slider gif
kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ
Monday, April 4, 2016
Saturday, April 2, 2016
SERIKALI YA UJERUMANI YATOA MSAADA WA NDEGE MAALUM AINA YA HUSKY A-1C KUSAIDIA DORIA YA KUPAMBANA NA VITENDO VYA UJANGILI KATIKA PORI LA AKIBA LA SELOUS
Waziri wa Maliasili
Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Ushirikiano wa
Kiuchumi na Maendeleo kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd
Muller alipowasili katika uwanja mdogo wa ndege wa Matambwe uliopo ndani ya
Hifadhi ya akiba ya Selous Mkoani Morogoro kwa ajili ya hafla ya makabidhiano
ya ndege maalum aina ya Husky A-1C kutoka Serikali ya Ujerumani itakayosaidia kufanya
doria za kupambana na ujangili katika hifadhi hiyo.
Sehemu ya kundi la Swala katika hifadhi ya akiba ya Selous.
Moja ya Twiga akiwa anakimbia katika hifadhi ya akiba ya Selous.
Sehemu ya wajumbe wa msafara wa Waziri Maghembe na Waziri wa Muller wakibadilishana mawazo katika hifadhi ya akiba ya Selous.
..............................................................
Serikali ya Ujerumani
imetoa msaada wa ndege maalum aina ya “Husky A-1C Aircraft” kwa Serikali ya
Tanzania kupitia Wizara ya Malisili na Utalii kwa ajili ya kusaidia katika doria
za kupambana na Ujangili katika Pori la Akiba la Selous.
Msaada huo wenye thamani
ya Euro 200,000 sawa na Tsh. 498,292,000, umekabidhiwa kwa Mhe. Waziri wa
Maliasili Prof. Jumanne Maghembe na Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na
Maendeleo wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd Muller katika hafla
fupi iliyofanyika Matambwe ndani ya pori la Akiba la Selous.
Hafla hiyo
ilihudhuriwa na Maafisa wa Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini wakiongozwa na
Balozi Mhe. Egon Konchanke, viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na
Utalii, Mamlaka ya Wanyamapori
Tanzania (TAWA), Mashirika ya Maendeleo ya Kimataifa ya FZS, WWF, GIZ na KFW.
Akizungumza katika
hafla hiyo Waziri Maghembe amesema ndege hiyo itasaidia jitihada za Serikali za
kupambana na Ujangili kwa kufanya doria katika anga ya hifadhi ya Akiba ya Selous
na kusaidia kutoa taarifa za kiuhalifu pale itakapobainika na kuchukuliwa hatua
stahiki za kukabiliana na uhalifu huo.
“Ndege hii
tunayoshuhudia mapokezi yake leo ni ukombozi kwa Wanyamapori katika Pori hili
la Akiba la Selous kwani itasaidia na kuimarisha doria za kupambana na ujangili
ndani na kuzunguka eneo zima la hifadhi”. Alisema Prof. Maghembe.
Waziri Maghembe
ameishukuru Serikali ya Ujerumani kupitia kwa Waziri Muller kwa msaada huo na
mingine ambayo wamekuwa wakiitoa kusaidia uhifadhi wa Wanamapori hapa nchini, Amebainisha
kuwa misaada hiyo imekuwa na tija kubwa katika kuendeleza uhifadhi wa
Wanyamapori ikilinganishwa na kipindi cha nyuma kabla ya kuwepo kwa misaada
hiyo.
Waziri Maghembe
alieleza kuwa sera ya Wanyamapori Tanzania inatambua ushirikiano wa wahisani na
watu binafsi katika kuisaidia Serikali Kifedha na Kitaaluma kwenye eneo la
uhifadhi, hivyo amewaomba wadau mbalimbali kuendelea kuipa ushirikiano Serikali
katika jitihada zake za kuendeleza Uhifadhi wa Wanyamapori nchini.
Kwa upande wake
Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Ujerumani Dkt. Gerd Muller alimueleza
Prof. Maghembe kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika
kuendeleza uhifadhi hapa nchini. Waziri huyo pia aliwapongeza Askari wa Wanyamapori
kwa kazi nzuri wanayofanya ya kulinda Wanyamapori katika mazingira magumu ya
porini.
Akizungumza kwa lugha
ya Kijerumani huku ikitafsiriwa kwa Kiingereza na Mkalimani wake Dkt. Muller alisema
ipo haja kubwa ya kuendelea kuwalinda Wanyamapori kwa nguvu zote kwa kuwa hawana
hatia na kwamba walikuwepo katika mazingira yao ya asili kabla hata ya binadamu
kuwepo hapo.
“Hawa viumbe hai
wanaowindwa walikuwepo katika mazingira haya kabla ya sisi binadamu kuja hapa,
Sote tunahitaji kuwalinda na kuishi kwa amani na viumbe hawa ndio kutakuwa na
amani duniani kote” Alieleza Dkt. Muller.
Mapema akizungumza
kabla ya tukio la kukabidhiwa ndege, Meneja wa Pori hilo la Akiba la Selous Bw.
Mabula Misungwi alieleza baadhi ya changamoto kuu zinazoikabili hifadhi hiyo
kuwa ni ujangili, miundombinu mibovu ya barabara kwa ajili ya doria na vifaa
ikiwemo magari ya doria.
Msafara wa Waziri
Maghembe na ugeni wake kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani walipata
fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya hifadhi ya Selous ikiwemo Matambwe na
Behobeho ambayo inajulikana kama Serengeti ndogo na kujionea Wanyamapori
mbalimbali wakiwemo Tembo, Twiga, Pundamilia, Swala, Nyani, Ngiri, Nyumbu na
mandhari mazuri ya mto behobeho.
Pori la Akiba la Selous
ni moja ya Pori kubwa duniani ikiwa na ukubwa wa zaidi ya Kilomita za mraba
50,000. Pori hili lipo ndani ya Mikoa mitano ya Tanzania ambayo ni Pwani,
Morogoro, Lindi, Mtwara na Songea. Pori hili limeathiriwa kwa kiasi kikubwa na
ujangili kwani katika Sensa ya mwaka 2013 ilionesha idadi ya tembo katika
pori hilo kuwa 13,000 idadi ambayo ni ndogo sana ikilinganishwa na ile ya
mwaka 2003 ambayo ilikuwa 70,000.
Saturday, March 26, 2016
WAZIRI MAGHEMBE AWASIMAMISHA KAZI WATENDAJI TFS NA KAIMU MKURUGENZI IDARA YA WANYAMAPORI
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Machi, 2016. Kulia ni Naibu Waziri Eng. Ramo Makani.
Sehemu ya waandishi wa habari na wajumbe mbalimbali walioshiriki Mkutano huo.
........................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Mghembe
amemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu nchini, (TFS)
Bw. Juma Mgoo pamoja na Wakurugenzi wawili wa Taasisi hiyo ili kupisha
uchunguzi kutokana na mwenendo usioridhisha wa ukusanyaji wa maduhuri ya
Serikali na usimamizi mbovu wa rasilimali za misitu nchini.
Prof. Maghembe ametaja majina ya Wakurugenzi hao aliowasimamisha
kazi kuwa ni Mkurugenzi Rasilimali Misitu, Bw. Zawadi Mbwambo pamoja na Kaimu
Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi endelevu ya Misitu, Bw. Nurdin Chamuya
Baada ya kuwasimamisha hao amewateua watu
wengine kushika nafasi zao wakati mchakato wa kuwapata watendaji wapya
ukifanyika na walioteuliwa kukaimu nafasi hizo ni Kaimu Mtendaji Mkuu TFS,
Gerald Kamwendo, Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Misitu, Mwanaidi Kijazi, na Kaimu
Mkurugenzi wa Matumizi Rasilimali Misitu, Haji Mpya.
Wengine waliosimamishwa kazi
na kanda zao katika mabano ni Hubert Haule (Kusini), Bakari Rashid (Mashariki),
Cuthbert Mafipa (Kaskazini), Emmanuel Minja (Magharibi), Haji Khatibu (Ziwa) na
Bruno Mallya (Nyanda za Juu Kusini).
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Prof.
Maghembe amesema hatua hiyo imekuja baada ya kubaini mapungufu mbalimbali
katika ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali na usimamizi usioridhisha wa
rasilimali za misitu.
Alisema kuwa hivi karibuni
walibaini shehena kubwa za magogo aina ya mninga katika Mkoa wa Rukwa wilayani
Kalambo yakiwa yamekatwa na kuwekwa ndani ya makontena ndani ya msitu pamoja na
kutengenezewa nyaraka feki zinazoonesha magogo hayo yanatoka nchini Zambia
tayari kwa kusafirishwa kupelekwa nchini China.
Amesema kuwa baada ya kubaini tukio hilo na kulitolea maamuzi alipata
taarifa kuwa shehena ya Magogo hayo yenye thamani ya shilingi milioni 500 za
Kitanzania yaliyotakiwa kupelekwa Makao makuu ya Wilaya ya Kalambo yamemwagiwa
petroli na kuchomwa moto wakati wiki mbili kabla alishatoa agizo la magogo hayo
kusafirishwa kupelekwa Matai ambapo ni Makao Makuu ya Wilaya ya Kalambo.
Aliongeza kuwa kumekuwa na ubadhilifu unaofanywa na Maofisa wa
ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika
Mikoa na Wilaya kwa kutowasilishwa katika mfuko Mkuu wa Serikali.
“Pesa zitokanazo na makusanyo hayo zimekuwa hazipelekwi benki
kwa wakati na hata zikipelekwa benki zimekuwa zikipelekwa pungufu na muda
mwingine pesa hizo zimekuwa hazipelekwi kabisa”. Alisema Prof. Maghembe.
Katika tukio lingine, Waziri Maghembe amemsimamisha kazi
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori wa Matumizi Endelevu, Dkt. Charles
Mulokozi kwa kosa la kukaidi agizo la kusaini vibali vya kusafirisha
Wanyamapori nje ya nchi.
Hatua hiyo imekuja baada ya
kukamatwa watu katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro wakitaka
kusafirisha nyani 61 “velvety monkeys” na kubaini kuwa Idara ya Wanyamapori
ndio iliyotoa vibali vya kusafirisha nyani hao na vibali hivyo kusainiwa na
Mkurugenzi huyo.
Alisema watu hao kutoka Ulaya
Mashariki na washirika wao wa hapa nchini, walikodisha ndege ili kuwaondoa
tumbili hao kwenda Ulaya Mashariki. Alisema harakati za kukamata tumbili hao
porini zilianza wiki iliyopita na jumla ya idadi yao ni 450 ilhali kuna taasisi
zinazolinda hayo mapori bila walinzi wa mapori hayo kujua
Prof. Maghembe alisema nyani hao
walikamatwa maeneo ya Upareni, Hanang Manyara na Kiliamanjaro ambapo aliwaita
wasimamizi na kuwapa taarifa juu ya watu hao na kuwakataza kutotoa kibali
chochote cha kusafirisha wanyama hao.
“Nikiwa Moshi katika Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa nilimuita Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Wanyamapori Matumizi
Endelevu, Dk Charles Mulokozi na kumuarifu juu ya kamata kamata hiyo na
kumuagiza kutotoa kibali cha kusafirisha wanyama ili tuwakamate watu hao,
lakini baadaye tukagundua yeye ndio amesaini kibali hicho kutoka Dar es
Salaam,” alisema Maghembe.
Ameongeza kuwa ndege iliyokamatwa ilikuwa imekodiwa kutoka Afrika ya Kusini kwa
ajili ya kusafirisha nyani hao kwenda Ulaya ya Mashariki, Ndege hiyo imeshikiliwa
pamoja na rubani wake kwa mahojiano zaidi.
Prof. Maghembe ametoa onyo kali kwa wale wote wanaohujumu
rasilimali za nchi na kusema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali.
“Hatutasita kumfukuza kazi mtu yeyote ambaye atashiriki katika
suala hili la kuiibia nchi mali zake au anakaa anaangalia kando wakati fedha za
nchi, mali za nchi zinaporwa” Alisema Prof. Maghembe kwa ukali.
SERIKALI YA TANZANIA HAINA MPANGO KWA KUTEKETEZA MENO YA TEMBO YALIYOHIFADHIWA
Serikali ya Tanzania imetoa tamko
kuwa kwa sasa haina mpango wowote wa kuteketeza meno ya tembo yaliyohifadhiwa
ambayo yametokana na vitendo vya ujangili na vifo asilia vya tembo.
Tamko hilo limetolewa hivi karibuni
na Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Balozi
wa Marekani hapa nchini Bw. Mark Childress alipotembelewa na balozi huyo ofisini
kwake kujadili maendeleo ya sekta ya Maliasili mchini.
Prof. Maghembe alisema hayo baada
Balozi huyo wa Marekani hapa nchini kutoa pendekezo kwa Serikali ya Tanzania
kuchoma sehemu meno ya tembo yaliyohifadhiwa ili kutoa ujumbe mzito duniani juu
ya dhamira ya Serikali kukomesha biashara hiyo haramu.
"Naomba niweke wazi kuwa kwa
sasa hatupo tayari kuteketeza meno haya, tunaweza kuyatumia kwenye tafiti za
kisayansi au vielelezo kwa ajili ya kesi za ujangili ambazo zipo mahakamani na
nyingine ambazo bado zinafanyiwa uchunguzi" Alisema Prof. Maghembe.
Zipo nchi mbalimbali duniani ambazo
zimechukua hatua ya kuteketeza meno yake ya tembo yaliyohifadhiwa ikiwemo nchi
jirani ya Kenya na Malawi ambapo inaaminika kuwa kufanya hivyo ni njia mojawapo
ya kushawishi Ulimwengu kukomesha biashara hii haramu ya meno ya tembo.
Nchi nyingine ni Chad, Ubelgiji,
Ufaransa, China, India, Marekani na Ureno. Kwa upande wa nchi ambazo zina
msimamo sawa na Tanzania katika kuendelea kuhifadhi meno yake ya Tembo ni
pamoja na Afrika ya Kusini, Botswana na Zimbabwe.
Akizungumzia kuhusu kuendeleza sekta
ya Maliasili nchini, Prof.Maghembe amemuomba Balozi wa Marekani Bw. Mark Childress
kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukuza sekta hiyo kwa kuleta
wawekezaji mbalimbali kutoka Marekani kuja kuwekeza Tanzania pamoja na kusaidia
kwenye mapambano dhidi ya Ujangili.
Aliongeza kuwa Tanzania ina fursa
nyingi ambazo zinahitaji uwekezaji mkubwa ikiwemo hoteli za kitalii, fukwe za
kisasa na kuendeleza vivutio mbalimbali vilivyomo hapa nchini.
Prof. Maghembe amemshukuru balozi
huyo kwa misaada mbalimbali kutoka Serikali ya Marekani ya kuendeleza sekta ya
Maliasili nchini ukiwemo wa hivi karibuni wa mbwa maalum (Snifer Dogs) kwa
ajili ya kusaidia utambuzi wa rasilimali za Maliasili zinazoweza kutoroshwa nje
ya nchi kupitia bandari na viwanja vya ndege.
Katika taarifa iliyowasilishwa kwenye
kikao baina ya Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe na Balozi wa Marekani
hapa nchini Bw. Mark Childress imeonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita Serikali ya Marekani imetoa misaada mbalimbali ambayo jumla yake ni
dola za kimarekani Milioni 41.35 katika kusaidia eneo la uhifadhi hapa nchini.
Akizungumzia mahusiano baina ya
Tanzania na Marekani Balozi Mark Childress alimueleza Prof. maghembe kuwa
Serikali ya Marekani itaendeleza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi hizi
mbili ambapo pia ofisi yake ya ubalozi imeshatafuta wadau mbalimbali ambao wapo
tayari kusaidia fedha, vifaa na mafunzo kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi na mapambano
dhidi ya ujangili.
Wednesday, March 23, 2016
WAZIRI WA MALIASILI PROF. JUMANNE MAGHEMBE AONANA NA BALOZI WA MAREKANI HAPA NCHINI MHE. MARK CHILDRESS KUJADILI MAENDELEO YA SEKTA YA MALIASILI NCHINI
Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akizungumza katika kikao na Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Mark Childress (kulia) na Ujumbe wake katika ukumbi wa Selous Makao Makuu ya Wizara hiyo Mpingo House leo tarehe 23 Machi, 2016. Waziri Maghembe amemuomba Balozi huyo wa Marekani kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukuza sekta ya utalii nchini kwa kuwakaribisha wawekezaji kutoka Marekani kuwekeza katika sekta hiyo.
Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Mark Childress (kulia) akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (kushoto). Balozi huyo wa Marekani ameahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Marekani katika kuendeleza sekta ya uhifadhi hapa nchini. Ameahidi pia kusaidia katika vita dhidi ya ujangili.
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akisisitiza jambo kwa Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Mark Childress (wa pili kushoto). Mhe. Maghembe alimueleza balozi huyo kuwa Tanzania haiko tayari kuteketeza meno ya Tembo yaliyohifadhiwa mpaka hapo itakapoona namna bora zaidi ya kufanya kwani kwa sasa Meno hayo yanaweza kutumika kwa ajili ya tafiti mbalimbali za kisayansi na kusaidia pia katika utambuzi na vielelezo vya mashtaka ya ujangili. Mhe Maghembe alisema hayo baada ya Balozi Childress kutoa pendekezo kwa Serikali kuona uwezekano wa kuteketeza sehemu ya meno ya Tembo yaliyohifadhiwa ili kutoa ujumbe duniani wa namna Serikali ya Tanzania ilivyodhamiria katika vita dhidi ya Ujangili.
Sehemu ya wajumbe kutoka ubalozi wa Marekani walioongozana na Mhe. Balozi Mark Childress wakifuatilia mada katika kikao hicho. Wajumbe hawa kila mmoja aliwasilisha mada ikionyesha ushirikiano wa Serikali ya Marekani na Tanzania katika sekta ya uhifadhi hapa nchini.
Baadhi ya wajumbe kutoka ubalozi wa Marekani na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kikao hicho.
Wajumbe kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii walioshiriki katika kikao hicho. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Bi. Angelina Madete.
Thursday, February 18, 2016
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU RIPOTI YA UTAFITI WA WATALII WALIOINGIA NCHINI MWAKA 2014

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (wa pili kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ukumbi Benki Kuu ya Tanzania (BOT) tarehe 18/02/2016 juu ya ripoti ya Utafiti wa Watalii walioingia nchini mwaka 2014. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Bw. Jonhson Nyella na Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Bw. Zahoro Kimwaga kulia.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano huo wa Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
................................................................................
Sekta
ya utalii Tanzania ambayo mchango wake katika mauzo ya nje ya nchi ni takribani
asilimia 24.0 iliendelea kukua katika
mwaka 2014 kama inavyodhihirishwa na ongezeko la idadi ya watalii wa kimataifa
kutoka 1,095,885 mwaka 2013 hadi 1,140,156 mwaka 2014. Matokeo ya utafiti wa mwaka 2014 yanaonyesha
ongezeko kubwa la mapato ya utalii ambayo yanatokana na ongezeko la idadi ya watatii. Wageni wengi wanaiona Tanzania kama kivutio pekee
chenye watu marafiki na mandhari ya kuvutia.
Utafiti
huu umefanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii (MNRT) kwa kushirikiana na Benki
Kuu ya Tanzania (BOT), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Idara ya Uhamiaji na
Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZCT).
Matokeo
muhimu ya utafiti ni kama ifuatavyo:
1)
Mapato
yatokanayo na Utalii yaliongezeka kwa asilimia 8.2 hadi kufikia Dola za Kimarekani 2,006.3 milioni
katika mwaka 2014, ikilinganishwa na Dola za Kimarekani milioni 1,853.3 zilizopatikana mwaka 2013;
2)
Zanzibar
ilipata Dola za Kimarekani 269.3 mwaka 2014 ikilinganishwa na dola za
Kimarekani milioni 210.5 mwaka 2013;
3)
Wastani wa matumizi yote ya mtalii kwa usiku
ilikuwa Dola za Kimarekani 221 chini kidogo ya Dola za Kimarekani 284 zilizoripotiwa
mwaka 2013.
4)
Wageni waliofika chini ya mpango mfuko ziara walitumia
wastani wa Dola za kimarekani 326.9 kwa mtu kwa usiku wakati wale waliokuja kwa
kujitegemea walitumia wastani wa Dola za kimarekani 147.8;
5)
Masoko
makuu 15 ya utalii nchini yanachangia asilimia 82 ya watalii wote wa kimataifa.
Zimbabwe, Uholanzi na China ni masoko mapya katika masoko makuu 15 katika mwaka
2014; ambayo yamechukua nafasi ya Sweden, Uswisi na India katika masoko Makuu
15 yaliyopatikana mwaka 2013;
6)
Utalii
wa wanyamapori - uliendelea kuwa shughuli kuu ya utalii katika Tanzania Bara ulichangia
kwa asilimia 43.5. Idadi kubwa ya watalii waliokujai kutembelea wanyamapori walikuja
kutoka Marekani, Uingereza, Ufaransa na Italia. Kwa upande Zanzibar, shughuli mashuhuri
ilikuwa utalii wa ufukweni na kiutamaduni;
7)
Matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa asilimia
54.1 ya wageni wanatumia kati ya siku nane hadi 28. Wageni kutoka Ujerumani,
Uholanzi, Italia, Ufaransa na Hispania walikaa muda mrefu zaidi na wale
waliotoka Zimbabwe walikaa siku chache zaidi;
8)
Kama ilivyoonekana katika tafiti zilizopita,
watalii hawakufurahishwa na kutokuwa na huduma ya credit cards katika maeneo
yanayotoa huduma za kitalii. Asilimia 87 ya watalii walilipia huduma mbalimbali
za kitalii kwa kutumia fedha taslimu.
Nakala
ya ripoti hii inapatikana katika tovuti ya taasisi washirika ambazo:
www.mnrt.go.tz, www.bot.go.tz, www.zanzibartourism.net
, www.nbs.go.tz na www. moha.go.tz.
Wednesday, February 17, 2016
JAMII HAPA NCHINI YAASWA KUTUMIA FURSA YA UFUGAJI WA NYUKI NA UPANDAJI WA MITI KIBIASHARA KUJIINUA KIUCHUMI

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Gladyness Mkamba (katikati) akizungumza wakati akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Gen. Gaudence Milanzi katika ufunguzi wa Mkutano wa mapitio ya kukamilisha mradi wa Kitaifa wa Uendelezaji Misitu na Ufugaji
Nyuki nchini (NFBKP II) unaofadhiliwa na Serikali ya Finland kwa ushirikiano na
Serikali ya Tanzania katika Chuo cha Taifa cha Utalii Tawi la Bustani Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Februari, 2016. Kushoto ni Mshauri wa masuala ya Malisili kutoka Ubalozi wa Finland hapa nchini Bw. Mikko Leppanen na Bi. Monika Kagya, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Misitu na Nyuki.

Sehemu ya washiriki wa mkutano huo kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na TAMISEMI.

Sehemu ya washiriki wa mkutano huo katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii Tawi la Bustani Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya
Maliasili na Utalii Bi. Gladyness Mkamba akizungumza na Waandishi wa Habari katika chuo cha Taifa cha Utalii Jijini
Dar es Salaam tarehe 16 Februari, 2016.

Mratibu Msaidizi wa mradi
wa NFBKP II, Bi. Magdalena Muya (kulia) akiwasilisha mada ya jumla juu ya mradi huo ambao ulianza mwaka 2013 na kukamilika mwaka huu 2016.
Mshauri wa masuala ya Malisili kutoka Ubalozi wa
Finland hapa nchini Bw. Mikko Leppanen akieleza jambo kwa waandishi wa habari.
Picha ya pamoja.
................................................................................................
................................................................................................
Jamii hapa nchini imeaswa kutumia fursa iliyopo ya
ufugaji wa nyuki na upandaji wa miti kibiashara kujiinua kiuchumi.
Wito huo umetolewa jana na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili
na Utalii Bi. Gladyness Mkamba akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es
Salaam.
Bi.
Mkamba alisema kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya kuzalisha asali kwa wingi
duniani ambayo ikitumiwa ipasavyo itasaidia kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja
na taifa kwa ujumla.
"Kwa
sasa Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika ambapo inazalisha asali tani 34,000
kwa mwaka baada ya Ethiopia inayozalisha tani 56,000. Hata hivyo kiwango hicho
ni kidogo kwa kuwa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha asali tani 1,038,000 kwa
mwaka" Alieleza.
Akizungumzia
changamaoto kuu inayosababisha kiwango hicho kisifikiwe kirahisi, amesema ni
utashi hafifu wa jamii kujishuulisha na kazi za ufugaji nyuki na uhifadhi wa
mazingira ikiwemo upandaji wa miti.
Bi. Mkamba aliongeza kuwa Jamii ikihamasishwa vya
kutosha juu ya faida za ufugaji nyuki na upandaji wa miti inaweza kutoa matokeo
ya haraka kwa kuwa asali ina faida kubwa ikiwemo za kiafya na za kiuchumi.
Kwa upande wake Bi.
Magdalena Muya ambaye ni Mratibu Msaidizi wa mradi wa Kitaifa wa Misitu na Ufugaji wa Nyuki nchini (NFBKP II) ameeleza kuwa changamoto zingine zinazokwamisha
mafanikio katika sekta ya ufugaji nyuki nchini ni ukosefu wa teknolojia za kisasa
za ufugaji nyuki na uzalishaji wa asali pamoja na ukosefu wa mitaji ya
kuanzisha miradi mikubwa ya ufugaji wa nyuki.
Nae mshauri wa masuala ya Malisili kutoka Ubalozi
wa Finland hapa nchini Bw. Mikko Leppanen, ameeleza kuwa Misitu ya Tanzania
inakabiliwa na changamoto ya uharibifu mkubwa unaosababishwa na shughuli za
kibinadamu ambapo hupelekea ukame na kuathiri pia uzalishaji wa asali ambao
hutegemea malighafi za misitu.
Mshauri huyo ameiasa jamii hapa nchini kutunza
mazingira ya misitu, kupanda miti kibiashara na kuhifadhi mazingira ambayo
yatasaidia kuweka mazingira bora ya kuishi ikiwa ni pamoja na kuwezesha ufugaji
wa nyuki kibiashara na kuwainua watu kiuchumi.
Wakati huo huo Kaimu Mkurugenzi Idara ya Misitu na
Nyuki Wizara ya Maliasili Bi. Gladyness Mkamba akizungumza kwa niaba ya Katibu
Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Gen. Gaudence Milanzi wakati akifungua
mkutano wa siku moja wa mapitio ya kukamilisha Mradi wa Kitaifa wa Misitu na
Ufugaji wa Nyuki nchini (NFBKP II) ameishukuru Serikali ya Finland kwa kusaidia
ufadhili wa mradi huo.
Ameeleza kuwa mradi huo ambao bajeti yake ni Euro
Milioni 19.5 ambazo ni zaidi ya Tsh. Bilioni 47 kwasasa unafadhili mpango wa
miaka minne wa Misitu binafsi katika Mikoa ya Iringa, Njombe na Morogoro kwa
lengo la kuinua kipato cha wananchi wa vijijini katika Mikoa ya Kusini mwa
Tanzania, Mikoa hiyo ni shemu ya Mikoa saba ya jumla inayofadhiliwa na mradi
huo.
Amesema hayo yatafanyika kwa kuanzisha misitu ya
uhakika yenye faida na kuongeza thamani ya mazao yake kwenye mtiririko wa
uzalishaji kuanzia mbegu za miti hadi kwenye bidhaa bora za mbao.
Mradi
huo ulianza Oktoba mwaka 2013 hadi Oktoba 2015 na kuongezewa muda wa ziada wa
miezi minne ambapo unakamilika mwezi huu wa Februari 2016.
Subscribe to:
Posts (Atom)
