Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani akizungumza na wananchi wa eneo la Mchangani waliovamia Hifadhi ya Msitu wa Biharamulo – Kahama uliopo Wilaya ya Chato Mkoani Geita alipotembelea kuona changamoto za uhifadhi. Asilimia 70 ya hifadhi hiyo kwa upande wa Wilaya ya Chato imeharibiwa kabisa na shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo, ufugaji na makazi ya kudumu, nyumba zinazoonekana pichani na sehemu ya makazi hayo.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani akionesha moja ya kigingi (beacon) cha mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa Biharamulo - Kahama uliopo Wilayani Chato Mkoa wa Geita ambao umevunjwa na wananchi waliovamia msitu huo kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo, ufugaji na makazi. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Gen. Mstaafu Ezekiel Kyunga na Mkuu wa Wilaya ya Chato, Shaaban Ntarambe (kulia).
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani akizungumza na wananchi wa eneo la Iponyanzege waliovamia Hifadhi ya Msitu wa Biharamulo – Kahama uliopo Wilaya ya Chato Mkoani Geita alipotembelea kuona changamoto za uhifadhi Mkoani humo.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Geita na Wilaya ya Chato katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo alipofanya ziara katika maeneo ya hifadhi yenye changamoto Mkoani humo kwa ajili ya kuyatafutia suluhu ya kudumu.
Hizi ni miongoni mwa athari za uvamizi wa wananchi hao katika Hifadhi ya Misitu wa Biharamulo - Kahama Wilayani Chato Mkoa wa Geita ambapo miti ya asili imekatwa kupisha shughuli za kilimo, ufugaji na makazi bila kujali athari za tabianchi.
_______________________________________
Wananchi wanaozunguka hifadhi za misitu na wanyamapori nchini
wametakiwa kutii sheria za uhifadhi na kujiepusha na vitendo viovu vya
uharibifu wa mazingira vinavyopelekea kupotea kwa uoto wa asili na kutishia
nchi kuwa jangwa ambapo pamoja na mambo mengine wametakiwa kuondoa mifugo yao
katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria.
Hayo
yamesemwa juzi Mkoani Geita na Naibu Waziri, Wizara ya Maliasili na Utalii,
Mhandisi Ramo Makani wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Mkoa huo
Wilayani Chato kuhusu maelekezo ya kuwaondoa wananchi waliovamia maeneo hifadhi
Mkoani humo na taifa kwa ujumla.
Alieleza kuwa vitendo hivyo vya uharibifu wa mazingira ni pamoja na ukataji wa miti
hovyo, kilimo kisichoendelevu, uchungaji holela wa mifugo, uanzishaji makazi na
shughuli zingine za kibinadamu katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria ikiwemo
Hifadhi za Misitu, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Hifadhi za Taifa.
"kwa
sasa Tanzania inapoteza takriban hekta 372,000 za uoto wa asili kila mwaka na endapo
hali hiyo ikiachwa iendelee tishio la kutoweka kwa uoto huo ni kubwa zaidi.
Takwimu pia zinaonyesha kuwa Tanzania ina eneo la uoto wa asili lenye ukubwa wa
takriban Hekta milioni 48.1 na kwamba kasi hiyo ikiachwa iendelee itaiacha
Tanzania bila uoto wa asili baada ya miaka 129" alisema Makani.
Akizungumzia
taratibu za kuwaondoa wananchi katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria alisema
watumishi na viongozi wote wa Serikali wanaotekeleza zoezi hilo wanatakiwa kufuata
sheria na miongozo iliyowekwa ikiwa ni pamoja na kujiepusha na vitendo viovu
vinavyoweza kuichafua Serikali ikiwemo rushwa na unyanyasaji wa wananchi, "watakaobainika
kwenda kinyume na utaratibu huo watachukuliwa hatua za kisheria" alisema.
Katika
utekelezaji na usimamizi wa sheria hizo za uhifadhi, aliwataka watumishi wa Wizara
ya Maliasili na Utalii kusimamia sheria hizo kila siku na kuendesha utekelezaji
wake kwa kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama za Wilaya na Mikoa ili kuimarisha
utekelezaji wa sheria hizo na kuweka uwazi katika utendaji.
Maagizo
hayo yamekuja ikiwa ni siku chache kabla ya kikosi kazi hicho ambacho kimeundwa na Serikali kikiwa na wajumbe kutoka Wizara sita zinazohusika moja
kwa moja na changamoto mbalimbali za ardhi kwa madhumuni ya kufanya uchunguzi
wa kina ikiwemo kupitia sheria zote zinazohusika kabla ya kuishauri serikali
namna bora ya kumaliza migogoro ya ardhi ikiwemo kwenye maeneo ya hifadhi.
Makani
alizitaja wizara hizo kuwa ni Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maliasili
na Utalii, TAMISEMI na Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambazo ndizo zimeanza utekelezaji
wa zoezi hilo linalotarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu. Alisema Wizara
nyingine mbili zitaungana baadae kukamilisha zoezi hilo ambazo ni Maji na
Umwagiliaji na Nishati na Madini.
Hata
hivyo alitoa tahadhari kwa wananchi juu ya uelewa wa tamko hilo ambapo alisema "Haitarajiwi
kwamba Wananchi wengine watatumia vibaya tamko hili na kuanza kuingia katika
maeneo ya hifadhi kwa shughuli zozote zile za kibinaadamu kwa kuwa vitendo
hivyo havihusiani na tamko hilo na hatua kali zitachukuliwa mara moja dhidi ya
wale watakaodiriki kwenda kinyume".
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Gen. Mstaafu Ezekiel Kyunga alisema
Mkoa wake unakabiliwa na uhaba wa ardhi uliosababishwa na ongezeko kubwa la
watu waliovutiwa na shughuli za kiuchumi Mkoani humo ikiwemo uchimbaji wa madini, uvuvi, ufugaji pamoja na
kilimo ambazo kwa namna moja ama nyingine imekuwa ni changamoto kubwa katika
uhifadhi Mkoani humo. Alieleza changamoto nyingine kuwa ni mitazamo tofauti ya baadhi ya wanasiasa kuhusu uhifadhi.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Shaaban Ntarambe alisema kumekuwepo na uharibifu mkubwa
wa misitu Wilayani humo ambapo Hifadhi ya Msitu wa Biharamulo - Kahama kwa upande wa Wilaya yake umeharibiwa
kwa asilimia 70 kutokana na shughuli za kilimo, ufugaji, uchimbaji madini na
makazi ya kudumu hali inayohatarisha kutoweka kwa hifadhi hiyo.
Msitu wa Biharamulo - Kahama una ukubwa wa hekta 134,684 na upo katika Wilaya tatu za Chato, Bukombe na Biharamulo. Kwa upande wa Wilaya ya Chato ambapo uharibifu huo umefanyika kwa asilimia 70 una ukubwa wa hekta 30,000.
No comments:
Post a Comment