slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Thursday, October 27, 2016

TFS YANASA LORI LIKISAFIRISHA MBAO KINYUME CHA SHERIA, DEREVA ATOKOMEA KUSIKOJULIKANA

Kaimu Afisa Habari na Mawasiliano ambaye pia Ofisa Misitu Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Nurdin chamuya (Kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) Jijiji Dar es Salaam jana kuhusiana na kukamatwa kwa lori lenye namba za usajili T676 ANQ lililokuwa linasafirisha mbao kinyume cha sheria kutoka Mkoani Kigoma kuja Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Afisa wa Himasheria wa Wakala huyo, Arjason Mloge. 
Kaimu Afisa Habari na Mawasiliano ambaye pia Ofisa Misitu Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Nurdin chamuya (Kushoto) na Afisa wa Himasheria wa Wakala huyo, Arjason Mloge wakionesha sehemu ya mbao zilizokuwa zimefunikwa na katoni za sabuni ndani ya lori lenye namba za usajili T676 ANQ lililokuwa linasafirisha mbao hizo kinyume cha sheria kutoka Mkoani Kigoma kuja Jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa sehemu ya mbao hizo zikiwa zimefunikwa na sabuni ndani ya lori hilo.
Maofisa wa kikosi Dhidi ya Ujangili kanda ya Dar es Salaam na kikosi cha Kufuatilia na Kuzuia Uharibifu wa Misitu cha Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania wakitumia mbwa maalum wa kunusa (Sniffer Dog) kwa ajili ya kutambua bidhaa haramu ndani ya lori hilo.
Muonekano wa nje wa Lori hilo.
______________________________

Kikosi cha Kufuatilia na Kuzuia Uharibifu wa Misitu cha Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kwa kushirikiana na Kikosi Dhidi ya Ujangili kanda ya Dar es Salaam kimefanikiwa kukamata lori lenye namba za usajili T 676 ANQ lililokuwa likisafirisha mbao kinyume cha sheria huku zikiwa zimefichwa kwa kufunikwa na bidhaa mbalimbali ikiwemo sabuni ili zisionekane kiurahisi kwenye vituo vya ukaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo, Kaimu Afisa Habari wa Wakala huyo, Nurdin Chamuya alisema tukio hilo limetokea tarehe 14 Oktoba, 2016 majira ya saa kumi usiku maeneo ya Amana, Ilala Jijini Dar es Salaam baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema juu ya uwepo lori hilo katika maeneo hayo.

Chamuya alisema baada ya kupata taarifa hizo vikosi hivyo vilifika eneo la tukio na kufanya mahojiano na baadhi ya wananchi waliokuwa karibu na lori hilo ambapo mmoja kati ya wahudumu wa lori hilo alieleza kuwa lori hilo lilitokea Mkoani Kigoma na kwamba lilikuwa limepakia mzigo wa sabuni na chupa za maji zilizotumika. Dereva wa lori hilo hakuweza kupatikana.

“Wahudumu hao walipotakiwa kufungua mlango wa lori hilo kwa ajili ya upekuzi zaidi walisita kwa madai kuwa hawakuwa na funguo za lori hilo, Hatimaye   waliwasiliana na mmlikiwa wa eneo ambaye alikuwa amekabidhiwa funguo kwa ajili ya ulinzi” alisema Chamuya.

Alieleza kuwa mmiliki huyo alipofika alisema, anamfahamu mwenye gari ambaye ndiye mpangaji wa eneo lilipokutwa gari na kwamba anazo taarifa za  gari hilo,  na ameombwa apokee mzigo na kuutunza hadi atakaporudi kutoka safari ya  Mwanza kwa tatizo la msiba wa Baba yake.

Baada ya mmiliki wa eneo hilo kufanya mawasiliano na mwenye gari kuhusu mzigo uliokuwa kwenye gari hilo, mwenye gari alieleza kuwa kwa taarifa za dereva wake na ajenti aliyepakia mzigo Kigoma, gari lake lilikuwa na chupa chakavu na sabuni kutoka Kigoma na hakuna aina nyingine ya mzigo kwa ufahamu wake na akaruhusu gari hilo kufunguliwa mbele ya mwenye eneo.

“Baada ya gari hilo kufunguliwa, kilichoonekana kwa urahisi ni sabuni na mifuko michache inayosomeka kwa nje kuwa ni dawa ya kuku. Baada ya upekuzi ndipo zilionekana mbao zilizokuwa zimefichwa chini ya katoni za sabuni. Tumeshikilia Lori hilo kwa hatua zaidi za kisheria.

“Kufuatia tukio hili, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania tunatoa onyo kali kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo vya uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu kinyume cha sheria ya misitu namba 14 ya mwaka 2002 pamoja na kanuni zake za mwaka 2004 na kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria za nchi” alisema Chamuya.

Akizungumzia athari mbalimbali za vitendo hivyo vya uvunaji holela wa mazao ya misitu bila ya kufuata taratibu za kisheria za uvunaji endelevu alisema vitendo hivyo vinatishia nchi kuwa jangwa ambapo takwimu zinaonyesha jumla ya hekta 372,000 za misitu nchini hupotea kila mwaka kutokana na matumizi makubwa ya rasilimali hizo ambayo yanazidi uzalishaji wake kwa ujazo wa mita 19.5 milioni kwa mwaka.

Chamuya ametoa wito kwa wananchi wote nchini kushirikiana na Serikali katika uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za misitu na kuacha fikra potofu kuwa kazi hiyo ni ya Serikali pekee na taasisi zake kwakuwa faida zake hunufaisha jamii yote na vivyo hivyo kama athari zitajitokeza basi zitaikumba jamii yote bila kubagua.

Friday, October 21, 2016

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, PROF. JUMANNE MAGHEMBE AAHIDI KUFANYA MABADILIKO MAKUBWA CHUO CHA TAIFA CHA UTALII

Waziri wa Maliasili Na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe akizungumza na watumishi wa Chuo cha Taifa cha Utalii Kampasi ya Bustani pamoja na waandishi wa habari alipotembelea chuo hicho juzi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe (wanne kushoto) akikagua sehemu ya jiko katika chuo hicho.
Picha ya pamoja kati ya Waziri wa Maliasili Na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na viongozi pamoja na watumishi wa chuo hicho.
________________________________________

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, ameahidi kuibadili Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Taifa cha Utalii na kuifanya kuwa Bodi ya Utawala.

Alisema lengo la mabadiliko hayo ni kuhakikisha Chuo hicho kinatoa wataalamu wenye sifa na viwango vinavyostahiki kufanya kazi ndani na nje ya nchi.

Waziri Maghembe ametoa kauli hiyo juzi alipotembelea chuo hicho na kuangalia namna ya kukiboresha na kukifanya kiwe cha ushindani.


Aidha, Prof.Maghembe ameutaka uongozi wa chuo hicho kuondoa jina la Wakala ambalo limekuwa likitumika na chuo hicho badala yake kiitwe Chuo cha Taifa cha Utalii ili kionyeshe hadhi yake kitaifa na kimataifa huku akisisitizia suala la ubunifu katika uendeshaji na kuongeza mapato badala ya kulalamika kukabiliwa na changamoto nyingi ambazo chuo kingeweza kuzitatua.


Amekitaka chuo hicho kuwa cha mfano kwa kuwafundisha wanafunzi k maadili mema kwa kuwa wafanyakazi wengi wa mahoteli nchini wamelalamikiwa kuwa na sifa za udokozi hivyo kuwafanya watu wenye mahoteli kuajiri wafanyakazi kutoka nje ili kuepuka fedheha hiyo.


"Baadhi ya wahudumu katika hoteli zetu wamekuwa na tabia ya udokozi, hii ni sifa mbaya kwa wageni kwani huharibu taswira ya hoteli"


Aliutaka uongozi wa chuo hicho kuwa na mitaala yenye kutoa mafunzo ya kupika vyakula vya asili ili kuenzi utamaduni wa Mtanzania na kuendeleza utalii wa kiutamaduni.

Thursday, October 20, 2016

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI ENG. RAMO MAKANI ATETA NA WANANCHI WALIOVAMIA HIFADHI ZA MISITU MKOANI GEITA

Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani akizungumza na wananchi wa eneo la Mchangani waliovamia Hifadhi ya Msitu wa Biharamulo – Kahama uliopo Wilaya ya Chato Mkoani Geita alipotembelea kuona changamoto za uhifadhi. Asilimia 70 ya hifadhi hiyo kwa upande wa Wilaya ya Chato imeharibiwa kabisa na shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo, ufugaji na makazi ya kudumu, nyumba zinazoonekana pichani na sehemu ya makazi hayo.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani akionesha moja ya kigingi (beacon) cha mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa Biharamulo - Kahama uliopo Wilayani Chato Mkoa wa Geita ambao umevunjwa na wananchi waliovamia msitu huo kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo, ufugaji na makazi. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Gen. Mstaafu Ezekiel Kyunga na Mkuu wa Wilaya ya Chato, Shaaban Ntarambe (kulia).
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani akizungumza na wananchi wa eneo la Iponyanzege waliovamia Hifadhi ya Msitu wa Biharamulo – Kahama uliopo Wilaya ya Chato Mkoani Geita alipotembelea kuona changamoto za uhifadhi Mkoani humo. 
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Geita na Wilaya ya Chato katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo alipofanya ziara katika maeneo ya hifadhi yenye changamoto Mkoani humo kwa ajili ya kuyatafutia suluhu ya kudumu.
Hizi ni miongoni mwa athari za uvamizi wa wananchi hao katika Hifadhi ya Misitu wa Biharamulo - Kahama Wilayani Chato Mkoa wa Geita ambapo miti ya asili imekatwa kupisha shughuli za kilimo, ufugaji na makazi bila kujali athari za tabianchi. 

_______________________________________

Wananchi wanaozunguka hifadhi za misitu na wanyamapori nchini wametakiwa kutii sheria za uhifadhi na kujiepusha na vitendo viovu vya uharibifu wa mazingira vinavyopelekea kupotea kwa uoto wa asili na kutishia nchi kuwa jangwa ambapo pamoja na mambo mengine wametakiwa kuondoa mifugo yao katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria. 

Hayo yamesemwa juzi Mkoani Geita na Naibu Waziri, Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Mkoa huo Wilayani Chato kuhusu maelekezo ya kuwaondoa wananchi waliovamia maeneo hifadhi Mkoani humo na taifa kwa ujumla.

Alieleza kuwa vitendo hivyo vya uharibifu wa mazingira ni pamoja na ukataji wa miti hovyo, kilimo kisichoendelevu, uchungaji holela wa mifugo, uanzishaji makazi na shughuli zingine za kibinadamu katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria ikiwemo Hifadhi za Misitu, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Hifadhi za Taifa.

"kwa sasa Tanzania inapoteza takriban hekta 372,000 za uoto wa asili kila mwaka na endapo hali hiyo ikiachwa iendelee tishio la kutoweka kwa uoto huo ni kubwa zaidi. Takwimu pia zinaonyesha kuwa Tanzania ina eneo la uoto wa asili lenye ukubwa wa takriban Hekta milioni 48.1 na kwamba kasi hiyo ikiachwa iendelee itaiacha Tanzania bila uoto wa asili baada ya miaka 129" alisema Makani.

Akizungumzia taratibu za kuwaondoa wananchi katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria alisema watumishi na viongozi wote wa Serikali wanaotekeleza zoezi hilo wanatakiwa kufuata sheria na miongozo iliyowekwa ikiwa ni pamoja na kujiepusha na vitendo viovu vinavyoweza kuichafua Serikali ikiwemo rushwa na unyanyasaji wa wananchi, "watakaobainika kwenda kinyume na utaratibu huo watachukuliwa hatua za kisheria" alisema.

Katika utekelezaji na usimamizi wa sheria hizo za uhifadhi, aliwataka watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kusimamia sheria hizo kila siku na kuendesha utekelezaji wake kwa kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama za Wilaya na Mikoa ili kuimarisha utekelezaji wa sheria hizo na kuweka uwazi katika utendaji.

Kwa upande wa wananchi ambao wapo katika vijiji na vitongoji vilivyosajiliwa kisheria aliwataka kutoanzisha au kuendeleza shughuli mpya za kibinadamu hususani zinazosababisha uharibifu wa mazingira ikiwemo kuathiri mabadiliko ya tabia nchi mpaka pale kikosi kazi cha kitaifa kitakapokamilisha kazi yake na kuishauri Serikali namna bora ya kumaliza migogoro ya ardhi nchini.

Maagizo hayo yamekuja ikiwa ni siku chache kabla ya kikosi kazi hicho ambacho kimeundwa na Serikali kikiwa na wajumbe kutoka Wizara sita zinazohusika moja kwa moja na changamoto mbalimbali za ardhi kwa madhumuni ya kufanya uchunguzi wa kina ikiwemo kupitia sheria zote zinazohusika kabla ya kuishauri serikali namna bora ya kumaliza migogoro ya ardhi ikiwemo kwenye maeneo ya hifadhi.

Makani alizitaja wizara hizo kuwa ni Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maliasili na Utalii, TAMISEMI na Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambazo ndizo zimeanza utekelezaji wa zoezi hilo linalotarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu. Alisema Wizara nyingine mbili zitaungana baadae kukamilisha zoezi hilo ambazo ni Maji na Umwagiliaji na Nishati na Madini.

Hata hivyo alitoa tahadhari kwa wananchi juu ya uelewa wa tamko hilo ambapo alisema "Haitarajiwi kwamba Wananchi wengine watatumia vibaya tamko hili na kuanza kuingia katika maeneo ya hifadhi kwa shughuli zozote zile za kibinaadamu kwa kuwa vitendo hivyo havihusiani na tamko hilo na hatua kali zitachukuliwa mara moja dhidi ya wale watakaodiriki kwenda kinyume".

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Gen. Mstaafu Ezekiel Kyunga alisema Mkoa wake unakabiliwa na uhaba wa ardhi uliosababishwa na ongezeko kubwa la watu waliovutiwa na shughuli za kiuchumi Mkoani humo ikiwemo uchimbaji wa madini, uvuvi, ufugaji pamoja na kilimo ambazo kwa namna moja ama nyingine imekuwa ni changamoto kubwa katika uhifadhi Mkoani humo. Alieleza changamoto nyingine kuwa ni mitazamo tofauti ya baadhi ya wanasiasa kuhusu uhifadhi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chato, Shaaban Ntarambe alisema kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa misitu Wilayani humo ambapo Hifadhi ya Msitu wa Biharamulo - Kahama kwa upande wa Wilaya yake umeharibiwa kwa asilimia 70 kutokana na shughuli za kilimo, ufugaji, uchimbaji madini na makazi ya kudumu hali inayohatarisha kutoweka kwa hifadhi hiyo.

Msitu wa Biharamulo - Kahama una ukubwa wa hekta 134,684 na upo katika Wilaya tatu za Chato, Bukombe na Biharamulo. Kwa upande wa Wilaya ya Chato ambapo uharibifu  huo umefanyika kwa asilimia 70 una ukubwa wa hekta 30,000.

Wednesday, October 12, 2016

SERIKALI YATOA UFAFANUZI KUHUSU UONDOAJI WA WANANCHI KATIKA MAENEO YALIYOHIFADHIWA

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) hivi karibuni Makao Makuu wa Wizara hiyo Mpingo House juu ya ufafanuzi wa kuwaondoa wananchi katika maeneo yaliyohifadhiwa. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Angelina Madete na Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa TFS, Mohammed Kilongo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) Makao Makuu wa Wizara hiyo  Mpingo House hivi karibuni juu ya ufafanuzi wa kuwaondoa wananchi katika maeneo yaliyohifadhiwa. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara Wanyamapori, Prof. Alexander  Songorwa.
_____________________________

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maliasili na Utalii

TAARIFA KWA UMMA

UFAFANUZI KUHUSU UONDOAJI WANANCHI KATIKA MAENEO YALIYOHIFADHIWA

Serikali inawakumbusha wananchi wote na kusisitiza kwamba ni wajibu wao kutii sheria na kuepuka kabisa vitendo viovu vinavyosababisha kupotea kwa uoto wa asili kwa kasi inayoendelea hivi sasa nchini na kutishia UHIFADHI ENDELEVU,  hali hii inapelekea nchi kuwa Jangwa kutokana na ukataji wa miti hovyo, kilimo kisichoendelevu, uchungaji holela wa mifugo, uanzishaji makazi na shughuli zingine za kibinadamu katika maeneo yaliyohifadhiwa ikiwa ni pamoja na Hifadhi za Misitu, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na  Hifadhi za Taifa.

Ikumbukwe kwamba takwimu zinaonyesha kuwa kwa sasa Tanzania inapoteza takriban hekta 372,000 za uoto wa asili kila mwaka na kwamba kasi hiyo ikiachwa iendelee tishio la kutoweka kwa uoto huo ni kubwa sana. Takwimu pia zinaonyesha kuwa Tanzania ina eneo la uoto wa asili lenye ukubwa wa takriban Hekta milioni 48.1 na kwamba kasi iliyopo ya uharibifu ikiachwa iendelee itaiacha Tanzania bila uoto wa asili baada ya miaka 129.

Takwimu hizi zitabakia hivyo ikiwa idadi ya watu haitaongezeka, ukuaji wa shughuli za kibinadamu hautaongezeka na aina ya shughuli hizo haitabadilika, jambo ambalo haliwezekani. Hivyo basi upo uwezekano wa idadi ya miaka hiyo kupungua hata kufikia nusu, sawa na umri wa kawaida kabisa wa binadamu.

Kutokana na kuzingatia tishio hilo na umuhimu wa uhifadhi katika Taifa kiuchumi, kijamii na kiikolojia, serikali ilitunga sera, sheria, kanuni na Taratibu kwa madhumuni hayo. Sheria hizo ni pamoja na :

·        Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori, Na. 5 ya mwaka 2009
·        Sheria ya Misitu, Na. 14 ya mwaka 2002
·        Sheria ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Sura 284, R.E 2002
·        Sheria ya Hifadhi za Taifa, Sura 282, R.E 2002

Kumekuwa na mazoezi yanayoendelea nchini yanayohusu utekelezaji wa sheria hizo ambapo Wakala wa Misitu Tanzania, Taasisi za hifadhi za Wanyamapori n.k zimekuwa zikiendesha mazoezi kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mikoa mbalimbali.

Kufuatia uzoefu katika utekelezaji wa sheria hizi na maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi na wadau wengine, Serikali imekuwa ikitoa miongozo mbalimbali katika mazingira tofauti na nyakati tofauti kwa kuzingatia sheria husika na kwa kuzingatia, pamoja na mambo mengine:

·        Ongezeko la idadi ya watu na milki zao zinazotokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii, dhidi ya ukubwa na ubora wa maeneo yaliyohifadhiwa yanayowazunguka, ikiwa ni pamoja na misitu, mapori ya akiba, mapori tengefu, hifadhi za taifa, njia za mapito ya Wanyamapori (wildlife corridors) na Maeneo ya mtawanyiko wa Wanyamapori (Wildlife dispersal areas) yaliyohifadhiwa kwa miaka mingi.

·        Uvamizi wa maeneo na kuendesha shughuli za kibinadamu kama vile kulima, kuchunga mifugo, kujenga makazi, kuchimba madini, kukata miti hovyo na uvunaji mwingine wa maliasili usiozingatia sheria

·      Kupungua hadhi kwa baadhi ya maeneo yaliyohifadhiwa hata kufikia viwango vya kupoteza sifa zilizosababisha maeneo hayo kuhifadhiwa na hivyo kulisababishia Taifa hasara kubwa kiuchumi, kiikolojia na kijamii

·       Haja ya kuboresha taarifa zinazoendana na wakati na uwiano sahihi kati ya ukubwa na ubora wa ardhi iliyopo katika maeneo na mahitaji halisi ya ardhi (yakiwemo maeneo yaliyohifadhiwa) na mipango ya matumizi bora ya ardhi.

·       Haja ya kuboresha njia za usimamizi na utekelezaji wa hatua mbalimbali za kisheria kwa kuzingatia zaidi sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali kwa namna endelevu.

Kwa Taarifa hii, ambayo inatolewa na Wizara ikitekeleza maagizo ya mamlaka za juu za Serikali, inaagizwa kama ifuatavyo:

Kama ilivyoahidi Bungeni na kama ilivyokwishatoa maelezo katika nyakati tofauti, serikali imekwishaunda kikosi kazi chenye wajumbe kutoka Wizara sita zinazohusika moja kwa moja na changamoto mbalimbali za ardhi, kwa madhumuni mapana ya kufanya uchunguzi wa kina na kupitia sheria zote zinazohusika kabla ya kuishauri serikali kuhusu namna bora zaidi na endelevu ya kumaliza migogoro ya ardhi ikiwemo inayohusisha maeneo yaliyohifadhiwa. Kikosi kazi hicho kinatarajiwa kukamilisha kazi yake hivi karibuni.

Katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu na endelevu wa migogoro ya ardhi:

·         Viongozi na Watumishi wanaohusika wasiwabughudhi wananchi na badala yake wazingatie taratibu katika kutekeleza sheria wakati wa kushughulikia ukiukwaji wa sheria kwa wananchi walioko katika vitongoji na vijiji vilivyosajiliwa.

·   Wananchi walioko katika maeneo hayo wasianzishe shughuli mpya za kibinadamu na wasiendelee na shughuli za kibinaadamu zinazosababisha uharibifu wa mazingira na kuathiri tabia nchi

·    Mifugo yote iliyoko ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa kisheria iondolewe haraka kwa kuzingatia taratibu

·    Haitarajiwi kwamba Wananchi wengine watatumia vibaya tamko hili na kuanza kuingia katika maeneo ya hifadhi kwa shughuli zozote zile za kibinaadamu kwa kuwa vitendo hivyo havihusiani na tamko hili na hatua kali zitachukuliwa mara moja dhidi ya wale watakaodiriki kwenda kinyume.

Serikali inatarajia kuendelea kupata ushirikiano kutoka kwa wadau wote wa uhifadhi na wananchi kwa ujumla katika kutekeleza azma yake ya kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi duniani zinazoendana na Malengo ya Dunia (Umoja wa Mataifa), ya Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goals) kupitia uhifadhi endelevu wa maliasili zake.

Wakati Serikali inaendelea kutoa Elimu kwa njia mbalimbali na kufanya uhamasishaji, Wananchi wanatarajiwa pia kujenga na kuimarisha uelewa, utayari na kushiriki katika jitihada hizo za Serikali.


Imetolewa na;

Mhandisi Ramo Makani
Naibu Waziri, Wizara ya Maliasili na Utalii

13 Oktoba, 2016

Monday, October 10, 2016

UMUHIMU WA HIFADHI YA MAZINGIRA ASILIA AMANI, KIVUTIO CHA UTALII NA CHANZO MUHIMU CHA MAJI YANAYOTUMIKA JIJINI TANGA

 Geti la kuingilia katika Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani iliyopo katika Wilaya ya Muheza na Korogwe Mkoani Tanga.
Kinyonga aina ya pembe tatu (three hornes chameleon) ambao hupatikana katika hifadhi ya Mazingira Asilia Amani tu.
 Moja ya vyura aina ya Usumbara (Leptopelis vermiculatus) ambao wanaopatikana katika Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani pekee.
Sehemu ya maporomoko ya maji katika hifadhi ya Msitu wa asili ya amani iliyopo Wilayani Muheza Mkoani Tanga ambayo imekuwa kivutio kwa watalii wanaotembelea eneo hilo.

Moja ya vyanzo vya maji katika Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani.

Moja ya aina ya vipepeo "Colourful moth (Utetheisa pulchella)"  wanaopatikana katika Hifadhi ya Mazingira Amani pekee.

Kituo cha Taarifa katika Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani. Nyumba hii ilitumika na Kingozi wa Kituo cha Treni cha Mjerumani miaka 1904.

_______________Na Hamza Temba - WMU_____________

Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani ndiyo hifadhi kongwe kuliko hifadhi asilia zote nchini, Hifadhi hii ilitangazwa rasmi kwenye gazeti la Serikali mwaka 1997. Hifadhi hii ipo katika Wilaya za Muheza na Korogwe umbali wa kilomita 64 kutoka Jijini Tanga.

 

Amani yenye ukubwa wa hekta 8,380 ni moja kati ya maeneo ya mfano yaliyohifadhiwa vizuri nchini kwa kutumia mfumo wa Uhifadhi Shirikishi baina ya Serikali na wananchi wanaoishi na kuzunguka katika hifadhi hiyo.

 

Akizungumza na Jarida hili, Afisa Misitu Mkuu wa Hifadhi hiyo, Angyelile Sousa alisema, Serikali kupitia Wakala wake wa Huduma za Misitu (TFS) imewekeana Makubaliano ya kuhifadhi Msitu huo na vijiji 21 vinavyozunguka hifadhi hiyo. Vijiji vinne kati ya hivyo ambavyo ni Shebomeza, Mlesa, Chemka na Mikwinini vimo ndani ya Hifadhi hiyo Asilia.

 

Sousa alisema katika mfumo huo kila kijiji kimeunda kamati ya uhifadhi wa mazingira ambazo zinashirikiana kwa karibu na uongozi wa hifadhi hiyo kwenye shughuli za uhifadhi ikiwemo ulinzi wa rasilimali zilizomo.

 

Alisema kuwa makubaliano hayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa na manufaa makubwa kwa kuwa wananchi wa vijiji hivyo wameelimishwa na kuuelewa umuhimu wa hifadhi hiyo ambayo ina faida kubwa kwao, kwa Serikali na kwa wananchi wote wa Mkoa wa Tanga.

 

Aliongeza kuwa mfumo huo umesaidia kuimarisha uhifadhi katika Msitu huo ambapo matukio ya moto yamedhibitiwa kwa kiasi kikubwa ikiwa na pamoja na shughuli za uharibifu wa mazingira kwa ujumla.

 

Akielezea faida za hifadhi hiyo alisema, Amani ni chanzo kikuu cha Maji yanayotumika katika Jiji la Tanga ambapo vyanzo vyake vinapeleka maji katika mto Zigi unaopeleka maji hayo Jijini humo. Vijiji vyote 21 vinavyozunguka hifadhi hiyo pia vinanufaika na maji hayo.

 

Alisema kuwa faida nyingine inayopatikana katika hifadhi hiyo ikiwa ni sehemu ya makubaliano kwenye uhifadhi shirikishi ni mchango wa asilimia 20 ya mapato yanayotokana na utalii ambayo yanatolewa kwa vijiji 21 vinavyopakana na hifadhi hiyo kwa ajili ya kusaidia katika shughuli za maendeleo za vijiji hivyo.

 

“Katika sehemu ya makubaliano hayo wananchi wa vijiji jirani wanaruhusiwa kuokota kuni kavu zinazopatikana katika hifadhi hiyo, matunda, mbogamboga pamoja na dawa za miti shamba. Wananchi hao wanaruhusiwa kuingia hifadhini kwa umbali wa mita 100 kutoka maeneo yao ya vijiji kwa ajili ya shughuli hizo” alisema Sousa.

 

Aliongeza kuwa watu binafsi pia wananufaika na hifadhi hiyo kwa kuwekeza katika mahoteli yanayowapatia kipato. Wananchi pia wanaotembeza watalii katika hifadhi hiyo wananufaika na ajira ambapo huchukua asilimia 60 ya mapato ya kutembeza watalii (Tour Guiding Fees), asilimia 20 ikibaki hifadhini na asilimia 20 nyingine ikienda kwenye vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo.

 

Akizungumzia vivutio mbalimbali vilivyomo katika hifadhi hiyo, Sousa alisema kuna vivutio vingi vya utalii vilivyohifadhiwa vizuri ikiwemo Misitu ya Asili na Wanyama mbalimbali kama vile Kima wa Bluu (Blue Monkey), Mbega Weupe na Weusi (Black and White Collabus), Nyoka, vinyonga pembe tatu (Three Hornes Chamelleon), vipepeo na ndege wa aina mbali mbali ambao baadhi yao husafiri umbali mrefu kutoka barani ulaya kwa ajili ya kukimbia baridi kali na kuzaliana katika hifadhi hiyo.

 

“Vivutio vingine vilivyopo katika hifadhi hii ni Maporomoko ya Maji (Water Falls) ambayo ni Derema, Chemka, Ndola na Pacha. Pia kuna vivutio vya Vilele vya Milima (viewpoints) kama Kiganga, Ngua, Makanya, Mbomole na Kilimahewa. Ukiwa katika vilele hivyo unaweza kuona Mji wa Korogwe na Jiji la Tanga kwa juu” alisema.

 

Mbali na vivutio hivyo, alisema kivutio kingine ambacho ni cha kipekee katika hifadhi hiyo ni aina ya Ua linaloitwa “Saintpaulia” ambalo lina rangi ya Zambarau “Violeth Color”, Ua hilo pia linatumika kama nembo ya hifadhi hiyo. Upekee wa Ua hilo ni kwamba likipandwa sehemu nyingine yeyote duniani hubadilika rangi yake ya asili, Tafiti mbalimbali zimefanywa ikiwemo kujaribiwa kupandwa nchini Ujerumani na kutoa majibu hayo hayo.

 

Pamoja na vivutio hivyo kivutio kingine katika hifadhi hiyo ni mashine ya kusagia unga iliyokuwa ikitumia nishati ya nguvu ya kusukumwa na maji miaka 1986 katika kijiji cha Kisiwani na mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia nishati hiyo hiyo iliyotumiwa na Wakoloni wa Kijerumani katika Kijiji cha Chemka.

 

Akizungumzia aina za utalii katika hifadhi hiyo alisema, upo Utalii wa Picha (Photography), Utalii wa Kutizama Ndege (Bird Watching), Utalii wa Kuangalia viumbe hai Usiku (Night Watching), Utalii wa Kiutafiti (Reseach Tourism), Utalii wa kiutamaduni (Cultural Tourism) na Utalii wa Kutembea na Kupanda Milima.

 

“Kwa upande wa gharama za kutembelea hifadhi ya Amani kama kiingilio kwa Mtalii mmoja kutoka nje ya nchi ni Dola 10 za Kimarekani na Mtanzania ni Shilingi10,000. Kwa upande wa gharama za watembeza watalii wa nje ni dola 15 za Kimarekani” alisema.

 

Nae Afisa Misitu wa Hifadhi hiyo, Isack Bob Matunda akizungumzia idadi ya watalii waliotembelea hifadhi hiyo na mapato yaliyopatikana alisema “Mwaka wa fedha 2015/16 jumla ya watalii 545 walitembelea hifadhi hii na jumla ya mapato yote yaliyopatikana ni shilingi milioni 50. Aidha, mwaka huu wa fedha 2016/17 mwezi Julai-Agosti jumla ya watalii 121 wameshatembelea hifadhi hii na mapato ambayo yameshapatikana ni shilingi milioni 7.3”.

 

Akielezea changamoto za uhifadhi, Afisa Misitu Mkuu wa Hifadhi hiyo, Angyelile Sousa alisema zipo changamoto kidogo ikiwemo uchimbaji wa madini kwenye vyanzo vya maji, uharibifu mdogo wa misitu ikiwa ni pamoja na uchomaji moto katika ukanda wa chini na miundombinu mibovu ya barabara.

Tuesday, October 4, 2016

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI, ENG. RAMO MAKANI AONGOZA MAADHIMISHO YA SIKU YA KUTUNDIKA MIZINGA KITAIFA MKOANI PWANI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani akizungumza na wananchi katika viwanja vya Mwambisi Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani jana wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kutundika Mizinga Kitaifa Mkoani humo. Naibu Waziri Makani ametoa wito kwa wananchi kutumia vizuri fursa ya maeneo ya misitu yaliyotengwa kwa shughuli za ufugaji nyuki kwenye ukanda wa wazi (buffer zone) kwa kutundika mizinga mingi na siyo kutumia maeneo hayo kwa shughuli nyingine za uharibifu wa mazingira kama uchomaji mkaa kwa kuwa kufanya hivyo kutasadia uhifadhi wa misitu na kuongeza uzalishaji bora wa mazao ya nyuki. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Dkt. Ezekiel Mwakalukwa, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu, Prof. Dos Santos Silayo (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Asumpta Mshana (wa pili kushoto).
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (katikati) akizindua Manzuki ya Makonga katika shamba la Miti Ruvu Kaskazini Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani jana wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kutundika Mizinga Kitaifa yaliyofanyika Wilayani humo. Manzuki hiyo itatumiwa kama shamba darasa la kuwaelimisha wananchi juu ya ufugaji wa nyuki kwa njia za kisasa zitakazowezesha kuzalisha mazao bora ya nyuki. Kulia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Asumpta Mshana (wa pili kushoto) na Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Daniel Isala (kushoto).
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kulia) akitundika mzinga wa nyuki katika shamba la Miti Ruvu Kaskazini Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani jana wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kutundika Mizinga Kitaifa Wilayani humo. Kushoto anaeshiriki nae ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Asumpta Mshana na kushoto kwa Mkuu wa Wilaya ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Asumpta Mshana (kushoto) wakifunga mzinga wa nyuki baada ya kuutundika mapema jana katika shamba la miti Ruvu Kaskazini Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani.
 Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo (kulia) akitundika mzinga katika shamba la miti Mwakonga 2 Wilayani Kibaha jana. Prof. Silayo alisema kuwa kwa sasa Ofisi yake inasimamia jumla ya manzuki 92 zenye mizinga 7,129 ambazo zipo katika kanda 7 na mashamba ya miti manne. Aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2015/2016 jula ya mizinga 2,706 ilivunwa na kupata asali kilo 7,129 za asali na kilo 195 za nta. Katika salamu zake Prof. Dos Santos alisema kuwa Asali ya Tanzania imepimwa katika maabara nchini ujerumani na kugundulika kuwa ni asali bora isiyo na kemikali na pia nyuki wa Tanzania hawana magonjwa hivyo asali yake ni salama. Alitoa wito kwa wananchi kutumia fursa zilizopo kufuga nyuki kwa wingi ili kujiinua kiuchumi na kuendeleza uhifadhi wa mazingira nchini.
 Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo (kulia) akifunga mzinga huo baada ya kuutundika huku  akisaidiwa na moja ya mfanyakazi wa taasisi hiyo.
Naibu Waziri wa Maliasili, Eng. Ramo Makani (wa pili kushoto) akikagua miche ya miti katika shamba la miti Ruvu Kaskazini Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani jana wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kutundika Mizinga Kitaifa yaliyofanyika Mkoani humo. Shamba hilo lina jumla viriba vya miti milioni moja kwa ajili ya kupandwa katika shamba hilo na maeneo mengine nchini. Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Asumpta Mshana, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo (wa tatu kulia) na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki, Dkt. Ezekiel Mwakalukwa (kushoto).
 Naibu Waziri Makani akiangalia moja ya mche wa mti unaoota katika kitalu hicho.
Naibu Waziri wa Maliasili, Eng. Ramo Makani (wa tatu kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Grace Procucts Ltd inayojishuulisha na utengenezaji wa vipodozi vilivyochanganywa na asali, Dkt. Elizabeth Kilili jana wakati akaikagua mabanda ya maonesho kwenye viwanja vya Mwambisi Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani katika Maadhimisho ya Siku ya Kutundika Mizinga Kitaifa yaliyofanyika Mkoani humo. Wapili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Asumpta Mshana.
Picha ya pamoja kati ya Naibu Waziri wa Maliasili, Eng. Ramo Makani (wa tatu mstari wa nyuma), Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Asumpta Mshana (wa nne mstari wa nyuma), Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Daniel Isala (wa pili kulia), Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Dkt. Ezekiel Mwakalukwa (kulia), Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo (kushoto) na Vijana wa "Skauti"  baada ya kuwakabidhi zawadi za asali (mstari wa mbele) muda mfupi baada ya kufunga maadhimisho hayo katika uwanja wa Mwambisi Wilayani Kibaha Mkoa wa Pawani jana.
Naibu Waziri Makani akimkabidhi zawadi ya asali mmoja ya vijana hao wa Skauti.