Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) hivi karibuni Makao Makuu wa Wizara hiyo Mpingo House juu ya ufafanuzi wa kuwaondoa wananchi katika maeneo yaliyohifadhiwa. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Angelina Madete na Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa TFS, Mohammed Kilongo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) Makao Makuu wa Wizara hiyo Mpingo House hivi karibuni juu ya ufafanuzi wa kuwaondoa wananchi katika maeneo yaliyohifadhiwa. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara Wanyamapori, Prof. Alexander Songorwa.
_____________________________
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maliasili na Utalii
TAARIFA KWA UMMA
UFAFANUZI
KUHUSU UONDOAJI WANANCHI KATIKA MAENEO YALIYOHIFADHIWA
Serikali
inawakumbusha wananchi wote na kusisitiza kwamba ni wajibu wao kutii sheria na
kuepuka kabisa vitendo viovu vinavyosababisha kupotea kwa uoto wa asili kwa
kasi inayoendelea hivi sasa nchini na kutishia UHIFADHI ENDELEVU, hali hii inapelekea nchi kuwa Jangwa kutokana
na ukataji wa miti hovyo, kilimo kisichoendelevu, uchungaji holela wa mifugo, uanzishaji
makazi na shughuli zingine za kibinadamu katika maeneo yaliyohifadhiwa ikiwa ni
pamoja na Hifadhi za Misitu, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Hifadhi za Taifa.
Ikumbukwe kwamba
takwimu zinaonyesha kuwa kwa sasa Tanzania inapoteza takriban hekta 372,000 za
uoto wa asili kila mwaka na kwamba kasi hiyo ikiachwa iendelee tishio la
kutoweka kwa uoto huo ni kubwa sana. Takwimu pia zinaonyesha kuwa Tanzania ina
eneo la uoto wa asili lenye ukubwa wa takriban Hekta milioni 48.1 na kwamba
kasi iliyopo ya uharibifu ikiachwa iendelee itaiacha Tanzania bila uoto wa
asili baada ya miaka 129.
Takwimu hizi
zitabakia hivyo ikiwa idadi ya watu haitaongezeka, ukuaji wa shughuli za
kibinadamu hautaongezeka na aina ya shughuli hizo haitabadilika, jambo ambalo
haliwezekani. Hivyo basi upo uwezekano wa idadi ya miaka hiyo kupungua hata
kufikia nusu, sawa na umri wa kawaida kabisa wa binadamu.
Kutokana na
kuzingatia tishio hilo na umuhimu wa uhifadhi katika Taifa kiuchumi, kijamii na
kiikolojia, serikali ilitunga sera, sheria, kanuni na Taratibu kwa madhumuni
hayo. Sheria hizo ni pamoja na :
·
Sheria
ya Uhifadhi Wanyamapori, Na. 5 ya mwaka 2009
·
Sheria
ya Misitu, Na. 14 ya mwaka 2002
·
Sheria
ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Sura 284, R.E 2002
·
Sheria
ya Hifadhi za Taifa, Sura 282, R.E 2002
Kumekuwa na mazoezi
yanayoendelea nchini yanayohusu utekelezaji wa sheria hizo ambapo Wakala wa
Misitu Tanzania, Taasisi za hifadhi za Wanyamapori n.k zimekuwa zikiendesha
mazoezi kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mikoa
mbalimbali.
Kufuatia
uzoefu katika utekelezaji wa sheria hizi na maoni mbalimbali kutoka kwa
wananchi na wadau wengine, Serikali imekuwa ikitoa miongozo mbalimbali katika
mazingira tofauti na nyakati tofauti kwa kuzingatia sheria husika na kwa
kuzingatia, pamoja na mambo mengine:
·
Ongezeko
la idadi ya watu na milki zao zinazotokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi
na kijamii, dhidi ya ukubwa na ubora wa maeneo yaliyohifadhiwa yanayowazunguka,
ikiwa ni pamoja na misitu, mapori ya akiba, mapori tengefu, hifadhi za taifa,
njia za mapito ya Wanyamapori (wildlife corridors) na Maeneo ya mtawanyiko wa
Wanyamapori (Wildlife dispersal areas) yaliyohifadhiwa kwa miaka mingi.
·
Uvamizi
wa maeneo na kuendesha shughuli za kibinadamu kama vile kulima, kuchunga
mifugo, kujenga makazi, kuchimba madini, kukata miti hovyo na uvunaji mwingine
wa maliasili usiozingatia sheria
· Kupungua
hadhi kwa baadhi ya maeneo yaliyohifadhiwa hata kufikia viwango vya kupoteza
sifa zilizosababisha maeneo hayo kuhifadhiwa na hivyo kulisababishia Taifa
hasara kubwa kiuchumi, kiikolojia na kijamii
· Haja
ya kuboresha taarifa zinazoendana na wakati na uwiano sahihi kati ya ukubwa na
ubora wa ardhi iliyopo katika maeneo na mahitaji halisi ya ardhi (yakiwemo
maeneo yaliyohifadhiwa) na mipango ya matumizi bora ya ardhi.
· Haja
ya kuboresha njia za usimamizi na utekelezaji wa hatua mbalimbali za kisheria
kwa kuzingatia zaidi sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali kwa namna
endelevu.
Kwa
Taarifa hii, ambayo inatolewa na Wizara ikitekeleza maagizo ya mamlaka za juu za
Serikali, inaagizwa kama ifuatavyo:
Kama
ilivyoahidi Bungeni na kama ilivyokwishatoa maelezo katika nyakati tofauti,
serikali imekwishaunda kikosi kazi chenye wajumbe kutoka Wizara sita zinazohusika moja kwa moja na changamoto mbalimbali
za ardhi, kwa madhumuni mapana ya kufanya uchunguzi wa kina na kupitia sheria
zote zinazohusika kabla ya kuishauri serikali kuhusu namna bora zaidi na
endelevu ya kumaliza migogoro ya ardhi ikiwemo inayohusisha maeneo yaliyohifadhiwa.
Kikosi kazi hicho kinatarajiwa kukamilisha kazi yake hivi karibuni.
Katika
kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu na
endelevu wa migogoro ya ardhi:
· Viongozi na Watumishi wanaohusika
wasiwabughudhi wananchi na badala yake wazingatie taratibu katika kutekeleza
sheria wakati wa kushughulikia ukiukwaji wa sheria kwa wananchi walioko katika vitongoji
na vijiji vilivyosajiliwa.
· Wananchi walioko katika maeneo hayo
wasianzishe shughuli mpya za kibinadamu na wasiendelee na shughuli za
kibinaadamu zinazosababisha uharibifu wa mazingira na kuathiri tabia nchi
· Mifugo yote iliyoko ndani ya maeneo
yaliyohifadhiwa kisheria iondolewe haraka kwa kuzingatia taratibu
· Haitarajiwi kwamba Wananchi wengine
watatumia vibaya tamko hili na kuanza kuingia katika maeneo ya hifadhi kwa
shughuli zozote zile za kibinaadamu kwa kuwa vitendo hivyo havihusiani na tamko
hili na hatua kali zitachukuliwa mara moja dhidi ya wale watakaodiriki kwenda
kinyume.
Serikali inatarajia
kuendelea kupata ushirikiano kutoka kwa wadau wote wa uhifadhi na wananchi kwa
ujumla katika kutekeleza azma yake ya kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi
duniani zinazoendana na Malengo ya Dunia (Umoja wa Mataifa), ya Maendeleo
Endelevu (Sustainable Development Goals) kupitia uhifadhi endelevu wa maliasili
zake.
Wakati Serikali
inaendelea kutoa Elimu kwa njia mbalimbali na kufanya uhamasishaji, Wananchi
wanatarajiwa pia kujenga na kuimarisha uelewa, utayari na kushiriki katika
jitihada hizo za Serikali.
Imetolewa na;
Mhandisi Ramo Makani
Naibu Waziri, Wizara ya Maliasili na Utalii
13 Oktoba, 2016
No comments:
Post a Comment