slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Thursday, April 13, 2017

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAANZA KUKUSANYA MAONI KUTOKA KWA WADAU WA UTALII YA KUBORESHA SERA YA TAIFA YA UTALII YA MWAKA 1999


Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki akizungumza katika mkutano huo.
 Picha ya pamoja.
Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Zahoro Kimwaga akizumza katika mkutano huo.

Na. Lusungu Helela - WMU
......................................................
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imewataka wadau wa Utalii nchini kutoa maoni yenye tija itakayopelekea upatikanaji wa Sera bora itakayoleta ufanisi katika uendeshaji wa huduma zinazotolewa katika sekta ya Utalii. 

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni miaka 17 sasa tangu Sera ya Taifa ya Utalii iliyopo ifanyiwe mapitio kwa mara ya mwisho mwaka 1999.  

Katika kutambua hilo, Wizara imeanza kupitia upya Sera hiyo ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Utalii inakwenda sambamba na mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani yakiwemo ya kiteknolojia, kijamii, kiuchumi, kisiasa na mazingira

Akizungumza katika mkutano  uliofanyika kwa muda wa siku mbili  Jijini Arusha kwa mikoa ya kanda ya Kaskazini, Naibu Katibu Mkuu  wa Wizara hiyo, Dkt. Aloyce Nzuki alisema Sera hiyo inafanyiwa marekebisho kwa kuwa imepitwa na wakati kutokana na mabadiliko makubwa yaliyotokea katika sekta hiyo kwa sasa. 

Aidha, alisema kwa kutambua mchango wa utalii kiuchumi , ni wazi kuwa sera wezeshi ya utalii yenye kutoa mwongozo wa utaratibu bora na sahihi wa usimamizi, uendelezaji na utendaji katika sekta hiyo  unahitajika.

"Tunataka kuibadilisha sera hiyo ili iweze kujibu changamoto za aina ya utalii wa sasa ambao kipindi cha nyuma haukuwepo", ametea mfano utalii mikutano pamoja na utalii wa kiutamaduni ambao umekuwa ukikua kwa kasi hapa nchini.

Kutokana na hali hiyo,  Dkt. Nzuki amesema marekebisho ya Sera hiyo yanahitaji mchango mkubwa kutoka kwa wadau kwa kuwa  inaendeshwa kwa kiasi kikubwa na Sekta Binafsi katika kutoa huduma na kufanya biashara za utalii hapa nchini.

Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Zahoro Kimwaga alisema uhuishwaji wa Sera hiyo utazingatia namna ambavyo wazawa wataweza kuwa wanufaika namba moja kwa kuwaandalia mazingira rafiki ya kuendesha biashara ya utalii tofauti na sasa ambapo makampuni mengi ya utalii ni ya watu kutoka nje. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TATO, Wilbert Chambulo alisema suala la kuifanyia marekebisho ya sera hiyo ni jambo jema ila sasa serikali iangalie namna ya kuboresha mashirikiano katika utoaji wa maamuzi kwa wafanyabiashara wa utalii nchini badala  ya kuamua peke yake.

Mkutano huo wa kukusanya maoni kutoka kwa wadau umeanza kufanyika mkoani Arusha kwa kuwashirikisha wadau kutoka mikoa minne ya Kanda ya Kaskazini na badaaye utafanyika katika kanda zingine kwa muda wa siku mbili kila kanda kwa ushirikiano kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii,   Shirikisho la Vyama Vya Utalii Tanzania  (TCT) pamoja na Benki ya Dunia chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu

No comments:

Post a Comment