slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Thursday, January 25, 2018

DK. KIGWANGALLA ATAJA ORODHA YA WATUHUMIWA WA UJANGILI LEO MJINI DODOMA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara hiyo Mjini Dodoma leo. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Aloyce Nzuki.

Na Hamza Temba - Dodoma
.........................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla leo Januari 25, 2018 mjini Dodoma ametaja majina ya watuhumiwa wa ujangili ambao wengi wao ni wamiliki na washirika wa Kampuni za uwindaji wa kitalii na kuwapa siku saba wawe wamefika kwa hiari yao wenyewe katika ofisi za Wizara hiyo Mjini Dodoma, Swagaswaga House kwa ajili kutoa maelezo kwanini wasichukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kujibu tuhuma hiyo na nyingine nyingi zinazowakabili mbele ya kamati atakayoiunda.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Dk. Kigwangalla ametaja baadhi ya tuhuma hizo ambazo ziko kinyume cha sheria na taratibu za uwindaji wa kitalii kuwa ni uwindaji haramu, uhawilishaji wa umiliki wa vitalu vya uwindaji pasipo kufuata sheria, udanganyifu kwenye kujaza fomu za uangalizi,  rushwa, uhalifu dhidi ya rasilimali za wanyamapori na uhujumu uchumi.

Alitaja tuhuma zingine kuwa ni ukiukwaji wa kanuni za uwindaji (kupiga wanyama usiku, kuwinda wanyama bila kujali umri, kupiga wanyama nje ya maeneo waliyopewa), kukutolipa tozo mbalimbali za maendeleo za jamii kwenye vijiji jirani na maeneo wanaoendesha biashara ya uwindaji, kushindwa kuendesha ipasavyo shughuli za kuzuia ujangili.

Dk. Kigwangalla aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni ndugu Pasanis na wenzake ambao wanamilikia kampuni ya Berlette Safari Corporation Ltd na Ngugu Shein Ralgi na wakurugenzi wenzake wa kampuni ya Game Frontiers of Tanzania Ltd.

Wengine ni Ndugu Howel na wakurugenzi wenzake wa kampuni ya Mkwawa Hunting Sfaris Tanzania Ltd, Ndugu Thomas Fredikin na wenzake wa Kampuni ya Mwiba Holdings Ltd, Wengert Windrose Safaris Tanzania  Ltd na Tanzania Game Trackers Safaris Ltd, na Ndugu Awadh na wenzake ambao wanamiliki kampuni ya Uwindaji wa Greenmiles Safaris Ltd.

Aliwataja washirika wengine kuwa ni Ndugu ni Kwizema, Ndugu Robert, Ndugu Solomon Makulu, Ndugu Siasa Shaban, Ndugu Hamis Abdul Ligagabile na mtumishi wa Wizara Wizara ya Maliasili na Utalii, Alex Aguma.

Katika hatua nyingine Dk. Kigwangalla ametoa Ilani ya siku 30 kwa watu mbalimbali ikiwemo Mawaziri Wakuu Wastaafu waliovamia kiwanja chenye hati namba 4091 kilichopo Njiro Jijini Arusha wafike kwa Kamishna Mkuu wa Ardhi waweze kuhakikiwa na kuthibitisha umiliki wao halali ama sivyo wavirejeshe Serikalini viweze kumilikishwa kwa mmiliki wake halali.

“Natoa ilani ya siku 30 kwa mtu yeyote ambaye anajua alivamia kiwanja katika eneo hili ambalo lina hati namba 4091 kilichopo Njiro, Arusha, haraka sana ajipange kupeleka taarifa zake mbele ya Kamishna wa Ardhi kabla hatujachukua hatua nyingine za kisheria, hati iliyoko pale ipo katika jina la Bodi ya Utalii Tanzania japo wao wanadai wana hati nyingine.

“Wengi wao wamejenga nyumba za kudumu katika eneo lile, na wengine ni viongozi waliokuwa mawaziri wakuu wastaafu nao wana viwanja katika eneo hilo na wamejenga nyumba zao katika eneo hilo,” alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema kiwanja hicho kilichokuwa na ekari zaidi ya 40 kilikuwa kinamilikiwa na taasisi ya Serikali ambayo ni kampuni tanzu ya Bodi ya Utalii Tanzania iliyokuwa inajulikana kama Serengeti Safari Lodges na baadae kikauzwa kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.

Wakati huo huo, Dk. Kigwangalla ametoa siku saba kwa Jeshi la Polisi nchini kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa wanne wanaojihusisha na mtandao wa ujangili pamoja na kupanga njama zilizopelekea mauaji ya Mhifadhi wa Wanyamapori Ndugu Wayne Lotter, raia wa Afrika ya Kusini ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Kampuni Pams Foundation, aliyeuawawa eneo la Chole Masaki Jijini Dar es Salaam mwezi Agosti mwaka jana.

“Natoa siku saba kwa wenzetu wa jeshi la Polisi wachukue hatua dhidi ya watu wanne, ambao mimi majina yao ninayafahamu ambao miongoni mwao watatu wanahusika na kuendesha biashara ya ujangili, na ni watu wakubwa, ni matajiri wakubwa na wana mitandao mikubwa ya ujangili.

“Ninafahamu taarifa hizi polisi wanazo lakini hawajachukua hatua za kuwakamata watu hawa na kuwafikisha kwenye macho ya sheria, muda ni mrefu  na sisi wenye taarifa hizi sasa tumeanza kuchoka kusubiri.

“Hawa watu wanne walihusika kupanga njama ambazo zilipelekea kusababisha mauaji ya kikatili ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Palm Foundation, Ndugu Wayle Lotter mwezi Agosti mwaka jana eneo la Chole Masaki mwezi Agosti mwaka jana.

“Nataka ndani ya siku hizi saba wawe wamechukua hatua na kama hawatochukua hatua manaake tutajua wana vested interest (maslahi) kwahivo tutaenda kuripoti kwa Amiri Jeshi mkuu ambaye ni Mhe. Rais aliyetutuma kazi ya kusimamia sekta hii,”. Alisema Dk. Kigwangalla.
 Dk. Kigwangalla akizungumza katika mkutano huo leo mjini Dodoma.

Tuesday, January 23, 2018

SERIKALI KUENDESHA MNADA WA HADHARA WA MENO YA VIBOKO JANUARI 29 JIJINI DAR ES SALAAM

Mnada huo utafanyika katika Jengo hili la Mpingo (Mpingo House) ambalo awali lilikuwa Makao Makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii kabla ya kuhamia Makao Makuu ya Nchi mjini Dodoma. 

Na Hamza Temba - WMU- Dodoma
...................................................................

*Wanunuzi wataruhusiwa kuyakagua (Januari 25 na 26) kabla ya mnada

*Watakaovuruga mnada kukiona cha mtemakuni

SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) itafanya mnada wa hadhara wa meno ya viboko vipande 12,467 vyenye uzito wa kilo 3,580.29.

Mnada huo utakaosimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango umepangwa kufanyika tarehe 29 Januari, 2018 kuanzia saa nne asubuhi katika Jengo la Mpingo, Barabara ya Nyerere Jijini Dar es Salaam, zilipokuwa  ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii (Ivory Room).

Kupitia taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Dk. James Wakibara amesema  mnada huo utawahusisha wafanyabiashara wa Nyara waliopewa leseni ya Nyara Daraja la Kwanza mwaka 2017.

Amesema wafanyabiashara hao wataruhusiwa kukagua meno hayo kati ya tarehe 25 na 26 Januari, 2018 kuanzia saa nne asubuhi hadi saa tisa na nusu jioni kabla ya siku ya mnada huo.

Aidha, amesema wanunuzi watakaoshinda mnada huo watatakiwa kulipa asilimia 25 ya malipo yote papo hapo na asilimia 75 itakayosalia itatakiwa kulipwa ndani ya siku kumi na nne zijazo baada ya mnada huo.

“Mtu yeyote atakayekuwa ametamka bei ya juu, kisha akashindwa kulipa asilimia 25 ya bei aliyotamka, atachukuliwa kuwa ni mwenye kutaka kuvuruga mnada na hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” ameonya Mkurugenzi huyo.

Amesema meno hayo yatauzwa kwa wastani wa uzito wa nusu kilo bila kugawanywa au kuchambuliwa wakati wa mnada na wanunuzi wataruhusiwa kuondoa bidhaa kwenye eneo la mnada baada ya kulipia ada na kodi husika kikamilifu na kupewa hati ya kumiliki nyara hizo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Dk. James Wakibara (kulia) akiteta jambo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kushoto) wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya 15 ya Jeshi Usu kwa kwa Maafisa wa Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro hivi karibuni Mkoani Katavi. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Rachel Kasanda.

Monday, January 22, 2018

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla kufungua Onesho la Chimbuko la Binadamu Afrika, Jijini Dar es Salaam

 Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Profesa Audax Mabulla akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo pichani) wakati wa utambulisho wa tukio hilo linalotarajiwa kufanyika kesho Januari 23.2018. 
Balozi wa Spain nchini, Bw. Felix Costales akizungumza katika tukio hilo mapema leo Januari 23,2018. Kulia kwake ni  Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Profesa Audax Mabulla. 
Vioneshwa kinachoelezea hatua za binadamu wa kale katika makumbusho ya Taifa ikiwa katika maandalizi ya mwisho mwisho kwa ajiri ya kesho
Na Andrew Chale, Dar es Salaam
............................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla (MB) anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kesho Januari 23.2018, kwenye uzinduzi wa Onesho la Chimbuko la Binadamu Afrika, tukio ambalo litafanyika majira ya saa 11 jioni katika viunga vya Makumbusho ya Taifa, yaliyopo mtaa wa Shabani Robert, mkabala na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).
Akizungumza wakati wa utambulisho wa tukio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Profesa Audax Mabulla amebainisha kuwa, tayari maandalizi ya onesho hilo yameenda sawa na watu mbalimbali watanatarajiwa kushuhudia tukio ambalo ni la siku moja wakiwemo viongozi wa Serikali na Mabalozi waliopo nchini, na
watalii wanatarajiwa kuhudhuria.

Profesa Mabulla amebainisha kuwa, Vioneshwa vyote katika onesho hilo hapo kesho, vimepatikana hapa Tanzania kutokana na tafiti za kisayansi na vimehifadhiwa Makumbusho ya Taifa.
“Vioneshwa hivi ni pamoja na masalia ya zamadamu, zana za mawe na
masalia ya wanyama walioishi takribani tangu miaka milioni 4 iliyopita. Pia zipo picha za zamadamu na mazingira waliyoishi wakifanya shughuli zao za kila siku.” alieleza Profesa Mabulla.

Kwa upande wake Mratibu kwa upande wa Tanzania Dk. Agness Gidna amesema Onesho limegawanyika katika sehemu kuu nne zikiwemo Makumbusho ya Taifa la Tanzania ikishirikiana na Ubalozi wa Spain Tanzania. Hii ni pamoja na Makumbusho ya Akiolojia ya
Madrid, Taasisi ya Chimbuko la Binadamu (IDEA) Madrid, Chuo Kikuu cha Alcala Madrid na Makumbusho ya CosmoCaixa Barcelona-Spain huku tamasha zima likidhaminiwa na Kampuni ya Simenti ya Twiga.

“Tunawashukuru kampuni ya Twiga Cement kwa kudhamini onesho la Chimbuko
la Binadamu Afrika (The Cradle of Humankind in Africa). Pia kutakuwa na Semina na onesho hili ni matokeo ya tafiti mbali mbali zinazofanyika bonde la Olduvai na Laetoli, Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro.” alieleza Dk Agness.

Aidha Dk.Agness ameongeza kuwa, Onesho hilo litakuwa katika pande nne ikiwemo sehemu ya kwanza inahusu ushahidi wa nyayo za zamadamu zilizongunduliwa huko Laetoli mwaka 1978 na mtafiti Dkt. Mary D. Leakey. Nyayo hizo ziliachwa na zamadamu anayeiitwa Australopithecus afarensis na ni ushaidi usiopingika wa zamadamu kutembea
wima kwa miguu miwili takribani miaka milioni 3.6 iliyopia.

Sehemu ya pili inahusu hadithi ya kusisimua ya kuwa binadamu (Genus Homo) ambapo kuna masalia ya zamadamu Zinjanthropus au Paranthropus boisei na Homo habilis, zana za mawe za mwanzo (Oldowan) zilizotumika katika kujipatia chakula na ushahidi wa kale wa ulaji wa nyama katika historia ya mabadiliko ya binadamu, takribani miaka million 2 iliyopita.
Sehemu ya tatu inahusu maisha ya jamii ya Homo erectus. Jamaii hii inafanana zaidi na binadamu wa sasa kuliko jamii zilizotangulia. Kuna masalia ya zamadamu Homo erectus, zana za mawe (Acheulian) na ushahidi wa ulaji wa wanyama wakubwa kama vile tembo na nyati wa zamani takribani miaka million 1.7 iliyopita.
Sehemu ya nne inaonesha kipindi cha mwanzo cha binadamu wa sasa (Homo sapiens) walioanza kutokea hapa Afrika miaka laki 2 iliyopita. Kuna masalia ya Homo sapiens na zana za mawe za muhula wa kati na muhula wa mwisho.
Mbali na onesho hilo, pia waandaji hao wa Makumbusho ya Taifa inawakaribisha watu wote kuhudhuria semina na ufunguzi wa onesho la Chimbuko la Binadamu Afrika.
Kwa upande wa Semina ambayo inatarajia kuanzia majira ya saa tisa kamili itaendeshwa na watafiti wa Kimataifa, akiwemo Prof. Manuel Dominguez-Rodrigo wa Chuo Kikuu cha Complutense, Spain; Prof. Audax ZP Mabulla na Dk. Agness Gidna.Vionesho ambavyo vinatarajiwa kuwapo kesho katika tukio hiloAfisa kutoka ubalozi wa Spain akipata maelezo kutoka kwa Mratibu upande wa Tanzania Dk. Agness Gidna  wa Makumbusho ya Taifa. Kulia ni Balozi wa Spain Bw. Felix Costales 

Tuesday, January 16, 2018

DK. KIGWANGALLA APONGEZA USHIRIKIANO WA FINLAND KATIKA UHIFADHI WA MISITU NCHINI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akizungumza na Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka ofisini kwake mjini Dodoma leo alipotembelewa na balozi huyo kwa ajili ya kujitambulisha na kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo katika uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini. 

Na Hamza Temba - Dodoma
.............................................................. 

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla ameipongeza Serikali ya Finland kwa ushirikiano na misaada mbalimbali ambayo imekuwa ikiitoa kuunga mkono juhudi za Serikali katika uhifadhi wa maliasili na uendelezaji wa misitu nchini.

Dk. Kigwangalla ametoa pongezi hizo leo Januari 16, 2018 kwa Balozi wa nchi hiyo hapa nchini, Mhe. Peka Huka ambaye amemtembelea ofisini kwake mjini Dodoma kwa ajili ya kujitambulisha na kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo katika uhifadhi na maendeleo ya misitu nchini.

“Napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Serikali ya Finland,  mmekuwa washirika wetu wakubwa wa maendeleo kwa muda mrefu ambao mmetusaidia mambo mbalimbali ikiwemo kuendeleza misitu nchini, kuendeleza Chuo cha Mafunzo ya Misitu Olmotonyi na hata mapitio ya Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998, ni matumaini yetu kuwa mtaendelea kudumisha ushirikiano huu”, alisema Dk. Kigwangalla.

Alimueleza balozi huyo kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika uhifadhi wa misitu nchini ikiwemo uhaba wa rasilimali fedha na teknolojia kwa ajili ya kuwezesha uhifadhi endelevu. Alisema changamoto nyingine ni uvunaji haramu wa mazao ya misitu ambayo husababisha eneo la hekta 372,000 za misitu kupotea kila mwaka.

Alisema mbali na nguvu kubwa inayotumiwa na Serikali katika udhibiti wa uvunaji holela wa mazao ya misitu Wizara yake kwa kushirikiana na taasisi zilizoko chini yake inaendelea kuweka mikakati thabiti kwa kushirikiana na mamlaka zingine za kiserikali kwa ajili ya kutafuta nishati mbadala pamoja na kuanzisha mashamba kwa ajili ya uzalishaji wa miti ya mkaa kwa njia endelevu.

Akizungumzia umuhimu wa misitu nchini, Dk. Kigwangalla alisema takribani kila kitu hapa nchini kinategemea uwepo wa misitu. Alisema zaidi ya asilimia 80 ya chanzo cha nishati ya umeme nchini ni maji ambayo hutegemea uwepo wa misitu, alitaja pia kilimo na ufugaji ambao pia hutegemea mvua na maji ambayo hutegemea pia uwepo wa misitu.

Kutokana na umuhimu huo, Dk. Kigwangalla amemuomba Balozi huyo kuhamasisha wawekezaji wa Finland  kuja kuwekeza Tanzania katika uzalishaji na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu nchini na kuahidi kuwapa ushirikiano.

Kwa upande wake Balozi Huka, alimueleza Dk. Kigwangalla kuwa nchi yake imekua ikifadhili miradi mbali mbali ya uendelezaji wa misitu katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo mikoa ya nyanda za juu kusini na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo.

Alimueleza Waziri Kigwangalla kuwa changamoto iliyopo ya uharibifu wa misitu nchini inahitaji uwepo wa nishati mbadala ambayo mchakato wa upatikanaji wake unatakiwa kushirikisha wadau na Mamlaka nyingine za Kiserikali ikiwemo Wizara ya Nishati.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akimkaribisha Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka ofisini kwake mjini Dodoma leo alipotembelewa na balozi huyo kwa ajili ya kujitambulisha na kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo katika uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akizungumza na Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka ofisini kwake mjini Dodoma leo alipotembelewa na balozi huyo kwa ajili ya kujitambulisha na kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo katika uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akimsikiliza Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka ofisini kwake mjini Dodoma leo.
 Balozi Peka Huka akimsikiliza Waziri Kigwangalla katika kikao hicho.
 Waziri Kigwangalla akifafanua jambo kwa Balozi Peka Huka (hayuko pichani) katika kikao hicho mapema leo mjini Dodoma.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akimuaga Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka baada ya mazungumzo ofisini kwake leo mjini Dodoma . 

Monday, January 15, 2018

DK. KIGWANGALLA ANENA-SERIKALI YADHAMIRIA KUIMARISHA HUDUMA KWA WAGENI WANAOINGIA NCHINI KUPITIA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA DAR ES SALAAM (JNIA)



Na Hamza Temba-Dar es Salaam
...................................................................................
SERIKALI kupitia wizara zake nne tofauti imedhamiria kukabiliana na changamoto mbalimbali za utoaji wa huduma kwa wageni wanaiongia na kutoka nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere (JNIA) jijijini Dar es Salaam.

Changamoto hizo ni pamoja na msongamano na joto katika eneo la kuchukulia mizigo, muda mrefu wa upatikanaji wa hati za kusafiria kwa wageni wanaoingia nchini pamoja na changamoto ya ufinyu wa eneo la kusubiri huduma uwanjani hapo.

Mawaziri wa Wizara hizo ambao wamefanya ziara ya pamoja katika uwanja huo jana na kukagua shughuli za utoaji huduma ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk.Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Dk.Susan Kolimba na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye.

Akizungumza uwanjani hapo, Dk. Kigwangalla alisema wamefikia hatua ya kukutana mawaziri hao baada ya wageni hasa watalii wanaiongia nchini kulalamika kuwa wanatumia muda mwingi kuhudumiwa katika eneo la uwanja huo kiasi cha kuwapotezea muda.

Dk.Kigwangala amesema kutokana na malalamiko hayo ya muda mrefu na mengine kadhaa hatua mbalimbali zimechukuliwa tangu Agosti 8 mwaka 2017 manaibu waziri wa wizara hizo nne walipofanya ziara uwanjani hapo kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi changamoto hizo na kwamba kukutana kwao jana ni muelendezo wa kushughulikia kero hizo ambapo mafanikio yameanza kuonekana.

Dk.Kigwangala amesema ipo haja ya kuweka mikakati ya kuboresha huduma katika viwanja vya ndege nchini ukiwamo JNIA huku akisisitiza umuhimu wa watendaji na watoa huduma katika nafasi mbalimbali kuwa wakarimu kwa wageni.

Amesema ni vema hata Polisi walioko uwanjani hapo wakimkamata mgeni basi badala ya kutumia nguvu wawe na ukarimu kwani ni muhimu kumdhibiti mgeni bila kutumia nguvu ili ikibainika hana kosa aachiwe na asiwe na malalamiko ya kunyanyaswa.

Dk.Kigwangala amesema kuna haja kwa wageni wanapokuja Tanzania wakirudi makwao wasimulie ukarimu na uzuri wa nchini yetu.

Ameongeza anatamani kuona kuanzia uwanjani hapo hadi hotelini ambako mgeni anakwenda anatumia muda mchache, anapata nafasi ya kuona picha za viongozi mbalimbali ambazo zitakuwa uwanjani, picha za wanyama na video ambazo zinaonesha utalii wa Tanzania.

Amesema kumpokea mgeni jambo moja lakini namna ya kumhudumia ni jambo jingine na ndilo muhimu zaidi na akafafanua hata teksi ambayo mgeni ataitumia kusafiri dereva awe na ukarimu hata wa kumsalimia na wakati mwingine kutabasamu.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya ndani Ndani Dk. Mwigulu Nchemba akizungumza baada ya ziara hiyo alisema jitihada mbalimbali zinafanywa kutatua changamoto hizo.

Ametaja hatua ambazo wizara yake inachukua ni kuharakisha utoaji huduma wa hati za kusafiria kwa njia ya kieletroniki.

Pia wameamua kuongeza idadi ya madawati ya kutolea huduma kwa wageni ikiwa sambamba na kuongeza watoaji huduma ili kurahisisha utoaji huduma wa muda mfupi.

“Taarifa zinaonesha kuwa kwa sasa kuna unafuu mkubwa wa kutoa huduma kwani badala ya saa tatu ambazo zilikuwa zinatumia awali hivi sasa muda wa utoaji huduma umeshuka hadi saa moja, lengo letu ni kushuka zaidi.
“Mbali ya kuboresha huduma tutahakikisha pia tunaongeza ulinzi na usalama katika viwanja vyetu vyote nchini ili kudhibiti wageni wenye nia ovu na nchi yetu.

“Tunafahamu mataifa mengi yameitikia mwito wa uwekezaji nchini hasa katika mikakati ya kufikia Serikali ya Viwanda na uchumi wa kati.
“Hivyo wageni wanakuja kwa nia njema ya kuwekeza lakini hatutaki wale wenye nia mbaya kutumia mwanya huo.Hivyo tutaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika viwanja vyetu,”amesema.

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Susan Kolimba amesema wanaridhishwa na hatua ambazo zinachukuliwa katika kuondoa changamoto zinazoelezwa kuwapo uwanjani hapo.

Amesema wizara yao inatamani kuona idadi ya wageni inaongezeka zaidi na wakati huo huo wakifurahia huduma ambazo wanazipata wakifika nchini kwetu. Alisema Wizara yake itaendelea kuitangaza Tanzania na vitutio vyake ili idadi ya watalii iweze kuongezeka.

“Tumefanya ziara na binafsi niseme tu nimeridhishwa na hatua ambazo zinachukuliwa katika kuondoa changamoto hizo,”amesema Dk.Kolimba.
Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema wizara yao tayari imechukua hatua mbalimbali za kuondoa changamoto zilizopo ikiwamo ya kufunga viyoyozi (AC) kwa ajili ya kuondoa hali ya joto.

“AC zilizopo ni za muda mrefu kwani ziliwekwa tangu majengo ya uwanja huo yalipojengwa. Hivyo tayari zimeanza kufungwa AC mpya na ndio maana joto limepungua” amesema.

Pia amesema wamepata kampuni ambayo itakayofanya ukarabati kwa kuongeza eneo la kukaa wageni wanaosubiri huduma mbalimbali kabla ya kutoka uwanjani.

Amesema kuna jitihada mbalimbali Serikali inafanya jitihada za kuondoa msongamano wa wageni ikiwamo ya kuharakisha ujenzi wa jengo jipya la kusafiria wageni la Terminal III ambalo litahudumia watu milioni sita badala ya jengo la sasa ambalo wakati linajengwa  lengo lake lilikuwa kuhudumia watu milioni moja.

“Ujenzi wa jengo jipya umekamilika kwa asilimia 70 na litakapokuwa tayari kwa asilimia 100 litaanza kutumika kwa kuwa kasi ya ujenzi inakwenda vizuri,’amesema.
 Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Mwigulu Nchemba wakati wa ziara ya pamoja ya kukagua Changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wageni hususan watalii  wanaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam JNIA jana kwa ajili ya kukabiliana nazo.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana wakati wa ziara ya pamoja ya kukagua Changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wageni hususan watalii  wanaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam JNIA kwa ajili ya kukabiliana nazo. Wengine walioshiriki ziara hiyo ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba (wa pili kulia), Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa tatu kulia) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Susan Kolimba (wa nne kulia).
 Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (wa pili kulia) akiteta jambo na  Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Susan Kolimba jijini Dar es salaam jana wakati wa ziara ya pamoja ya kukagua Changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wageni hususan watalii  wanaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam JNIA kwa ajili ya kukabiliana nazo. Wengine walioshiriki ziara hiyo ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba (wa tatu kushoto) na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto) .
 Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (wa tatu kulia) akiteta jambo na  Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Susan Kolimba jijini Dar es salaam jana wakati wa ziara ya pamoja ya kukagua Changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wageni hususan watalii  wanaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam JNIA kwa ajili ya kukabiliana nazo. Wengine walioshiriki ziara hiyo ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba (kulia) na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kulia).
 6
Naibu Waziri  wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Dkt. Susan Kolimba kulia  akitoa maelezo kwa   Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Mwigulu Nchemba kushoto, Naibu Waziri wa Ujenzi,  Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto) na  Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (wa pili kulia) wakati wa ziara hiyo.