NA HAMZA TEMBA - WMU
......................................................................
Kufuatia malalamiko ya wahifadhi juu ya kauli na vitendo mbalimbali za baadhi ya wananchi na viongozi wa kisiasa vyenye lengo la kukwamisha shughuli za uhifadhi nchini kwa maslahi yao binafsi kwa visingizio kuwa ni maagizo kutoka juu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa tamko na kusema kuwa hakuna kiongozi wa juu wa Serikali anayepinga zoezi la uhifadhi wa maliasili nchini.
Majaliwa
ameyasema hayo juzi wakati akizungumza na viongozi na watendaji wakuu wa Wizara
ya Maliasili na Utalii, wakuu wa taasisi za uhifadhi zilizopo chini ya wizara
hiyo na wakuu wa hifadhi za taifa pamoja na mapori ya akiba katika kikao
alichokiitisha kwenye ukumbi wa ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma.
“Wapo watu
wanaotumia majina ya viongozi wakuu kukwamisha mazoezi yanayoendeshwa na
wahifadhi nchini. Hakuna kiongozi wa juu anaeweza kuzuia zoezi muhimu kama
hili. Na Kama kuna mtu anakuja kukuambia wewe fulani kasema, mwambie
niunganishe na yeye mwenyewe. Tumeona maeneo mengi sana, watu wanafanya
madudu wanasema huyu kaagizwa kutoka juu, juu ni wapi, kwa Mkurugenzi wako? kwa
Katibu Mkuu? Naibu Waziri au Waziri? Au huku kwa Waziri mkuu? Makamu wa
Rais au Rais?,” alihoji.
“Fanyeni,
bora ukosee halafu tuseme hapo umekosea utarekebisha, kuliko kuogopa kufanya
kwa sababu mtu kakukwamisha, kwani ulivokuwa unaimplement (unafanya) alikuambia
nani? si kutokana na na sheria na taratibu, muhimu zaidi ni kuzingatia sheria
na taratibu, usije ukafanya mambo ya ajabu,” aliongeza.
Ili
kufanikisha zoezi hilo aliwaagiza pia kuhakikisha wanaweka alama za mipaka (beacons)
katika hifadhi zao hadi kufikia januari 31, 2017 ili kuepusha migogoro na
wananchi wanaovamia maeneo hayo kwa makusudi au kwa kutokujua maeneo ya mipaka
husika.
“Nendeni
mkawaambie mwisho ni hapa weka na beacon kabisa, na sheria zitachukua mkondo
wake kwa yeyote ambaye hatafata maelekezo yenu. Tatizo la migogo iliyozungumzwa
kati wa wafugaji na wahifadhi au wafugaji na kamati za ulinzi na usalama za
wilaya na mikoa ni lazma likafanyiwe kazi, lazima tuendelee kudhibiti kuingia mifugo
ndani ya mapori,” alisisitiza.
Aliwaagiza
pia kusimama kwenye majukwaa na kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi
wanaozunguka maeneo yao ya hifadhi. “Namba moja wa utoaji elimu ni wewe mkuu wa
pori, ni lazma utoe maelezo ya pori lako ni wapi linakoishia, kama mpaka huo ni
wa kisheria muwaambie, nini umuhimu wa kutoingia, wananchi wapate elimu namna
ya kuhifadhi pori na faida zake,” alisema.
Akizungumzia
changamoto iliyoibuliwa katika kikao hicho kuhusu mgongano uliopo katika
usimamizi wa misitu baina Wakala wa Huduma za misitu Tanzania na Serikali za
Mitaa alisema Serikali inaenda kuliangalia upya suala hilo ili ione namna bora
ya kutoa majukumu ya kusimamia rasilimali zote za misitu kwa chombo kimoja
tofauti na ilivyo hivi sasa, hatua ambayo inaelezwa kuwa itasaidia kwa kiasi
kikubwa kuondoa changamoto za uharibifu wa misitu nchini.
“Kama
ilivyoelezwa kuwa kuna mgongano wa majukumu kwenye kitengo cha misitu, baina ya
TFS na DFO (Ofisa misitu wa Wilaya), DFO anauza bila hata kumconsult (kumtaarifu)
TFS na anagonga na nyundo…, kwa hiyo tutaliangalia tuone majukumu yale na namna
ambavyo tunaweza tukayapa chombo kimoja ili kisimamie lakini TFS mmeperform
(mmefanya) vizuri endeleeni kufanya hivyo vizuri kwa sasa,” alisema huku akipigiwa
makofi na watendaji hao.
Changamoto
nyingine iliyoibuliwa katika kikao hicho ni matukio ya kuingizwa kwa mifugo
katika maeneo ya hifadhi yaliyoko mpakani huku asilimia kubwa ya mifugo hiyo
ikielezwa kutoka nje ya nchi, Waziri Mkuu Majaliwa amekemea kitendo hicho na
kuagiza mifugo hiyo iondolewe mara moja. “Hatutaki ng'ombe wa nje ya nchi
kuingia ndani ya nchi, mifugo ya ndani imetutosha,” alisema.
Aidha ameutaka
uongozi wa Wizara kuimarisha doria za mara kwa mara, kuongeza ajira za
makamanda (askari wa wanyamapori) na vitendea kazi muhimu vya kuimarisha doria
ikiwemo magari.
Kwa upende
wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe alisema ipo
changamoto kubwa ya tishio la kutoweka kwa mvua na kukauka kwa vyanzo muhimu
vya maji nchini kutokana na uharibifu wa maeneo yaliyohifadhiwa pamoja na
mlipuko wa magonjwa mbalimbali yanayosababishwa na muingiliano wa mifugo na
wanyamapori kama vile kimeta na homa ya bonde la ufa.
Naye
Mkurugenzi wa Idara ya Utalii wa Wizara hiyo, Zahoro Kimwaga alisema, umuhimu
wa uhifadhi una faida mtambuka ambapo sekta ya utalii pekee inachangia
asilimia 17 ya pato la taifa huku ikitoa ajira za moja kwa moja na zisizo za
moja kwa moja takriban milioni 1.5. Alisema sekta hiyo pia inachangia asilimia
25 ya mapato yote ya fedha za kigeni ikiwa ni sekta kiongozi kwa muda wa miaka
mitatu mfululizo.
Aliongeza
kuwa hadi kufikia Novemba 20 mwaka huu takwimu zinaonyesha kuwa maendeleo ya
sekta ya utalii yameongezeka kwa asilimia 5 licha ya malalamiko mbalimbali kuhusu
sekta hiyo baada ya Serikali kuweka kodi ya VAT katika huduma za kitalii nchini.
No comments:
Post a Comment