slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Saturday, March 26, 2016

WAZIRI MAGHEMBE AWASIMAMISHA KAZI WATENDAJI TFS NA KAIMU MKURUGENZI IDARA YA WANYAMAPORI

Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Machi, 2016. Kulia ni Naibu Waziri Eng. Ramo Makani.
Sehemu ya waandishi wa habari na wajumbe mbalimbali walioshiriki Mkutano huo.
........................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Mghembe amemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu nchini, (TFS) Bw. Juma Mgoo pamoja na Wakurugenzi wawili wa Taasisi hiyo ili kupisha uchunguzi kutokana na mwenendo usioridhisha wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali na usimamizi mbovu wa rasilimali za misitu nchini.

Prof. Maghembe ametaja majina ya Wakurugenzi hao aliowasimamisha kazi kuwa ni Mkurugenzi Rasilimali Misitu, Bw. Zawadi Mbwambo pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi endelevu ya Misitu, Bw. Nurdin Chamuya

Baada ya kuwasimamisha hao amewateua watu wengine kushika nafasi zao wakati mchakato wa kuwapata watendaji wapya ukifanyika na walioteuliwa kukaimu nafasi hizo ni Kaimu Mtendaji Mkuu TFS, Gerald Kamwendo, Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Misitu, Mwanaidi Kijazi, na Kaimu Mkurugenzi wa Matumizi Rasilimali Misitu, Haji Mpya.

Wengine waliosimamishwa kazi na kanda zao katika mabano ni Hubert Haule (Kusini), Bakari Rashid (Mashariki), Cuthbert Mafipa (Kaskazini), Emmanuel Minja (Magharibi), Haji Khatibu (Ziwa) na Bruno Mallya (Nyanda za Juu Kusini).

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Prof. Maghembe amesema hatua hiyo imekuja baada ya kubaini mapungufu mbalimbali katika ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali na usimamizi usioridhisha wa rasilimali za misitu.

Alisema kuwa hivi karibuni walibaini shehena kubwa za magogo aina ya mninga katika Mkoa wa Rukwa wilayani Kalambo yakiwa yamekatwa na kuwekwa ndani ya makontena ndani ya msitu pamoja na kutengenezewa nyaraka feki zinazoonesha magogo hayo yanatoka nchini Zambia tayari kwa kusafirishwa kupelekwa nchini China.

Amesema kuwa baada ya kubaini tukio hilo na kulitolea maamuzi alipata taarifa kuwa shehena ya Magogo hayo yenye thamani ya shilingi milioni 500 za Kitanzania yaliyotakiwa kupelekwa Makao makuu ya Wilaya ya Kalambo yamemwagiwa petroli na kuchomwa moto wakati wiki mbili kabla alishatoa agizo la magogo hayo kusafirishwa kupelekwa Matai ambapo ni Makao Makuu ya Wilaya ya Kalambo.

Aliongeza kuwa kumekuwa na ubadhilifu unaofanywa na Maofisa wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika Mikoa na Wilaya kwa kutowasilishwa katika mfuko Mkuu wa Serikali.

“Pesa zitokanazo na makusanyo hayo zimekuwa hazipelekwi benki kwa wakati na hata zikipelekwa benki zimekuwa zikipelekwa pungufu na muda mwingine pesa hizo zimekuwa hazipelekwi kabisa”. Alisema Prof. Maghembe.

Katika tukio lingine, Waziri Maghembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori wa Matumizi Endelevu, Dkt. Charles Mulokozi kwa kosa la kukaidi agizo la kusaini vibali vya kusafirisha Wanyamapori nje ya nchi.

Hatua hiyo imekuja baada ya kukamatwa watu katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro wakitaka kusafirisha nyani 61 “velvety monkeys” na kubaini kuwa Idara ya Wanyamapori ndio iliyotoa vibali vya kusafirisha nyani hao na vibali hivyo kusainiwa na Mkurugenzi huyo.

Alisema watu hao kutoka Ulaya Mashariki na washirika wao wa hapa nchini, walikodisha ndege ili kuwaondoa tumbili hao kwenda Ulaya Mashariki. Alisema harakati za kukamata tumbili hao porini zilianza wiki iliyopita na jumla ya idadi yao ni 450 ilhali kuna taasisi zinazolinda hayo mapori bila walinzi wa mapori hayo kujua

Prof. Maghembe alisema nyani hao walikamatwa maeneo ya Upareni, Hanang Manyara na Kiliamanjaro ambapo aliwaita wasimamizi na kuwapa taarifa juu ya watu hao na kuwakataza kutotoa kibali chochote cha kusafirisha wanyama hao.

“Nikiwa Moshi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa nilimuita Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Wanyamapori Matumizi Endelevu, Dk Charles Mulokozi na kumuarifu juu ya kamata kamata hiyo na kumuagiza kutotoa kibali cha kusafirisha wanyama ili tuwakamate watu hao, lakini baadaye tukagundua yeye ndio amesaini kibali hicho kutoka Dar es Salaam,” alisema Maghembe.


Ameongeza kuwa ndege iliyokamatwa ilikuwa imekodiwa kutoka Afrika ya Kusini kwa ajili ya kusafirisha nyani hao kwenda Ulaya ya Mashariki, Ndege hiyo imeshikiliwa pamoja na rubani wake kwa mahojiano zaidi.

Prof. Maghembe ametoa onyo kali kwa wale wote wanaohujumu rasilimali za nchi na kusema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali.

“Hatutasita kumfukuza kazi mtu yeyote ambaye atashiriki katika suala hili la kuiibia nchi mali zake au anakaa anaangalia kando wakati fedha za nchi, mali za nchi zinaporwa” Alisema Prof. Maghembe kwa ukali.

SERIKALI YA TANZANIA HAINA MPANGO KWA KUTEKETEZA MENO YA TEMBO YALIYOHIFADHIWA

Serikali ya Tanzania imetoa tamko kuwa kwa sasa haina mpango wowote wa kuteketeza meno ya tembo yaliyohifadhiwa ambayo yametokana na vitendo vya ujangili na vifo asilia vya tembo.

Tamko hilo limetolewa hivi karibuni na Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Balozi wa Marekani hapa nchini Bw. Mark Childress alipotembelewa na balozi huyo ofisini kwake kujadili maendeleo ya sekta ya Maliasili mchini.

Prof. Maghembe alisema hayo baada Balozi huyo wa Marekani hapa nchini kutoa pendekezo kwa Serikali ya Tanzania kuchoma sehemu meno ya tembo yaliyohifadhiwa ili kutoa ujumbe mzito duniani juu ya dhamira ya Serikali kukomesha biashara hiyo haramu.

"Naomba niweke wazi kuwa kwa sasa hatupo tayari kuteketeza meno haya, tunaweza kuyatumia kwenye tafiti za kisayansi au vielelezo kwa ajili ya kesi za ujangili ambazo zipo mahakamani na nyingine ambazo bado zinafanyiwa uchunguzi" Alisema Prof. Maghembe.

Zipo nchi mbalimbali duniani ambazo zimechukua hatua ya kuteketeza meno yake ya tembo yaliyohifadhiwa ikiwemo nchi jirani ya Kenya na Malawi ambapo inaaminika kuwa kufanya hivyo ni njia mojawapo ya kushawishi Ulimwengu kukomesha biashara hii haramu ya meno ya tembo.

Nchi nyingine ni Chad, Ubelgiji, Ufaransa, China, India, Marekani na Ureno. Kwa upande wa nchi ambazo zina msimamo sawa na Tanzania katika kuendelea kuhifadhi meno yake ya Tembo ni pamoja na Afrika ya Kusini, Botswana na Zimbabwe.

Akizungumzia kuhusu kuendeleza sekta ya Maliasili nchini, Prof.Maghembe amemuomba Balozi wa Marekani Bw. Mark Childress kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukuza sekta hiyo kwa kuleta wawekezaji mbalimbali kutoka Marekani kuja kuwekeza Tanzania pamoja na kusaidia kwenye mapambano dhidi ya Ujangili.

Aliongeza kuwa Tanzania ina fursa nyingi ambazo zinahitaji uwekezaji mkubwa ikiwemo hoteli za kitalii, fukwe za kisasa na kuendeleza vivutio mbalimbali vilivyomo hapa nchini.

Prof. Maghembe amemshukuru balozi huyo kwa misaada mbalimbali kutoka Serikali ya Marekani ya kuendeleza sekta ya Maliasili nchini ukiwemo wa hivi karibuni wa mbwa maalum (Snifer Dogs) kwa ajili ya kusaidia utambuzi wa rasilimali za Maliasili zinazoweza kutoroshwa nje ya nchi kupitia bandari na viwanja vya ndege.

Katika taarifa iliyowasilishwa kwenye kikao baina ya Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe na Balozi wa Marekani hapa nchini Bw. Mark Childress imeonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali ya Marekani imetoa misaada mbalimbali ambayo jumla yake ni dola za kimarekani Milioni 41.35 katika kusaidia eneo la uhifadhi hapa nchini.



Akizungumzia mahusiano baina ya Tanzania na Marekani Balozi Mark Childress alimueleza Prof. maghembe kuwa Serikali ya Marekani itaendeleza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi hizi mbili ambapo pia ofisi yake ya ubalozi imeshatafuta wadau mbalimbali ambao wapo tayari kusaidia fedha, vifaa na mafunzo kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi na mapambano dhidi ya ujangili. 

Wednesday, March 23, 2016

WAZIRI WA MALIASILI PROF. JUMANNE MAGHEMBE AONANA NA BALOZI WA MAREKANI HAPA NCHINI MHE. MARK CHILDRESS KUJADILI MAENDELEO YA SEKTA YA MALIASILI NCHINI

Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akizungumza katika kikao na Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Mark Childress (kulia) na Ujumbe wake katika ukumbi wa Selous Makao Makuu ya Wizara hiyo Mpingo House leo tarehe 23 Machi, 2016. Waziri Maghembe amemuomba Balozi huyo wa Marekani kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukuza sekta ya utalii nchini kwa kuwakaribisha wawekezaji kutoka Marekani kuwekeza katika sekta hiyo.
Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Mark Childress (kulia) akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (kushoto). Balozi huyo wa Marekani ameahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Marekani katika kuendeleza sekta ya uhifadhi hapa nchini. Ameahidi pia kusaidia katika vita dhidi ya ujangili.
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akisisitiza jambo kwa  Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Mark Childress (wa pili kushoto). Mhe. Maghembe alimueleza balozi huyo kuwa Tanzania haiko tayari kuteketeza meno ya Tembo yaliyohifadhiwa mpaka hapo itakapoona namna bora zaidi ya kufanya kwani kwa sasa Meno hayo yanaweza kutumika kwa ajili ya tafiti mbalimbali za kisayansi na kusaidia pia katika utambuzi na vielelezo vya mashtaka ya ujangili. Mhe Maghembe alisema hayo baada ya Balozi Childress kutoa pendekezo kwa Serikali kuona uwezekano wa kuteketeza sehemu ya meno ya Tembo yaliyohifadhiwa ili kutoa ujumbe duniani wa namna Serikali ya Tanzania ilivyodhamiria katika vita dhidi ya Ujangili.
Sehemu ya wajumbe kutoka ubalozi wa Marekani walioongozana na Mhe. Balozi Mark Childress wakifuatilia mada katika kikao hicho. Wajumbe hawa kila mmoja aliwasilisha mada ikionyesha ushirikiano wa Serikali ya Marekani na Tanzania katika sekta ya uhifadhi hapa nchini.  
Baadhi ya wajumbe kutoka ubalozi wa Marekani na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kikao hicho.
Wajumbe kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii walioshiriki katika kikao hicho. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Bi. Angelina Madete.

Thursday, February 18, 2016

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU RIPOTI YA UTAFITI WA WATALII WALIOINGIA NCHINI MWAKA 2014


Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (wa pili kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ukumbi Benki Kuu ya Tanzania (BOT) tarehe 18/02/2016 juu ya ripoti ya Utafiti wa Watalii walioingia nchini mwaka 2014. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Bw. Jonhson Nyella na Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Bw. Zahoro Kimwaga kulia.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano huo wa Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

................................................................................

Sekta ya utalii Tanzania ambayo mchango wake katika mauzo ya nje ya nchi ni takribani  asilimia 24.0 iliendelea kukua katika mwaka 2014 kama inavyodhihirishwa na ongezeko la idadi ya watalii wa kimataifa kutoka 1,095,885 mwaka 2013 hadi 1,140,156 mwaka 2014.  Matokeo ya utafiti wa mwaka 2014 yanaonyesha ongezeko kubwa la mapato ya utalii ambayo yanatokana na ongezeko la idadi ya watatii.  Wageni wengi wanaiona Tanzania kama kivutio pekee chenye watu marafiki na mandhari ya kuvutia.

Utafiti huu umefanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii (MNRT) kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Idara ya Uhamiaji na Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZCT). 

Matokeo muhimu ya utafiti ni kama ifuatavyo:

1)   Mapato yatokanayo na Utalii yaliongezeka kwa asilimia 8.2 hadi  kufikia Dola za Kimarekani 2,006.3 milioni katika mwaka 2014, ikilinganishwa na Dola za Kimarekani  milioni 1,853.3 zilizopatikana mwaka 2013;

2)   Zanzibar ilipata Dola za Kimarekani 269.3 mwaka 2014 ikilinganishwa na dola za Kimarekani milioni 210.5 mwaka 2013;

3)    Wastani wa matumizi yote ya mtalii kwa usiku ilikuwa Dola za Kimarekani 221 chini kidogo ya Dola za Kimarekani 284 zilizoripotiwa mwaka 2013.

4)    Wageni waliofika chini ya mpango mfuko ziara walitumia wastani wa Dola za kimarekani 326.9 kwa mtu kwa usiku wakati wale waliokuja kwa kujitegemea walitumia wastani wa Dola za kimarekani 147.8;

5)   Masoko makuu 15 ya utalii nchini yanachangia asilimia 82 ya watalii wote wa kimataifa. Zimbabwe, Uholanzi na China ni masoko mapya katika masoko makuu 15 katika mwaka 2014; ambayo yamechukua nafasi ya Sweden, Uswisi na India katika masoko Makuu 15 yaliyopatikana mwaka 2013;

6)   Utalii wa wanyamapori - uliendelea kuwa shughuli kuu ya utalii katika Tanzania Bara ulichangia kwa asilimia 43.5. Idadi kubwa ya watalii waliokujai kutembelea wanyamapori walikuja kutoka Marekani, Uingereza, Ufaransa na Italia. Kwa upande Zanzibar, shughuli mashuhuri ilikuwa utalii wa ufukweni na kiutamaduni;

7)    Matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa asilimia 54.1 ya wageni wanatumia kati ya siku nane hadi 28. Wageni kutoka Ujerumani, Uholanzi, Italia, Ufaransa na Hispania walikaa muda mrefu zaidi na wale waliotoka Zimbabwe walikaa siku chache zaidi;

8)    Kama ilivyoonekana katika tafiti zilizopita, watalii hawakufurahishwa na kutokuwa na huduma ya credit cards katika maeneo yanayotoa huduma za kitalii. Asilimia 87 ya watalii walilipia huduma mbalimbali za kitalii kwa kutumia fedha taslimu.


Nakala ya ripoti hii inapatikana katika tovuti ya taasisi washirika ambazo: www.mnrt.go.tz, www.bot.go.tz, www.zanzibartourism.net , www.nbs.go.tz  na www. moha.go.tz. 

Wednesday, February 17, 2016

JAMII HAPA NCHINI YAASWA KUTUMIA FURSA YA UFUGAJI WA NYUKI NA UPANDAJI WA MITI KIBIASHARA KUJIINUA KIUCHUMI

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Gladyness Mkamba (katikati) akizungumza wakati akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Gen. Gaudence Milanzi katika ufunguzi wa Mkutano wa mapitio ya kukamilisha mradi wa Kitaifa wa Uendelezaji Misitu na Ufugaji Nyuki nchini (NFBKP II) unaofadhiliwa na Serikali ya Finland kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika Chuo cha Taifa cha Utalii Tawi la Bustani Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Februari, 2016. Kushoto ni Mshauri wa masuala ya Malisili kutoka Ubalozi wa Finland hapa nchini Bw. Mikko Leppanen na Bi. Monika Kagya, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Misitu na Nyuki.
 Sehemu ya washiriki wa mkutano huo kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na TAMISEMI. 
Sehemu ya washiriki wa mkutano huo katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii Tawi la Bustani Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Gladyness Mkamba akizungumza na Waandishi wa Habari  katika chuo cha Taifa cha Utalii Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Februari, 2016.
Mratibu Msaidizi wa mradi wa NFBKP II, Bi. Magdalena Muya (kulia) akiwasilisha mada ya jumla juu ya mradi huo ambao ulianza mwaka 2013 na kukamilika mwaka huu 2016.
Mshauri wa masuala ya Malisili kutoka Ubalozi wa Finland hapa nchini Bw. Mikko Leppanen akieleza jambo kwa waandishi wa habari.
Picha ya pamoja.

................................................................................................

Jamii hapa nchini imeaswa kutumia fursa iliyopo ya ufugaji wa nyuki na upandaji wa miti kibiashara kujiinua kiuchumi.

Wito huo umetolewa jana na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Gladyness Mkamba akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam.

Bi. Mkamba alisema kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya kuzalisha asali kwa wingi duniani ambayo ikitumiwa ipasavyo itasaidia kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

"Kwa sasa Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika ambapo inazalisha asali tani 34,000 kwa mwaka baada ya Ethiopia inayozalisha tani 56,000. Hata hivyo kiwango hicho ni kidogo kwa kuwa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha asali tani 1,038,000 kwa mwaka" Alieleza.

Akizungumzia changamaoto kuu inayosababisha kiwango hicho kisifikiwe kirahisi, amesema ni utashi hafifu wa jamii kujishuulisha na kazi za ufugaji nyuki na uhifadhi wa mazingira ikiwemo upandaji wa miti.

Bi. Mkamba aliongeza kuwa Jamii ikihamasishwa vya kutosha juu ya faida za ufugaji nyuki na upandaji wa miti inaweza kutoa matokeo ya haraka kwa kuwa asali ina faida kubwa ikiwemo za kiafya na za kiuchumi.

Kwa upande wake Bi. Magdalena Muya ambaye ni Mratibu Msaidizi wa mradi wa Kitaifa wa Misitu na Ufugaji wa Nyuki nchini (NFBKP II) ameeleza kuwa changamoto zingine zinazokwamisha mafanikio katika sekta ya ufugaji nyuki nchini ni ukosefu wa teknolojia za kisasa za ufugaji nyuki na uzalishaji wa asali pamoja na ukosefu wa mitaji ya kuanzisha miradi mikubwa ya ufugaji wa nyuki.

Nae mshauri wa masuala ya Malisili kutoka Ubalozi wa Finland hapa nchini Bw. Mikko Leppanen, ameeleza kuwa Misitu ya Tanzania inakabiliwa na changamoto ya uharibifu mkubwa unaosababishwa na shughuli za kibinadamu ambapo hupelekea ukame na kuathiri pia uzalishaji wa asali ambao hutegemea malighafi za misitu.

Mshauri huyo ameiasa jamii hapa nchini kutunza mazingira ya misitu, kupanda miti kibiashara na kuhifadhi mazingira ambayo yatasaidia kuweka mazingira bora ya kuishi ikiwa ni pamoja na kuwezesha ufugaji wa nyuki kibiashara na kuwainua watu kiuchumi.

Wakati huo huo Kaimu Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili Bi. Gladyness Mkamba akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Gen. Gaudence Milanzi wakati akifungua mkutano wa siku moja wa mapitio ya kukamilisha Mradi wa Kitaifa wa Misitu na Ufugaji wa Nyuki nchini (NFBKP II) ameishukuru Serikali ya Finland kwa kusaidia ufadhili wa mradi huo.

Ameeleza kuwa mradi huo ambao bajeti yake ni Euro Milioni 19.5 ambazo ni zaidi ya Tsh. Bilioni 47 kwasasa unafadhili mpango wa miaka minne wa Misitu binafsi katika Mikoa ya Iringa, Njombe na Morogoro kwa lengo la kuinua kipato cha wananchi wa vijijini katika Mikoa ya Kusini mwa Tanzania, Mikoa hiyo ni shemu ya Mikoa saba ya jumla inayofadhiliwa na mradi huo.

Amesema hayo yatafanyika kwa kuanzisha misitu ya uhakika yenye faida na kuongeza thamani ya mazao yake kwenye mtiririko wa uzalishaji kuanzia mbegu za miti hadi kwenye bidhaa bora za mbao.
Mradi huo ulianza Oktoba mwaka 2013 hadi Oktoba 2015 na kuongezewa muda wa ziada wa miezi minne ambapo unakamilika mwezi huu wa Februari 2016.

Tuesday, February 9, 2016

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII PROF. JUMANNE MAGHEMBE AZUNGUMZIA TUKIO LA KUSHAMBULIWA HELKOPTA YA DORIA ILIYOPELEKEA KIFO CHA RUBANI WAKE

Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo tarehe 09/02/2016 katika ukumbi wa Ngorongoro Makao Makuu ya Wizara hiyo kuzungungumzia tukio la hivi karibuni (tarehe 29 Januari 2016) la kushambuliwa kwa helkopta ya doria na kuuawa Rubani Rogers Gowel Raia wa Uingereza. Katikati ni Naibu Waziri Maliasili na Utalii Eng. Ramo Makani na Katibu Mkuu Wizara hiyo Maja Gen. Gaudence Milanzi. SOMA TAARIFA KAMILI HAPO CHINI (SCROL DOWN FOR MORE DETAILS)
 Mkutano na Waandishi wa Habari ukiwa unaendelea.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, INSPEKTA Jenerali (IGP), Ernest Mangu, kulia akifafanua moja ya jambo katika Mkutano huo. Kulia ni Waziri wa  Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe.
 Baadhi ya viongozi kutoka Wizara ya Maliasili walioshiriki mkutano huo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Bw. Herman Keraryo. 
Waandishi wa habari wakichukua matukio ya mkutano huo na baadhi ya washiriki wakifuatilia.

Monday, February 8, 2016

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII PROF. JUMANNE MAGHEMBE AONANA NA BALOZI WA UJERUMANI NCHINI MHE. EGON KONCHANKE

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe (wa pili kulia) akizungumza na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Mhe. Egon Konchanke (kushoto) alipomtembelea ofisini kwake Mpingo House jijini Dare s Salaam tarehe 08 Februari 2016. Kulia ni Bi.Lena Thiede kutoka Ubalozi wa Ujerumani nchini ambaye ni MKuu wa Kitengo cha Shirikisho la Kikanda Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka kundi la Wshirika wa Maendeleo sekta ya Mazingira, Maliasili na Mabadiliko ya Tabia ya nchi. Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kufahamiana na kuendeleza mashirikiano baina ya Ujerumani na Tanzania katika kulinda na kuhifadhi maliasili zilizopo nchini. Wa pili kulia ni Katibu wa Waziri Bw. Imani Nkuwi. 
 Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Mhe. Egon Konchanke (wa pili kulia) akizungumza Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe (wa kwanza kulia ) walipoonana ofisini kwake Mpingo House jijini Dare s Salaam  tarehe 08 Februari 2016. Wengine kushoto ni Bi.Lena Thiede kutoka Ubalozi wa Ujerumani nchini,  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Generali Gaudence Milanzi.