slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Sunday, August 7, 2016

KATIBU MKUU WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, MAJ. GEN. GAUDENCE MILANZI AONGOZA WATUMISHI WA WIZARA HIYO KUMUAGA ALIYEKUWA MKURUGENZI WA UTAWALA NA RASILIMALI WATU, SAID MSAMBACHI

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kushoto) akizungumza katika hafla fupi iliyoandaliwa na watumishi wa Wizara hiyo kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Utumishi, Said Msambachi (kulia) aliyestaafu rasmi kwa mujibu wa sheria tarehe 16 Juni, 2016. Hafla hiyo ilifanyika juzi tarehe 05 Agosti, 2016 katika ukumbi wa mikutano wa Selous, Makao Makuu wa Wizara hiyo, Jengo la Mpingo, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mstaafu wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Said Msambachi (kulia) akitoa nasaha zake kwa watumishi wa Wizara hiyo katika hafla fupi ya kumuaga iliyoandaliwa na watumishi hao tarehe 05 Agosti, 2016. Aliwaasa watumishi hao kutekeleza majukumu yao kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uaminifu kama chachu ya maendeleo yao kazini. Aliwataka pia kufanya kazi kwa ushirikiano kujiepusha na majungu, vitendo vya rushwa na ubaguzi pahala pa kazi. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maj. Gen. Gaudence Milanzi.
 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Utumishi, Ziana Mlawa (kushoto) akitoa shukurani kwa niaba ya watumishi wote kwa ushirikiano walioupata kutoka kwa Bw. Said Msambachi (kulia) katika kipindi chote cha miaka mitano alichofanya kazi katika Wizara hiyo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu, Idara ya Utawala na Utumishi, Aurelia Matagi, akitoa ufafanuzi wa ratiba na kuongoza utambulisho katika hafla hiyo.
Mkurugenzi Mstaafu wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Said Msambachi na Mama Msambachi wakikata Keki ya kuagwa waliyoandaliwa na watumishi wa Wizara hiyo.
Taswira ya keki hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (wa tatu kushoto) akimkabidhi Mkurugenzi Mstaafu wa Idara ya Utawala, Said Msambachi (wa pili kulia) risiti ya friji (pichani kulia) aliyozawadiwa na watumishi wa Wizara hiyo.
 Baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo katika hafla hiyo.
 Baadhi ya watumishi wa Wizara walioshiriki hafla hiyo.
 Baadhi ya watumishi wa Wizara katika hafla hiyo.
 Sehemu ya watumishi katika hafla hiyo.
 Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kushoto) akizungumza na watumishi walihudhuria hafla hiyo.
 Picha ya pamoja kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (wa pili kushoto, msatari wa mbele), Mkurugenzi Mstaafu wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Said Msambachi (wa tatu kushoto), Mkurugenzi anayekaimu nafasi yake kwa sasa ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala, Ziana Mlawa (kulia), Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu, Aurelia Matagi na Watumishi wa Wizara walioshiriki hafla hiyo (mstari wa pili na wa tatu nyuma) .
Picha ya pamoja kati ya Mkurugenzi Mstaafu wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Said Msambachi (katikati) na Mkurugenzi anayekaimu nafasi yake kwa sasa ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala, Ziana Mlawa (kulia) na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu, Aurelia Matagi (kushoto).

Monday, August 1, 2016

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI, ENG. RAMO MAKANI AONGEA NA WANANCHI WA KONDOA VIJIJINI KUHUSU UTATUZI WA MGOGORO WA PORI LA AKIBA MKUNGUNERO

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kulia) akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Keikei Wilayani Kondoa jana kwa ajili ya kusikiliza kero zao mbalimbali kuhusu Pori la Akiba Mkungunero. Wananchi hao wameiomba Serikali iwape maeneo kwa ajili ya Kilimo, Ufugaji na Makazi kutokana na uhaba wa ardhi katika maeneo hayo. 

Naibu Waziri Makani aliwaomba wananchi hao kuwa na subira wakati huu Serikali inapoenda kushuulikia maombi yao ambapo tayari imeshaundwa tume ambayo ipo chini ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kukusanya takwimu mbali mbali ikiwemo mahitaji halisi ya ardhi na idadi ya watu ambapo zitatumika katika kutatua changamoto zilizopo. 

Alieleza kuwa Serikali ya awamu ya tano imepanga kutatua kero mbalimbali za  wananchi ambapo tayari migogoro yote ya ardhi nchini imeshaorodheshwa kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu, ambapo kitaundwa kikosi kazi cha kitaifa kitakachohusisha Wizara ya Ardhi, Kilimo, Maliasili, Tamisemi, Sheria na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira.

Eng. Makani alisema kuwa Tanzania bado ina maeneo mengi ambayo yanaweza kutumika kwa ajili ya kilimo na ufugaji, hivyo kumega hifadhi ili kukabiliana na tatizo uhaba wa ardhi itakuwa jambo la mwisho kufanyika baada ya maeneo mengine kuzingatiwa. Aliitaka tume iliyoundwa kukamilisha kazi yake haraka ili changamoto hiyo iweze kupatiwa ufumbuzi na mamlaka husika.

Pori la Akiba Mkungunero lilitangazwa rasmi na Tangazo la Serikali la mwaka 1996 na zoezi la kutafsiri mipaka husika likafanyika mwaka 2006. Tangu hapo ukaanza mgogoro kati ya wananchi na hifadhi kwa madai kuwa baadhi ya vitongoji vya vijiji vyao halali vipo ndani ya hifadhi hiyo. 
Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini, Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji (kulia) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango akizungumza na wananchi wa Jimbo lake wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika kijiji cha keikei Wilayani Kondoa.

 Dkt. Kijaji aliwasilisha kero na changamoto mbalimbali za wananchi wake, moja ikiwa ni uhaba wa maeneo kwa ajili ya kilimo na ufugaji,  maeneo ya vijiji halali vilivyopimwa kudaiwa kuwemo ndani ya hifadhi na mahusiano mabaya kati ya wananchi wake na watumishi wa Pori la Akiba Mkungunero. 

Akijibu changamoto hizo, Naibu Waziri Makani aliahidi kuzifanyia kazi kwa mujibu wa sheria za nchi na taratibu zilizowekwa mara baada ya tume iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa kukamilisha kazi yake na kukabidhi taarifa na mapendekezo yake Wizarani.  Aliongeza kuwa kumega maeneo ya hifadhi haiwezi kuwa jibu pekee la changamoto zinazowakabili wananchi bali wanaweza kutumia maeneo madogo waliyonayo kwa kuweka mipango mizuri ikawa na tija zaidi kwa taifa na watu wake.
Mwananchi wa Kijiji cha Kisondoko, Khalifa Othman akiwasilisha kero zake wakati wa mkutano huo. Kilio chake kikubwa kilikuwa kupatiwa maeneo kwa ajili ya ufugaji na kilimo. Kulia aliyesimama ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Vijijini ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kwadelo, Omari Kariati. Kushoto ni Naibu Waziri, Eng. Ramo Makani.
  Mkazi wa Kijiji cha Kisondoko Wilayani Kondoa akitoa kero zake kwenye Mkutano huo. Aliiomba Serikali kuzisaidia jamii za Wabarbaij na Wamang'ati kupata maeneo ya kulima na kufuga kwakuwa kwa sasa jamii hizo zimetengwa na hazina kabisa maeneo kwa ajili ya shughuli hizo, "Sisi Wamang'ati hatuna hata kipande cha ardhi na tukifa hatujui tutazikwa wapi" alieleza. 
 Naibu Waziri Makani akiendelea kuongoza mkutano huo. Alifikisha salam za Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa wananchi hao ambapo aliwataka, Kudumisha amani ya nchi yetu, kutumia amani hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha zaidi kukuza uchumi wa taifa letu. 
Baadhi ya wajumbe walioshiriki mkutano huo.

Saturday, July 30, 2016

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI, ENG. RAMO MAKANI ATEMBELEA MAENEO YA HIFADHI YA MISITU NA WANYAMAPORI YENYE MIGOGORO MBALIMBALI MKOANI TABORA

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani akisaini kitabu cha wageni katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambapo alifanya ziara ya kikazi ya siku nne na kutembelea maeneo mbalimbali ya hifadhi ya Hifadhi ya Misitu na Wanyamapori yenye migogoro. Maeneo hayo ni Hifadhi ya Msitu wa Wembere (Wilaya ya Igunga), Eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Isawima (Wilaya ya Kaliua), Eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Ipole (Wilaya ya Skonge),  Msitu wa Hifadhi wa Ipembampazi (Wilaya ya Skonge) na Msitu wa hifadhi wa Ilomero (Wilaya ya Nzega).
 Naibu Waziri wa Maliasili, Eng. Ramo Makani akizungumza na baadhi ya wananchi waliovamia Msitu wa Hifadhi wa Wembere Wilayani Igunga hivi karibuni. Aliwataka wananchi hao kutii sheria za nchi na kusubiri maelekezo ya Serikali ambapo aliwaagiza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya Igunga na Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) kukusanya taarifa mbalimbali zinazohusu hifadhi hiyo na vijiji jirani ambapo zitatumika kumaliza mgogoro huo.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani akizungumza na wananchi wa waliovamia Msitu wa Wembere na kuweka makazi, Wilayani Igunga hivi karibuni. Alitoa maelekezo mbali kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya na Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania kwa ajili ya kukabili changamoto zilizopo katika hifadhi hiyo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani akizungumza na Viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Igunga pamoja na viongozi wengine kutoka Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA). 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa pili kushoto) akikagua maeneo ya Hifadhi ya Msitu wa Isawima Wilayani Kaliua hivi karibuni. Hifadhi hiyo ambayo imetengwa na vijiji 11 kwa ajili ya kuanzishwa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Isawima umevamiwa na wananchi kutoka maeneo ya nje ya vijiji hivyo na kuweka makazi, mifugo na kilimo jambo lililoikwamisha jumuiya hiyo kupewa kibali cha kurasimishwa na Wizara ya Maliasili na Utalii. Eng. Makani alitoa maelekezo kwa uongozi wa Wilaya ya Kaliua na Halmashauri kutumia mamlaka ya kisheria waliyo nayo kuwahamisha wavamizi hao ili jumuiya hiyo iweze kuanzishwa. 
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Wachawaseme, Wilayani Kaliua wakiwa kwenye Mkutano wa Hadhara wa Naibu Waziri wa Maliasili, Eng. Ramo Makani.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kushoto) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Wachawaseme, Wilayani Kaliua alipotembelea kuona changamoto wa Uhifadhi na kuweka utaratibu wa kuzikabili.
Mmoja wa wananchi waliovamia Hifadhi ya Isawima, Kaliua, Charles Msinda (kulia) akiiomba Serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Maliasili, Eng. Ramo Makani (wa pili kulia) iwafikirie kuwapa maeneo mbadala baada ya kuondoka katika Hifadhi ya Msitu huo. 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (katikati) akizungumza na viongozi wa Chama (CCM) na Serikali Wilayani Skonge. Kulia kwake ni mkuu wa Wilaya hiyo, Peres Boniface.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani akizungumza na jamii wa wavuvi wa Mto Koga, Wilayani Skonge ikiwa na hatua ya kusuluhisha mgogoro kati yao na muwekezaji, Muhsin Abdllah "Shein" ambaye ni Mkurugenzi wa Northern Hunting. Eng. Makani aliwataka viongozi wa Wilaya na Halmashauri kukaa pamoja na muwekezaji huyo na wadau mbaimbali kwa ajili ya kamaliza mgogoro huo. Aliwata viongozi hao kuangaliwa upya vibali vinavyotolewa kwa wavuvi hao ili idadi yake ilingane na ukubwa na mahitaji ya Mto huo.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kulia) akisikiliza malalamiko kutoka kwa muwekezaji ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Northern Hunting, Muhsin Abdallah (kushoto)  aliyewekeza katika kitalu cha uwindaji kwenye Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Ipole Wilayani Skonge.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ipembampazi, Wilayani Skonge Tabora. Wananchi hao wameiomba Serikali iwamegee eneo la hifadhi kwa ajili mradi wa kilimo cha umwagiliaji, Uluwa, Hifadhi ya Msitu ambao upo chini ya Halmashauri ya Wilaya Kaliua. Eng. Makani alitoa maelekezo mbalimbali kwa Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya na Mkoa ikiwa ni pamoja kuangalia taratibu za kisheria na kimazingira juu ya uwezekano wa ombi hilo na kuliwasilisha Wizarani kwa ajili ya hatua zaidi. 

Tuesday, July 26, 2016

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI, ENG. RAMO MAKANI AZINDUA MIRADI YA TANAPA CHAMWINO, DODOMA, ASEMA TATIZO LA WANYAMAPORI KUVAMIA MAKAZI YA WATU KUPATIWA UFUMBUZI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kushoto) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ilangali Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma jana muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi katika zahanati ya kijiji hicho. Mradi huo wa zahanati umefadhiliwa kwa ushirikiano wa TANAPA Tsh. Milioni 25, Mbunge wa Jimbo la Mtera (Livingstone Lusinde) Tsh. Milioni 14.3 na Wananchi wa kjiji hicho Tsh. Milioni 12. 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kushoto) akizindua mradi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari Maila iliyopo Chamwino, Dodoma jana, mradi huo umefadhiliwa kwa ushirikiano wa TANAPA kupitia Mradi wa Ujirani Mwema, Tsh. Milioni 115.83 na Wananchi wa Kata ya Manda Tsh. Milioni 33.72. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Mtera, Lingstone Lusinde.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga (kulia) Hati ya Makabidhiano ya mradi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari Maila iliyopo Chamwino, Dodoma jana, mradi huo umefadhiliwa kwa ushirikiano wa TANAPA kupitia Mradi wa Ujirani Mwema,  Tsh. Milioni 115.83 na Wananchi wa Kata ya Manda Tsh. Milioni 33.72. Watano kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Witness Shoo.
 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Tanzania - TANAPA  ambaye pia Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Shirika hilo, Witness Shoo akitoa taarifa ya juu ya miradi miwili iliyofadhiliwa na Shirika hilo katika vijiji vya Ilangali na Manda. Alisema shirika hilo limechangia Tsh. Milioni 148.3 kupitia mradi wa Ujirani Mwema. 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa pili kulia) akikagua vitanda vya mradi wa bweni la wasichana wa shule ya Sekondari Maila iliyopo Chamwino, Dodoma jana, mradi huo umefadhiliwa kwa ushirikiano wa TANAPA kupitia Mradi wa Ujirani Mwema, Tsh. Milioni 115.83 na Wananchi wa Kata ya Manda Tsh. Milioni 33.72. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Mtera, Lingstone Lusinde na Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Samuel Amon (wa tatu kulia).
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa tatu kulia) akiongoza msafara kukagua fensi ya bweni la wasichana katika shule ya Sekondari Maila muda mfupi kabla ya kuzinduliwa. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Witness Shoo na Mbunge wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde (wanne kulia)
 Picha ya pamoja.
 Taswira ya jengo la Zahanati ya kijiji cha Ilangali lililofadhiliwa na TANAPA
 Taswira ya jengo la Bweni la Wasichana shule ya Sekondari Maila lililofadhiliwa na TANAPA.
____________________________________

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imepanga kulipatia ufumbuzi tatizo la uvamizi wa Wanyamapori kwenye makazi ya watu wanaozunguka Hifadhi zenye Wanyamapori nchini kwa kuwashirikisha wananchi wa vijiji hivyo, kuwapatia mafunzo na silaha maalum za kujilinda na kufukuza wanyamapori hao wakati wa dharua.

Hayo yalibainishwa jana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Eng. Ramo Makani akizungumza na wananchi wa vijiji vya Manda na Ilangali Wilayani Chamwino Mkoa wa Dodoma wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi na uzinduzi wa miradi iliyofadhiliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kupitia Mradi wa Ujirani Mwema katika vijiji hivyo.

Akijibu kero iliyowasilishwa kwake na Mbunge wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinge katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye vijiji hivyo kuhusu Wanyamapori wanaovamia maeneo ya vijiji vya jirani na Hifadhi ya Ruaha na kuharibu mazao ya wananchi, Eng. Makani alisema, changamoto hiyo inashuulikiwa kwa upana wake na kwamba Serikali inakuja na mpango wa kukabiliana nayo kwa kuwashirikisha wananchi wa vijiji husika.

Akizungumzia mpango huo alisema kuwa Serikali itaanzisha mafunzo maalum ya kujikinga na Wanyamapori kwa baadhi ya wananchi watakaoainishwa kwenye maeneo husika na kupewa silaha maalum kwa ajili ya kuwafukuza kabla ya kuleta madhara. Aliongeza kuwa Askari wa Wanyamapori waliopo pamoja na changamoto za kijiografia za baadhi ya maeneo hawatoshi kulinda maeneo yote ya vijijini hususani wakati wa dharua hivyo kwa kuwapa mafunzo na zana na kujilinda baadhi ya wananchi itasaidia katika kukabilina na tatizo hilo kwa wakati.

Katika hatua za maandalizi ya awali ya mpango huo, aliwaagiza viongozi wa vijiji vya Ilangali na Manda ambavyo vinayozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kuanza kazi ya kutambua vijana wakakamavu, wenye elimu, uadilifu, uaminifu na maadili bora kuanzia watano hadi kumi kwa ajili ya kujiunga na mpango huo pale utakapokuwa tayari kuingia kwenye hatua ya utekelezaji.

Hapo awali akiweka jiwe la msingi kwenye mradi wa zahanati ya kijiji cha Ilangali na baadae kuzindua mradi wa bweni la wasichana shule ya Sekondari Maila  iliyofadhiliwa na TANAPA, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, Naibu Waziri, Eng. Makani alisema kuwa misaada hiyo ni sehemu faida za uhifadhi ambayo wananchi wananufaika nayo kwa kushirikiana na Serikali katika uhifadhi. Aliwataka wananchi hao kuendelea kushirikiana na Serikali katika uhifadhi ili faida kama hizo ziendelee kupatikana kwa wingi kwa kuwa uhifadhi ukiimarika na wanyamapori wakaongezeka na utalii nao utakua na kuongeza mapato zaidi.

"Fedha zilizotumika katika Mradi huu tunaoushuhudia hapa leo ni sehemu ya faida za Uhifadhi, tunawaomba sana wananchi muendelee kuunga mkono juhudi za Serikali za kulinda Wanyamapori na kupiga vita ujangili, tuendelee kulinda chanzo cha fedha hizo, tukipata watalii wengi zaidi na fedha hizo zitaongezeka maradufu. Alisema Makani.

Akizungumzia miradi hiyo miwili, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Shirika hilo, Witness Shoo alisema kuwa shirika hilo limechangia Tsh. Milioni 148.3 katika miradi hiyo ya Ujirani Mwema. Aliongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 1994 - 95 na 2014 - 15 Shirika hilo limechangia jumla ya Tsh. Bilioni 2 kwa vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha katika miradi ya sekta ya  ya elimu, maji, afya na uhifadhi kwa ujumla.

Sunday, July 24, 2016

NAIBU WAZIRI WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, ENG. RAMO MAKANI ATEMBELEA TAASISI TA TAALUMA YA WANYAMAPORI PASIANSI MKOANI MWANZA

 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani akisallimiana na watumishi wa Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi Mkoani Mwanza alipotembelea chuoni hapo tarehe 22 Julai, 206.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kulia) akipanda mti wa kumbukumbu kwa kutembelea Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori ya Pasiansi iliyopo Mkoani Mwanza kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kuwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Taasisi hiyo, Lowaeli Damalu.
  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa pili kulia) akikagua mazingira ya Taasisi hiyo. Kulia ni Mkuu wa Taasisi hiyo, Lowaeli Damalu.
  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wanne kushoto) akizungumza na Mkandarasi anayejenga Jiko na Bwalo la Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi. Jiko na Bwalo hilo linapanuliwa liweze kukidhi mahitaji ya wanfunzi chuoni hapo.
  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa pili kushoto) akizungumza na watumishi na wakufunzi wa Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori ya Pasiansi alipotembelea chuoni hapo hivi karibuni.
Mkufunzi wa mafunzo ya kijeshi katika Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori ya Pasiansi, Koplo Jamal Said Mbaruku akichangia katika mkutano na Naibu Waziri.

Saturday, July 23, 2016

NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII, ENG. RAMO MAKANI ATEKELEZA AHADI YA SERIKALI ALIYOITOA BUNGENI YA KUTEMBELEA ENEO LA MGOGORO WA HIFADHI YA MSITU WA SAYAKA MKOANI MWANZA KWA AJILI YA KUUTAFUTIA SULUHU YA KUDUMU

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa pili kulia) akikagua eneo la mpaka katika Msitu wa Hifadhi wa Sayaka katika Kijiji cha Bugatu, Wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza hivi karibuni. Anayeongoza utambuzi wa mpaka huo ni Afisa Misitu na Nyuki TFS Wilaya ya Magu, Ayoub Mikae (wa tatu kulia). Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Magu, Boniventure Kiswaga.  Eng. Makani aliahidi kwa niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi yenye migogoro nchini kwa ajili ya kutafutiwa suluhu ya kudumu. 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa sita kushoto) akiwa na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Magu na baadhi ya Wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Msitu wa Sayaka wakikagua mpaka wa hifadhi hiyo hivi karibuni. Kinachoonekana mbele yao ni Kigingi cha mpaka kinachodaiwa kusogezwa mbele na wananchi wa maeneo hayo kwa ajili ya kumega eneo la Hifadhi. 
  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kulia) akizungumza na wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Msitu wa Sayaka katika Kijiji cha Bugatu Wilayani Magu Mkoani Mwanza hivi karibuni. Aliahidi kwa niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi yenye migogoro nchini na kutafutiwa suluhu ya kudumu. 
Naibu Waziri Maliasili , Eng. Ramo Makani (kulia) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Bugatu, Wilaya ya Magu, Mkoani Mwanza hivi karibuni wakati akikagua ramani ya Hifadhi ya Msitu wa Sayaka kubaini maeneo ya mpaka yenye mgogoro. Eng. Makani aliahidi kwa niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi yenye migogoro nchini kwa ajili ya kutafutiwa suluhu ya kudumu
Mbunge wa Jimbo la Magu, Boniventure Kiswaga (kulia) akizungumza na wananchi wa Jimbo lake katika Kijiji cha Bugatu Wilayani Magu hivi karibuni.
Mwananchi wa Kijiji cha Salama kilichopo kandokando ya Hifadhi ya Msitu wa Sayaka Wilayani Magu, Charles Kassandiga (kushoto) akitoa ombi kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho la kupatiwa maeneo ya kulima na kufuga kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kulia). Eng. Makani aliahidi kwa niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi yenye migogoro nchini na kutafutiwa suluhu ya kudumu. 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kushoto) akiongoza kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama cha Wilaya ya Magu alipotembelea Wilayani humo hivi karibuni kuona eneo la mgogoro katika Hifadhi ya Msitu wa Sayaka ambapo aliahidi kwa niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi yenye migogoro nchini na kutafutiwa suluhu ya kudumu.
_____________________________________
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeahidi kupitia upya maeneo yote ya Hifadhi nchini yenye migogoro ya ardhi kwa ajili ya kuyatafutia suluhu ya kudumu kwa kutumia mbinu shirikishi.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Eng. Ramo Makani wakati akizungumza na Wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Msitu wa Sayaka katika Kijiji cha Busega Wilayani Magu Mkoani Mwanza.

Eng. Makani alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano imekusudia kubadilisha mfumo wa utendaji Serikali ambapo kwenye utatuzi wa migogoro iliyopo kwenye maeneo ya hifadhi nchini itatatuliwa kwa kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika na kuweka kumbukumbu sahihi za makubaliano kufikia suluhu ya kudumu.

“Maeneo yote yenye migogoro tunaenda kuyapitia upya, tukija kwenye utatuzi tutawashirikisha wananchi kupitia Serikali zao za Vijiji ambazo wajumbe wake watahusika kwenye makubaliano kwa kuzingatia umuhimu na faida za Uhifadhi lakini huku tukihakikisha tunajibu kero zinazowakabili” Aliesema Eng. Makani.

Aliongeza kuwa wakati wa kutatua migogoro hiyo yataainishwa maeneo kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kilimo kuepusha muingiliano kati ya wakulima na wafugaji pamoja na kuepusha uvamizi kwenye maeneo ya Hifadhi yaliyoainishwa, utaratibu huo utazingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya Serikali.

Awali akizungumzia mgogoro wa Hifadhi ya Msitu wa Sayaka, Eng. Makani alisema kuwa, uamuzi wa kufika katika eneo hilo la mgogoro ni kuona uhalisia kabla ya kuchukuliwa hatua za kumaliza mgogoro huo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali aliyoitoa bungeni hivi karibuni kwa Mbunge wa Jimbo la Magu, Boniventure Kiswaga.

Katika mgogoro huo wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi hiyo walitoa malalamiko yao kwa Naibu Waziri Makani kuwa maofisa wa TFS wamekuwa wakisogeza vigingi vya mpaka wa eneo hilo kumega maeneo ya vijiji bila kuwashirikisha. “Sio kwamba tunapinga Uhifadhi, lakini tunauliza kwanini vigingi vinahama kila mwaka kusogelea maeneo yetu” Alihoji Mwanyekiti wa Kijiji cha Bugatu, Charles Kusenza.

Akijibu malalamiko hayo Afisa Misitu na Nyuki wa TFS Wilaya ya Magu, Ayoub Mikae alisema kuwa, kilichokuwa kinafanyika sio kusogeza vigingi bali na kuimarisha vigingi vilivyokuwepo ambapo utambuzi wake ulifanyika kitaalam kwa kutumia GPS. Aliongeza kuwa baadhi ya wananchi wasio waadilifu walidaiwa kusogeza vigingi vya mpaka wa Hifadhi hiyo ili wapate eneo la kulima jambo lililoleta taswira tofauti wakati wa kufanya marekebisho sahihi kwa kutumia mtambo wa GPS uliosaidia kubaini mpaka asilia.

Ayoub alisema kuwa sababu ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu Sayaka ilikuwa ni kuhifadhi uoto wa asili, kutunza vyanzo vya maji na kuhifadhi samaki wa Ziwa Victoria kwa kuwa mto uliopo katika hifadhi hiyo unapeleka maji Ziwa Victoria.

Baada ya kusikiliza hoja mbalimbali za wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi hiyo katika mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Bugatu, Eng. Makani alisema kuwa tatizo kubwa aliloliona katika mgogoro huo ni changamoto za Uhifadhi ikiwemo uelewa hafifu wa baadhi ya wananchi juu ya umuhimu wa uhifadhi, ushirikishwaji hafifu wa wananchi kwenye uwekaji wa vigingi na baadhi ya wananchi kuchanganya vigingi vya hifadhi ya maji na hifadhi ya Msitu, changamoto ambazo alisema zitazingatiwa kwa kina wakati wa utatuzi wa mgogoro huo.

Alisema kuwa “Tunahitaji uhifadhi endelevu, peke yetu bila wananchi hatuwezi, tunahitaji uhifadhi rafiki, tukiwa na uelewa wa pamoja juu ya umuhimu wa uhifadhi na tukajibu kero zenu mtatusaidia kulinda na kuhifadhi Maliasili zetu”. 

Kwa upande wa Wananchi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo waliopewa fursa ya kuchangia na kuuliza maswali kwenye mkutano huo walipaza sauti zao kuiomba Serikali kupitia Naibu Waziri huyo kuwasaidia maeneo ya kufuga na kulima kutokana na ufinyu wa maeneo uliosababishwa na ongezeko kubwa la watu. Naibu Waziri Makani Aliahidi kwa niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi nchini yenye migogoro na kuyatafutiwa suluhu ya kudumu kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya Serikali.