slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Saturday, July 30, 2016

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI, ENG. RAMO MAKANI ATEMBELEA MAENEO YA HIFADHI YA MISITU NA WANYAMAPORI YENYE MIGOGORO MBALIMBALI MKOANI TABORA

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani akisaini kitabu cha wageni katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambapo alifanya ziara ya kikazi ya siku nne na kutembelea maeneo mbalimbali ya hifadhi ya Hifadhi ya Misitu na Wanyamapori yenye migogoro. Maeneo hayo ni Hifadhi ya Msitu wa Wembere (Wilaya ya Igunga), Eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Isawima (Wilaya ya Kaliua), Eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Ipole (Wilaya ya Skonge),  Msitu wa Hifadhi wa Ipembampazi (Wilaya ya Skonge) na Msitu wa hifadhi wa Ilomero (Wilaya ya Nzega).
 Naibu Waziri wa Maliasili, Eng. Ramo Makani akizungumza na baadhi ya wananchi waliovamia Msitu wa Hifadhi wa Wembere Wilayani Igunga hivi karibuni. Aliwataka wananchi hao kutii sheria za nchi na kusubiri maelekezo ya Serikali ambapo aliwaagiza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya Igunga na Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) kukusanya taarifa mbalimbali zinazohusu hifadhi hiyo na vijiji jirani ambapo zitatumika kumaliza mgogoro huo.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani akizungumza na wananchi wa waliovamia Msitu wa Wembere na kuweka makazi, Wilayani Igunga hivi karibuni. Alitoa maelekezo mbali kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya na Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania kwa ajili ya kukabili changamoto zilizopo katika hifadhi hiyo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani akizungumza na Viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Igunga pamoja na viongozi wengine kutoka Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA). 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa pili kushoto) akikagua maeneo ya Hifadhi ya Msitu wa Isawima Wilayani Kaliua hivi karibuni. Hifadhi hiyo ambayo imetengwa na vijiji 11 kwa ajili ya kuanzishwa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Isawima umevamiwa na wananchi kutoka maeneo ya nje ya vijiji hivyo na kuweka makazi, mifugo na kilimo jambo lililoikwamisha jumuiya hiyo kupewa kibali cha kurasimishwa na Wizara ya Maliasili na Utalii. Eng. Makani alitoa maelekezo kwa uongozi wa Wilaya ya Kaliua na Halmashauri kutumia mamlaka ya kisheria waliyo nayo kuwahamisha wavamizi hao ili jumuiya hiyo iweze kuanzishwa. 
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Wachawaseme, Wilayani Kaliua wakiwa kwenye Mkutano wa Hadhara wa Naibu Waziri wa Maliasili, Eng. Ramo Makani.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kushoto) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Wachawaseme, Wilayani Kaliua alipotembelea kuona changamoto wa Uhifadhi na kuweka utaratibu wa kuzikabili.
Mmoja wa wananchi waliovamia Hifadhi ya Isawima, Kaliua, Charles Msinda (kulia) akiiomba Serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Maliasili, Eng. Ramo Makani (wa pili kulia) iwafikirie kuwapa maeneo mbadala baada ya kuondoka katika Hifadhi ya Msitu huo. 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (katikati) akizungumza na viongozi wa Chama (CCM) na Serikali Wilayani Skonge. Kulia kwake ni mkuu wa Wilaya hiyo, Peres Boniface.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani akizungumza na jamii wa wavuvi wa Mto Koga, Wilayani Skonge ikiwa na hatua ya kusuluhisha mgogoro kati yao na muwekezaji, Muhsin Abdllah "Shein" ambaye ni Mkurugenzi wa Northern Hunting. Eng. Makani aliwataka viongozi wa Wilaya na Halmashauri kukaa pamoja na muwekezaji huyo na wadau mbaimbali kwa ajili ya kamaliza mgogoro huo. Aliwata viongozi hao kuangaliwa upya vibali vinavyotolewa kwa wavuvi hao ili idadi yake ilingane na ukubwa na mahitaji ya Mto huo.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kulia) akisikiliza malalamiko kutoka kwa muwekezaji ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Northern Hunting, Muhsin Abdallah (kushoto)  aliyewekeza katika kitalu cha uwindaji kwenye Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Ipole Wilayani Skonge.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ipembampazi, Wilayani Skonge Tabora. Wananchi hao wameiomba Serikali iwamegee eneo la hifadhi kwa ajili mradi wa kilimo cha umwagiliaji, Uluwa, Hifadhi ya Msitu ambao upo chini ya Halmashauri ya Wilaya Kaliua. Eng. Makani alitoa maelekezo mbalimbali kwa Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya na Mkoa ikiwa ni pamoja kuangalia taratibu za kisheria na kimazingira juu ya uwezekano wa ombi hilo na kuliwasilisha Wizarani kwa ajili ya hatua zaidi. 

Tuesday, July 26, 2016

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI, ENG. RAMO MAKANI AZINDUA MIRADI YA TANAPA CHAMWINO, DODOMA, ASEMA TATIZO LA WANYAMAPORI KUVAMIA MAKAZI YA WATU KUPATIWA UFUMBUZI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kushoto) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ilangali Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma jana muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi katika zahanati ya kijiji hicho. Mradi huo wa zahanati umefadhiliwa kwa ushirikiano wa TANAPA Tsh. Milioni 25, Mbunge wa Jimbo la Mtera (Livingstone Lusinde) Tsh. Milioni 14.3 na Wananchi wa kjiji hicho Tsh. Milioni 12. 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kushoto) akizindua mradi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari Maila iliyopo Chamwino, Dodoma jana, mradi huo umefadhiliwa kwa ushirikiano wa TANAPA kupitia Mradi wa Ujirani Mwema, Tsh. Milioni 115.83 na Wananchi wa Kata ya Manda Tsh. Milioni 33.72. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Mtera, Lingstone Lusinde.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga (kulia) Hati ya Makabidhiano ya mradi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari Maila iliyopo Chamwino, Dodoma jana, mradi huo umefadhiliwa kwa ushirikiano wa TANAPA kupitia Mradi wa Ujirani Mwema,  Tsh. Milioni 115.83 na Wananchi wa Kata ya Manda Tsh. Milioni 33.72. Watano kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Witness Shoo.
 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Tanzania - TANAPA  ambaye pia Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Shirika hilo, Witness Shoo akitoa taarifa ya juu ya miradi miwili iliyofadhiliwa na Shirika hilo katika vijiji vya Ilangali na Manda. Alisema shirika hilo limechangia Tsh. Milioni 148.3 kupitia mradi wa Ujirani Mwema. 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa pili kulia) akikagua vitanda vya mradi wa bweni la wasichana wa shule ya Sekondari Maila iliyopo Chamwino, Dodoma jana, mradi huo umefadhiliwa kwa ushirikiano wa TANAPA kupitia Mradi wa Ujirani Mwema, Tsh. Milioni 115.83 na Wananchi wa Kata ya Manda Tsh. Milioni 33.72. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Mtera, Lingstone Lusinde na Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Samuel Amon (wa tatu kulia).
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa tatu kulia) akiongoza msafara kukagua fensi ya bweni la wasichana katika shule ya Sekondari Maila muda mfupi kabla ya kuzinduliwa. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Witness Shoo na Mbunge wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde (wanne kulia)
 Picha ya pamoja.
 Taswira ya jengo la Zahanati ya kijiji cha Ilangali lililofadhiliwa na TANAPA
 Taswira ya jengo la Bweni la Wasichana shule ya Sekondari Maila lililofadhiliwa na TANAPA.
____________________________________

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imepanga kulipatia ufumbuzi tatizo la uvamizi wa Wanyamapori kwenye makazi ya watu wanaozunguka Hifadhi zenye Wanyamapori nchini kwa kuwashirikisha wananchi wa vijiji hivyo, kuwapatia mafunzo na silaha maalum za kujilinda na kufukuza wanyamapori hao wakati wa dharua.

Hayo yalibainishwa jana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Eng. Ramo Makani akizungumza na wananchi wa vijiji vya Manda na Ilangali Wilayani Chamwino Mkoa wa Dodoma wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi na uzinduzi wa miradi iliyofadhiliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kupitia Mradi wa Ujirani Mwema katika vijiji hivyo.

Akijibu kero iliyowasilishwa kwake na Mbunge wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinge katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye vijiji hivyo kuhusu Wanyamapori wanaovamia maeneo ya vijiji vya jirani na Hifadhi ya Ruaha na kuharibu mazao ya wananchi, Eng. Makani alisema, changamoto hiyo inashuulikiwa kwa upana wake na kwamba Serikali inakuja na mpango wa kukabiliana nayo kwa kuwashirikisha wananchi wa vijiji husika.

Akizungumzia mpango huo alisema kuwa Serikali itaanzisha mafunzo maalum ya kujikinga na Wanyamapori kwa baadhi ya wananchi watakaoainishwa kwenye maeneo husika na kupewa silaha maalum kwa ajili ya kuwafukuza kabla ya kuleta madhara. Aliongeza kuwa Askari wa Wanyamapori waliopo pamoja na changamoto za kijiografia za baadhi ya maeneo hawatoshi kulinda maeneo yote ya vijijini hususani wakati wa dharua hivyo kwa kuwapa mafunzo na zana na kujilinda baadhi ya wananchi itasaidia katika kukabilina na tatizo hilo kwa wakati.

Katika hatua za maandalizi ya awali ya mpango huo, aliwaagiza viongozi wa vijiji vya Ilangali na Manda ambavyo vinayozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kuanza kazi ya kutambua vijana wakakamavu, wenye elimu, uadilifu, uaminifu na maadili bora kuanzia watano hadi kumi kwa ajili ya kujiunga na mpango huo pale utakapokuwa tayari kuingia kwenye hatua ya utekelezaji.

Hapo awali akiweka jiwe la msingi kwenye mradi wa zahanati ya kijiji cha Ilangali na baadae kuzindua mradi wa bweni la wasichana shule ya Sekondari Maila  iliyofadhiliwa na TANAPA, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, Naibu Waziri, Eng. Makani alisema kuwa misaada hiyo ni sehemu faida za uhifadhi ambayo wananchi wananufaika nayo kwa kushirikiana na Serikali katika uhifadhi. Aliwataka wananchi hao kuendelea kushirikiana na Serikali katika uhifadhi ili faida kama hizo ziendelee kupatikana kwa wingi kwa kuwa uhifadhi ukiimarika na wanyamapori wakaongezeka na utalii nao utakua na kuongeza mapato zaidi.

"Fedha zilizotumika katika Mradi huu tunaoushuhudia hapa leo ni sehemu ya faida za Uhifadhi, tunawaomba sana wananchi muendelee kuunga mkono juhudi za Serikali za kulinda Wanyamapori na kupiga vita ujangili, tuendelee kulinda chanzo cha fedha hizo, tukipata watalii wengi zaidi na fedha hizo zitaongezeka maradufu. Alisema Makani.

Akizungumzia miradi hiyo miwili, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Shirika hilo, Witness Shoo alisema kuwa shirika hilo limechangia Tsh. Milioni 148.3 katika miradi hiyo ya Ujirani Mwema. Aliongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 1994 - 95 na 2014 - 15 Shirika hilo limechangia jumla ya Tsh. Bilioni 2 kwa vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha katika miradi ya sekta ya  ya elimu, maji, afya na uhifadhi kwa ujumla.

Sunday, July 24, 2016

NAIBU WAZIRI WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, ENG. RAMO MAKANI ATEMBELEA TAASISI TA TAALUMA YA WANYAMAPORI PASIANSI MKOANI MWANZA

 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani akisallimiana na watumishi wa Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi Mkoani Mwanza alipotembelea chuoni hapo tarehe 22 Julai, 206.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kulia) akipanda mti wa kumbukumbu kwa kutembelea Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori ya Pasiansi iliyopo Mkoani Mwanza kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kuwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Taasisi hiyo, Lowaeli Damalu.
  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa pili kulia) akikagua mazingira ya Taasisi hiyo. Kulia ni Mkuu wa Taasisi hiyo, Lowaeli Damalu.
  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wanne kushoto) akizungumza na Mkandarasi anayejenga Jiko na Bwalo la Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi. Jiko na Bwalo hilo linapanuliwa liweze kukidhi mahitaji ya wanfunzi chuoni hapo.
  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa pili kushoto) akizungumza na watumishi na wakufunzi wa Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori ya Pasiansi alipotembelea chuoni hapo hivi karibuni.
Mkufunzi wa mafunzo ya kijeshi katika Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori ya Pasiansi, Koplo Jamal Said Mbaruku akichangia katika mkutano na Naibu Waziri.

Saturday, July 23, 2016

NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII, ENG. RAMO MAKANI ATEKELEZA AHADI YA SERIKALI ALIYOITOA BUNGENI YA KUTEMBELEA ENEO LA MGOGORO WA HIFADHI YA MSITU WA SAYAKA MKOANI MWANZA KWA AJILI YA KUUTAFUTIA SULUHU YA KUDUMU

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa pili kulia) akikagua eneo la mpaka katika Msitu wa Hifadhi wa Sayaka katika Kijiji cha Bugatu, Wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza hivi karibuni. Anayeongoza utambuzi wa mpaka huo ni Afisa Misitu na Nyuki TFS Wilaya ya Magu, Ayoub Mikae (wa tatu kulia). Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Magu, Boniventure Kiswaga.  Eng. Makani aliahidi kwa niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi yenye migogoro nchini kwa ajili ya kutafutiwa suluhu ya kudumu. 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa sita kushoto) akiwa na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Magu na baadhi ya Wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Msitu wa Sayaka wakikagua mpaka wa hifadhi hiyo hivi karibuni. Kinachoonekana mbele yao ni Kigingi cha mpaka kinachodaiwa kusogezwa mbele na wananchi wa maeneo hayo kwa ajili ya kumega eneo la Hifadhi. 
  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kulia) akizungumza na wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Msitu wa Sayaka katika Kijiji cha Bugatu Wilayani Magu Mkoani Mwanza hivi karibuni. Aliahidi kwa niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi yenye migogoro nchini na kutafutiwa suluhu ya kudumu. 
Naibu Waziri Maliasili , Eng. Ramo Makani (kulia) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Bugatu, Wilaya ya Magu, Mkoani Mwanza hivi karibuni wakati akikagua ramani ya Hifadhi ya Msitu wa Sayaka kubaini maeneo ya mpaka yenye mgogoro. Eng. Makani aliahidi kwa niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi yenye migogoro nchini kwa ajili ya kutafutiwa suluhu ya kudumu
Mbunge wa Jimbo la Magu, Boniventure Kiswaga (kulia) akizungumza na wananchi wa Jimbo lake katika Kijiji cha Bugatu Wilayani Magu hivi karibuni.
Mwananchi wa Kijiji cha Salama kilichopo kandokando ya Hifadhi ya Msitu wa Sayaka Wilayani Magu, Charles Kassandiga (kushoto) akitoa ombi kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho la kupatiwa maeneo ya kulima na kufuga kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kulia). Eng. Makani aliahidi kwa niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi yenye migogoro nchini na kutafutiwa suluhu ya kudumu. 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kushoto) akiongoza kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama cha Wilaya ya Magu alipotembelea Wilayani humo hivi karibuni kuona eneo la mgogoro katika Hifadhi ya Msitu wa Sayaka ambapo aliahidi kwa niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi yenye migogoro nchini na kutafutiwa suluhu ya kudumu.
_____________________________________
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeahidi kupitia upya maeneo yote ya Hifadhi nchini yenye migogoro ya ardhi kwa ajili ya kuyatafutia suluhu ya kudumu kwa kutumia mbinu shirikishi.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Eng. Ramo Makani wakati akizungumza na Wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Msitu wa Sayaka katika Kijiji cha Busega Wilayani Magu Mkoani Mwanza.

Eng. Makani alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano imekusudia kubadilisha mfumo wa utendaji Serikali ambapo kwenye utatuzi wa migogoro iliyopo kwenye maeneo ya hifadhi nchini itatatuliwa kwa kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika na kuweka kumbukumbu sahihi za makubaliano kufikia suluhu ya kudumu.

“Maeneo yote yenye migogoro tunaenda kuyapitia upya, tukija kwenye utatuzi tutawashirikisha wananchi kupitia Serikali zao za Vijiji ambazo wajumbe wake watahusika kwenye makubaliano kwa kuzingatia umuhimu na faida za Uhifadhi lakini huku tukihakikisha tunajibu kero zinazowakabili” Aliesema Eng. Makani.

Aliongeza kuwa wakati wa kutatua migogoro hiyo yataainishwa maeneo kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kilimo kuepusha muingiliano kati ya wakulima na wafugaji pamoja na kuepusha uvamizi kwenye maeneo ya Hifadhi yaliyoainishwa, utaratibu huo utazingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya Serikali.

Awali akizungumzia mgogoro wa Hifadhi ya Msitu wa Sayaka, Eng. Makani alisema kuwa, uamuzi wa kufika katika eneo hilo la mgogoro ni kuona uhalisia kabla ya kuchukuliwa hatua za kumaliza mgogoro huo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali aliyoitoa bungeni hivi karibuni kwa Mbunge wa Jimbo la Magu, Boniventure Kiswaga.

Katika mgogoro huo wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi hiyo walitoa malalamiko yao kwa Naibu Waziri Makani kuwa maofisa wa TFS wamekuwa wakisogeza vigingi vya mpaka wa eneo hilo kumega maeneo ya vijiji bila kuwashirikisha. “Sio kwamba tunapinga Uhifadhi, lakini tunauliza kwanini vigingi vinahama kila mwaka kusogelea maeneo yetu” Alihoji Mwanyekiti wa Kijiji cha Bugatu, Charles Kusenza.

Akijibu malalamiko hayo Afisa Misitu na Nyuki wa TFS Wilaya ya Magu, Ayoub Mikae alisema kuwa, kilichokuwa kinafanyika sio kusogeza vigingi bali na kuimarisha vigingi vilivyokuwepo ambapo utambuzi wake ulifanyika kitaalam kwa kutumia GPS. Aliongeza kuwa baadhi ya wananchi wasio waadilifu walidaiwa kusogeza vigingi vya mpaka wa Hifadhi hiyo ili wapate eneo la kulima jambo lililoleta taswira tofauti wakati wa kufanya marekebisho sahihi kwa kutumia mtambo wa GPS uliosaidia kubaini mpaka asilia.

Ayoub alisema kuwa sababu ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu Sayaka ilikuwa ni kuhifadhi uoto wa asili, kutunza vyanzo vya maji na kuhifadhi samaki wa Ziwa Victoria kwa kuwa mto uliopo katika hifadhi hiyo unapeleka maji Ziwa Victoria.

Baada ya kusikiliza hoja mbalimbali za wananchi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi hiyo katika mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Bugatu, Eng. Makani alisema kuwa tatizo kubwa aliloliona katika mgogoro huo ni changamoto za Uhifadhi ikiwemo uelewa hafifu wa baadhi ya wananchi juu ya umuhimu wa uhifadhi, ushirikishwaji hafifu wa wananchi kwenye uwekaji wa vigingi na baadhi ya wananchi kuchanganya vigingi vya hifadhi ya maji na hifadhi ya Msitu, changamoto ambazo alisema zitazingatiwa kwa kina wakati wa utatuzi wa mgogoro huo.

Alisema kuwa “Tunahitaji uhifadhi endelevu, peke yetu bila wananchi hatuwezi, tunahitaji uhifadhi rafiki, tukiwa na uelewa wa pamoja juu ya umuhimu wa uhifadhi na tukajibu kero zenu mtatusaidia kulinda na kuhifadhi Maliasili zetu”. 

Kwa upande wa Wananchi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo waliopewa fursa ya kuchangia na kuuliza maswali kwenye mkutano huo walipaza sauti zao kuiomba Serikali kupitia Naibu Waziri huyo kuwasaidia maeneo ya kufuga na kulima kutokana na ufinyu wa maeneo uliosababishwa na ongezeko kubwa la watu. Naibu Waziri Makani Aliahidi kwa niaba ya Serikali kupitiwa upya maeneo yoye ya Hifadhi nchini yenye migogoro na kuyatafutiwa suluhu ya kudumu kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya Serikali.

Wednesday, July 20, 2016

NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII, ENG. RAMO MAKANI ATAKA JAMII ZINAZOZUNGUKA MAENEO YA HIFADHI NCHINI ZISHIRIKISHWE KULINDA MALIASILI ZA TAIFA

 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa kwanza kulia) akizungumza na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, Massana Mwishawa (wa pili kulia) alipotembelea hifadhi hiyo tarehe 21 Julai, 2016 kwa ajili ya kujionea kero mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi. Kushoto aliyesimama na Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu kwa jina la Msukuma.
  Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, Massana Mwishawa (wa pili kulia) akimuonesha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa kwanza kulia) sehemu ya fukwe za hifadhi hiyo ambazo ni makazi ya Mamba na Ndege wa aina mbali mbali alipotembelea hifadhi hiyo tarehe 21 Julai, 2016 kwa ajili ya kujionea kero mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi. Kushoto aliyesimama na Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu kwa jina la Msukuma. 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa pili kulia) akiteta jambo na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mwl. Herman Kapufi (kulia) katika fukwe ya Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo alipotembelea hifadhi hiyo tarehe 21 Julai, 2016 kwa ajili ya kujionea kero mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi. Kushoto anaesaini kitabu cha wageni ni Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu kwa jina la Msukuma. 
Picha ya pamoja kati ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (katikati waliokaa), Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mwl. Herman Kapufi (wa tatu kushoto waliokaa), Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu kwa jina la Msukuma (wa tatu kulia waliokaa), Kaimu Mkurugenzi Mkuu TANAPA, Ibrahim Mussa (wa pili kushoto waliokaa) na baadhi ya Watumishi wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo hifadhini hapo tarehe 21 Julai, 2016
Mamba katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo.
 Moja ya Fukwe katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo.
 Huduma za malazi katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo.
Huduma bora ya vyumba inapatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo.
Huduma za usafiri wa boti zinapatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Rubondo.
____________________________________________________________

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani ameitaka Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuzishirikisha jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi hapa nchini kutambua umuhimu wa kuhifadhi maeneo hayo ili kutoa ulinzi shirikishi katika kupambana na Ujangili.

Eng. Makani amesema hayo jana wakati akizungumza na viongozi pamoja na watumishi wa Mamlaka hiyo akiwa ziarani Mkoani Geita katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo.

“Wananchi waoishi jirani na maeneo haya ya hifadhi ni muhimu wakaelimishwa juu ya faida za uhifadhi kiikolojia na kiuchumi kwenye maisha yao ambapo itawapa msukumo wa kuyatunza na kuyalinda” Alisema Eng. Makani.

Aliongeza kuwa vita dhidi ya Ujangili hapa nchini haiwezi kufanikiwa kirahisi iwapo jamii inayozunguka maeneo ya Hifadhi haitatoa ushirikiano kwa Serikali katika kulinda na kuhifadhi Maliasili zilizopo.

“Pamoja na mbinu nyingine, washirikisheni wananchi watusaidie kupambana na ujangili ili fedha ambayo ingetumiwa na Serikali kwa kazi hiyo itumike kuendeleza hifadhi zetu pamoja na kutoa huduma nyingine za kijamii” Alisema Eng. Makani.

Akizungumzia faida za uhifadhi kiuchumi hapa nchini alisema kuwa, Sekta ya utalii ndio sekta pekee inayoongoza kwa kuliingizia taifa mapato mengi ya nje (foreign currency) ambayo ni asilimia 25 ya mapato yote. Sekta hiyo pia inachangia pato la taifa kwa asilimia 17.2.

Eng. Makani aliongeza kuwa “Serikali ya awamu ya tano ina mpango wa kuboresha sekta ya utalii ili iweze kuiingizia zaidi mapato, katika kufanikisha hilo tumeweka mkakati wa kuboresha ofisi zetu za utalii za Kanda ili ziweze kutangaza na kukuza zaidi utalii wa ndani”.

Kwa upande wa hoteli zinazotoa huduma ya kitalii hapa nchini alisema kuwa ifikapo mwezi Septemba mwaka huu, Serikali itaanza rasmi zoezi la kuorodhesha hoteli zote zinazotoa huduma hiyo na kuzipanga kwenye makundi ya ubora ambapo zile zitakazoonekana hazina hadhi kabisa zitaondolewa katika mtandao wa kutoa huduma hiyo. Alisema zoezi hilo litaboresha huduma za kitalii nchini na kusaidia watalii kufikia hoteli wanazozihitaji na kupata huduma stahiki .

Katika kushirikisha sekta binafsi kwenye kukuza utalii nchini, amewaomba watoa huduma za ndege kuangalia upya viwango vya gharama zao za usafiri ili wananchi wengi zaidi waweze kumudu na kunufaika na huduma hiyo.

Wakati huo huo aliwaasa watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo kufanya kazi kwa bidii, kuwa na maadili mema na uadilifu kazini. Aliwataka pia kuwa mstari wa mbele kupiga vita ujangili, kuboresha ukusanyaji wa mapato na kushirikisha wananchi kwenye uhifadhi.

Hapo awali akiwasilisha taarifa ya hifadhi hiyo kwa Naibu Waziri wa Maliasili, Eng. Ramo Makani, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, Massana Mwishawa alisema kuwa changamoto kubwa inayoikabili hifadhi hiyo ni ujangili na upatikanaji mdogo wa mapato ambao hauwiani na mahitaji ya hifadhi hiyo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Luiza Kasheku maarufu kama Msukuma, alimuomba Naibu Waziri huyo wa Maliasili kuboresha Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo ambayo ipo Jimboni kwake iweze kupata mapato ya kutosha na kujiendesha yenyewe. Hifadhi hiyo kwa sasa inategemea mapato kutoka kwenye hifadhi nyingine kujiendesha.

Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo iliyopo Mkoani Geita ni moja ya sehemu pekee na muhimu katika uzalishaji wa mazalia ya samaki katika ziwa Victoria. Sehemu nyingine ni Hifadhi ya Kisiwa cha Saanane iliyopo Mkoani Mwanza. Hifadhi hizi zina umuhimu mkubwa katika upatikanaji wa samaki katika Ziwa Victoria.

Tuesday, July 19, 2016

WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHE. KASSIM MAJALIWA AZUNGUMZA NA WATUMISHI WA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, AAGIZA MAUZO YA VITALU VYA MASHAMBA YA MITI YAFANYIKE KWA NJIA YA MNADA

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Watumishi wa Wazara ya Maliasili na Utalii kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha LAPF, Kijitonyama jijini Dar es salaam Julai 18, 2016 .
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza katika mkutano huo.
 Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi akizungumza katika Mkutano huo.
 Baadhi ya Watumishi wa Wizar ya Maliasili na Utalii wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha LAPF, Kijitonyama jijini Dar es salaam Julai 18, 2016 .
Baadhi ya Waandishi wa Habari na Watumishi wa Wizara ya Maliasi na Utalii katika Mkutano huo.
Picha ya pamoja kati wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa (katikati waliokaa) na Viongozi pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
____________________________________

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kubadilisha mfumo wa uvunaji wa vitalu vya miti kwenye mashamba ya Serikali ili kuweka uwazi kwenye biashara hiyo na kuipatia zaidi Serikali mapato.

Mhe. Majaliwa alisema hayo jana kwenye Mkutano na Viongozi pamoja na Watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kisenga uliopo Kijitonayama Jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia mabadiliko hayo, Mhe. Majaliwa alisema kuwa utaratibu uliokuwa ukitumika hapo awali wa kuuza miti kwenye mashamba ya Serikali kwa njia ya vibali hauna tija kwakuwa umekuwa ukiikosesha Serikali mapato na kuwanufaisha wafanyabiashara wachache.

“Utaratibu wa sasa wa kutumia vibali unatuletea migongano ndani ya Wizara na kuikosesha Serikali mapato, hivyo ni lazima tuubadilishe” Aliongeza Majaliwa.

Aliuagiza Uongozi wa Wizara kufanya marekebisho kwenye utaratibu huo na kuweka utaratibu wa mnada ili kuweka uwazi zaidi na kuondoa manung’uniko kwenye biashara hiyo. “vibali visitishwe, mnada uanze  kama inavyofanyika kwenye mitiki” Alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Hivi karibuni Mhe. Majaliwa alisitisha utoaji wa vibali vya uvunaji wa miti kwenye mashamba matano yanayomilikiwa na Serikali kutokana na kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Majaliwa aliagiza mabadiliko ya haraka katika vizuizi vya ukaguzi wa Maliasili ambavyo amesema vimekuwa havina tija na kuagiza baadhi yake vifutwe kabisa. Miongoni vya vizuizi alivyoagiza vifutwe ni Kibaha Stendi, Kimanzichana na Mbagala, pia aliagiza kuimarishwa kwa kituo cha Vikindu, Kibiti na Vigwaza.

Mhe. Majaliwa aliwaagiza wataalamu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na Tamisemi kwa ajili ya kuweka mfumo mzuri wa kuhifadhi na kuvuna mazao ya misitu yaliyopo katika Halmashauri na kutenga Misitu ya Asili tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo kumekuwepo muingiliano katika kutekeleza majukumu hayo jambo linalopelekea uharibifu wa misitu. 

Hapo awali Mhe. Majaliwa alieleza lengo kuu la Mkutano huo kuwa ni katika utaratibu wake wa kawaida aliojiwekea wa kutembelea Wizara na kuzungumza na watumishi kwa ajili kukumbushana majukumu yao, kuangalia changamoto mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi. Aliwaasa watumishi wa Wizara ya Maliasili kuwa wazalendo, waadilifu, waaminifu na kuongeza uwajibikaji ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya kuwahudumia vizuri wananchi.

“Ninyi ni watu muhimu sana katika utoaji wa huduma kwa wananchi, tekelezeni majukumu yenu kwa uadilifu wa hali ya juu. Kamilisheni malengo yenu kulingana na mpangokazi wenu mliojiwekea” Alisema Mhe. Majaliwa.

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe alisisitiza watumishi wa Wizara hiyo kuhakikisha kuwa wanalinda misitu kule iliko na sio kusubiri katika vituo na kukamata rasilimali zake ambazo zimevunwa isivyo halali na kuzitoza faini, kinyume chake rasilimali hizo zilipiwe kihalali kabla ya kuvunwa. Aliahidi pia kuisuka upya Idara ya Misitu. 

Thursday, July 14, 2016

WAZIRI WA MALIASILI, PROF. JUMANNE MAGHEMBE AONANA NA BALOZI WA FINLAND HAPA NCHINI, PEKKA HUKKA

Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (katikati) akizungumza na Balozi wa Finland  hapa nchini, Pekka Hukka (kulia) alipotembelewa na Balozi huyo ofisini kwake, Mpingo House taerehe 12 Julai, 2016. Kushoto ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa TFS, Richard Kamwenda.
 Balozi wa Finland hapa nchini, Pekka Hukka (kulia), akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kulia) alipomtembelea ofisini kwake kujadili mambo mbalimbali yanayohusu Uhifadhi wa Maliasili na uendelezaji wa sekta ya Misitu nchini. Kushoto ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa TFS, Richard Kamwenda.