa  siku tano na mtu mmoja aliyetajwa kwa  jina  la Mzigua aliyewarubuni kwa kuwaonyesha njia za mkato ndani ya Pori hilo wao bila kujua na kuamua kuwakimbia.
Bw. Lisasi Cherehani ambaye ni mmoja wa wafugaji hao alisema ‘’tulimpa Mzigua kiasi cha zaidi ya shilingi 5,000,000 kutoka kwa wafugaji  kama malipo ya kutufikisha eneo la Ilonga mkoani Morogoro tukitokea vijiji vya Ndundunyekanza, Kipungila  na Chumbi vilivyopo wilayani Rufiji mkoani Pwani kwa makubaliano  kuwa  atatupitisha  njia fupi ya mkato tutakayotembea kwa muda wa siku tano tu, hatukujua anatutupitisha ndani ya pori hili. ‘’
Baada ya kutelekezwa,  wafugaji hao ambao walikuwa katika hali mbaya waliomba msaada kwa ndugu zao  ambao waliwasiliana na Uongozi wa Pori la Akiba la Selous ambao kwa haraka walifanya jitihada za kuokoa maisha yao  ikiwa ni kuwapa huduma ya kwanza,  maji, uji pamoja na kuwakimbiza hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence  Milanzi aliwatembelea wafugaji hao jana kwa ajili ya  kuwapa pole na kuwapelekea  chakula yakiwemo maji pamoja na  unga.
Aidha, Milanzi  aliagiza Wafugaji hao  waachiwe huku akitoa wito kwa wananchi kuacha kupita maeneo ya Hifadhi kwa vile ni kosa kisheria na wale wote watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria na kuahidi kuwa mtu huyo aliyewa danganya kwa  kuwapitisha ndani ya Hifadhi hiyo ni lazima akamatwe kwa udi na uvumba.
‘’Sisi kama Serikali kitu cha kwanza ni ubinadamu tumewahudumia  na  hivyo natoa tamko la kuwaachia wafugaji wote waliopotea ndani ya Pori hili kwa vile mateso  waliyoyapata na mali waliyoipoteza ni kubwa sana  baada ya kudanganywa kwa na kupitishwa ndani ya Pori la Akiba la Selous.’’ Alisema Milanzi
Mmoja wa  wafugaji aliyekuwa katika msafara huo na aliyekuwa akiwasiliana kwa njia ya simu  , Bw. Lisesi Cherehani akielezea namna walivyotelekezwa  katika pori hilo,  alisema kuwa walianza safari hiyo  siku ya jumatano ambapo walikuwa wakitembea usiku na mchana  kwa muda w siku tano bila kujua wanapitishwa ndani ya Hifadhi hiyo ndipo wakaanza kushikwa na kiu kwa vile maji waliyokuwa nayo yaliwaishia na kila walipokuwa wakijaribu kumuuliza aliyewapitisha njia hiyo alikuwa akiwambia baada muda mfupi watakutana na maji hata hivyo waliendelea na safari bila mafanikio ndipo walipoanza kuanguka na baadhi ya wafugaji walianza kunywa mikojo yao pamoja na damu za kondoo kwa ajili ya kuokoa maisha yao.
Aliongeza kuwa, wasingekuwa Askari wanyamapori ambao walikuja kuwapa msaada wa kibinadamu kwa kuwapatia maji pamoja na kuwanyesha uji wangeweza kufa wote.‘’Nawashukuru sana askari wanyamapori kwa kutuhudumia bila wao leo hii msingemkuta mtu yeyote hapa tungekuwa tayari tumeshakufa.’’ Alisema Bw. Cherehani.
Mfugaji mwingine, Mbaga Mahila aliwashukuru sana Askari wanyampori  kwa utu waliouonesha tokea mwanzo walipowaokoa hadi hapo walipofikia na kuitaka jamii ibadilishe mtazamo wa kuwaona askari wanyamapori kama watu katili jambo ambalo halina ukweli wowote.
Pia, Masanje Hambe aliiomba Serikali iwasamehe kwa kuwa wametambaua  kosa la kuingia ndani ya Pori la Akiba la Selous kinyume cha sheria lakini hata hivyo hawakujua kuwa wanapitishwa ndani ya hifadhi hiyo.
Awali,  Mkuu wa Kanda ya Mashariki Kingupira, Bw. Paschal Mrina alisema wamepata  taarifa za wafugaji hao kutoka kwa Wasamaria wema na Uongozi wa wilaya ya Rufiji kuwa  kuna wafugaji  wamepotelea ndani ya hifadhi hiyo  na kwa bahati nzuri kulikuwa na mfugaji mmoja aliyekuwa na simu ndipo wakaanza kuwasiliana naye na kuunda kikosi maalum cha doria kwa ajili ya kuwaokoa.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kanda hiyo alisema  wamefanikiwa kuwaokoa wafugaji wote na  ilionekana mizoga saba na wengine ambao hawakuonekana taratibu za kuanza kutafuta zimeandaliwa  
Alielezea njia walizotumia kuokoa wafugaji hao ni kuwa waliunda vikosi vitatu vya doria ambapo kikosi cha kwanza kilifanya doria kwa njia za miguu, kikosi cha pili kilfanya doria kwa njia za magari na kikosi cha tatu kilifanya doria  kwa kutumia ndege kwa ajili ya kubaini walipo.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wafugaji, Bw. Magembe Makoye alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuacha kuwafukuza wafugaji katika maeneo waliyopo badala yake  wawatafutie maeneo mbadala ili kuthibiti matukio kama hayo ambayo yamepelekea hasara na mateso makubwa kwa wafugaji.
Pori la Akiba la Selous lina ukubwa wa kilomita za mraba 50,000 na limegawanywa katika kanda nane huku Kanda ya Mashariki  Kipungira ikiwa moja kati  ya kanda kubwa yenye kilomita za mraba 7,650, Shughuli zinazofanyika  katika Pori hilo ni Utalii wa picha na pamoja na uwindaji

PUBLIC NOTICE: GRADING OR RE-GRADING OF ACCOMMODATION FACILITIES IN DAR ES SALAAM REGION (PHASE I)

The United Republic of Tanzania
MINISTRY OF NATURAL RESOURCES AND TOURISM
NOTICE FOR GRADING OR RE-GRADING OF ACCOMMODATION 
FACILITIES IN DAR ES SALAAM REGION (PHASE I)

All owners and operators of accommodation facilities in Dar es Salaam Region are hereby notified that the Ministry of Natural Resources and Tourism shall conduct Grading/Re-grading of all designated accommodation facilities in Dar es Salaam Region. To this effect, the Ministry gives thirty (30) days notice, from the date of issuance of this notice, for the owners and operators of accommodation facilities in Dar es Salaam Region to make the necessary preparations for a smooth and efficient run of the ensuing exercise.

The Criteria for Grading, and the list of accommodation facilities scheduled for grading/re-grading in this Phase 1 for 2017, are available HERE also available at www.tanzaniatourism.go.tz and www.tourismcollege.go.tz. 
.
This notice is given in consideration of Sections 10 (3), 17, 53 (1) (b) and (c), 46 (1) (a) and (f) of the Tourism Act, No. 29 of 2008; and Regulation 5 of the Tourism (Fees and Charges) of 2015 (GN.267).


Issued by:
PERMANENT SECRETARY
MINISTRY OF NATURAL RESOURCES AND TOURISM
MPINGO HOUSE – 40 JULIUS NYERERE ROAD
15472 – DAR ES SALAAM
TEL: +255 22 2864271/ 2864230


6 JANUARY, 2017

To  access the Criteria and List of accomodation click the link FOLLOW ME below;

Sunday, January 1, 2017

SERIKALI KULIPA DENI LA WALIOTHIRIKA NA WANYAMAPORI - MHANDISI MAKANI

Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akikagua moja ya shamba la mahindi lililoharibiwa na tembo katika kijiji cha Kunzugu, wilaya ya Bunda Mkoani Mara jana  wakati wa ziara yake ya kuangalia changamoto za uhifadhi mkoani humo. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili. 
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kulia) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kunzugu, wilaya ya Bunda, mkoani Mara jana alipotembelea moja ya shamba la mahindi lilioharibiwa na tembo wakati wa ziara yake ya kuangalia changamoto za uhifadhi mkoani humo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akiangalia nyumba iliyoangushwa na tembo katika kijiji cha Makundusi, wilaya ya Serengeti, mkoani Mara jana wakati wa ziara yake ya kuangalia changamoto za uhifadhi mkoani humo. Nyuma yake ni Mbunge wa Serengeti, Marwa Ryoba Chacha. 

NA HAMZA TEMBA - WMU
.......................................................

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema italipa madeni yote ya miaka ya nyuma ya vifuta jasho na vifuta machozi ambayo inadaiwa na wananchi waliokubwa na vitendo vya uharibifu wa wanyamapori nchini kabla ya bunge lijalo la bajeti, madeni hayo ni yale ambayo yameshaifikia wizara hiyo na kuhakikiwa. 

Akizungumza jana na uongozi wa wilaya ya Bunda wakati wa kuhitimisha ziara yake ya siku moja ya kufuatilia changamoto za uhifadhi wilayani humo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhandisi Ramo Makani amesema uamuzi huo wa Serikali utaondoa kilio cha muda mrefu cha wananchi ambao wamepata madhara mbalimbali ya wanyamapori ikiwemo vifo, majeruhi, kuliwa mazao na kuharibiwa mashamba yao. 

"Serikali ya awamu ya tano imeshakamilisha takwimu za madai, yale yote tunayodaiwa huko nyuma, yaliyoifikia Wizara yakafanyiwa uhakiki na nimesema kwenye uhakiki huo ndani ya kipindi cha miaka kumi, kwa wilaya zaidi kidogo ya 80 ambazo ndizo zina changamoto hizi kwa kiwango kikuu, deni jumla ni shilingi 2,081,532,700 (bil. 2.9)", amesema. 

Amesema wilaya ambazo zimeathirika zaidi na vitendo hivyo na ambazo madai yao ni makubwa zaidi ya Wilaya zingine ni Serengeti na Bunda ambazo ziko mkoani Mara na zinapakana na Hifadhi ya taifa ya Serengeti, Ziwa Victoria, Pori la Akiba Grumeti na Ikorongo. "Serengeti ndiyo inayoongooza kwa madai hayo, shilingi milioni 408,547,600 alafu Bunda shilingi milioni 265,969,750",. 

Pamoja na Serikali kujiwekea utaratibu huo na wananchi wa kulipa vifuta jasho na vifuta machozi kwa waathirika, amesema ipo haja ya kutafuta njia endelevu ya kukabiliana na changamoto hizo na fedha ambayo ingetumika kulipia fidia hizo ikatumika kuwezesha mpango huo endelevu. Amesema mpango huo utawezekana kwa kuwashirikisha wananchi.

"Mpango endelevu wa kukabiliana na changamoto hiyo ni ule wa ushiriki wa pamoja wa Serikali na wananchi katika kukabiliana na vitendo vya uharibifu dhidi ya wanyamapori", amesema. 

Ili kufanikisha mpango huo ameuagiza uongozi wa wilaya ya Bunda na Serengeti kuratibu ushiriki wa wananchi wao katika zoezi hilo kwa kuunda vikundi shirikishi katika kila kijiji, kubaini mahitaji yake ikiwemo vifaa na kuwasilisha taarifa hiyo wizarani kabla ya tarehe 15 januari mwaka huu, kwa ajili ya hatua zaidi za kufanikisha mpango huo. 

Amesema ushirikiano huo pekee hautoshi kukabiliana na changamoto hizo kama wananchi nao hawataipunguzia mzigo serikali wa kupambana na vitendo vyao viovu dhidi ya uhifadhi, ili nguvu hiyo itumike katika kushirikiana nao kwenye ulinzi dhidi ya wanyama waharibifu. "Wananchi waache vitendo viovu dhidi ya uhifadhi, ujangili, kuua wanyamapori",. 

Ameeleza kuwa miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa changamoto hizo ni matokeo ya tabia za wananchi kusogelea maeneo ya hifadhi kwa ajili ya shughuli za kibinadamu, jambo ambalo lina athari kubwa katika uhifadhi na usalama wa wananchi wenyewe, hivyo ni lazima liepukwe.

"Njia ambayo tembo alikua akipita miaka 20, 30, 40 ndo anapita kila siku, sisi tumeenda kujenga, tumeenda kulima mashamba, sasa tembo wao na wenyewe wana ownership (umiliki), ile njia wao wanaona ni ya kwao tu, kwahiyo akikutana na wewe anafanya hayo anayoyafanya, hata kwenda kukaa kufanya shughuli za kibinaadamu ikiwemo kujenga na kulima jirani kabisa na kwenye mpaka ya hifadhi na yenyewe ni tatizo". 


Naibu Waziri Makani amehitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Mara jana ambapo alitembelea vijiji kadhaa wilayani Bunda na Serengeti na kushudia athari mbalimbali za uharibifu wa wanyamapori pamoja na kupokea malalamiko mbalimbali ya uharibifu huo kutoka kwa wananchi. Alishuhudia mashamba kadhaa ya mahindi yaliyokuwa karibu na maeneo ya hifadhi yakiwa yameharibiwa na tembo.