JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA
Wizara ya Maliasili na
Utalii imesitisha utoaji wa vibali vya kusafirisha mkaa kutoka Wilaya moja hadi
nyingine kuanzia terehe 01 Julai mwaka huu.
Agizo hilo limetolewa na
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe na kuungwa mkono na Baraza
la wafanyakazi la Wizara wa Maliasili na Utalii kwa lengo kupunguza uharibifu
mkubwa wa mazingira hususan ukataji wa miti hovyo.
Baraza hilo lililofanyika
mjini Dodoma tarehe 10 Aprili, 2017 pia lilijadili umuhimu wa kutumia mkaa
mbadala kwa miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya ambapo mpango
mahususi wa kutumia mkaa mbadala utakaozalishwa na kiwanda cha Mufindi – Iringa
utawasilishwa ifikapo mwezi Julai mwaka huu.
Baraza la Wafanyakazi wa
Maliasili na Utalii pia limepitisha kwa kauli moja kuongeza jitihada katika
kukabiliana na ujangili hasa katika Pori la Akiba la Selous, Pori Tengefu la
Loliondo, Rungwa na Yaeda Chini. Nguvu zaidi ya kukabiliana na changamoto ya
uingizaji wa mifugo katika maeneo ya hifadhi ambao unachangia kwa kiasi kikubwa
ongezeko la ujangili pia ilijadiliwa.
Aidha, Baraza liliazimia
mali za majangili pamoja na mifugo itakayokamatwa katika maeneo ya hifadhi
yataifishwe kwa mujibu wa sheria.
Katika kukabiliana na
changamoto ya usafirishaji wa magogo nje ya nchi, Baraza liliazimia kuwa
usafirishaji wa magogo ufanyike kwa kutumia nyaraka halisi (Original Documents)
badala ya vivuli vya nyaraka (Photocopy).
Baraza hilo la Wafanyakazi
pia liliazimia kuwa watumishi wote wa wizara wazingatie sheria na kanuni za
utumishi wa umma katika maeneo yao ya kazi pamoja na utoaji wa huduma kwa Umma.
Mkutano huo wa Baraza la
Wafanyakazi hufanyika mara mbili kwa mwaka kwa lengo la kupitia utekelezaji wa
bajeti ya mwaka uliopita na kutoa maoni yao kwa bajeti ya Wizara inayotarajiwa
kuwasilishwa bungeni pamoja na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili na
kuweka mkakati wa kukabiliana nazo. Wajumbe wa Baraza hilo ni wawakilishi wa
watumishi kutoka katika Idara, Vitengo, Taasisi na Vituo vya Wizara.
Imetolewa
na;
Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Maliasili na
Utalii,
11
Aprili, 2017
Dodoma.
Hongereni sana kwa kuliona hili swala la uvunaji msitu kiholela maana sasa ivi ukienda mapori yote yaliopo mkoani mbeya kama upendo na mamba pfm mengi yamevamiwa sana na kumekuwa na ukwepaji mkubwa wa ushuru wa serekali kuu na vijinini pia wanakijiji awafaidiki na haya me naomba hii sera ya pfm iangaliwe mara mbili maana haina tija kwa wanakijiji na mapori yanazidi kupotea.. pia kwenge swala la mifugo kuingia hifadhini hasa selous na mbuga zingene hasa ambazo zipo karibu na kabila la wamasai ukiangalia kwa undani zaidi utaona watu ambao wanazunguka hizo hifadhi awana ile elimu juu ya faida za uwepo kwa hifadhi ivyo wapewe elimu kidogo kidogo jamii itaelewa umuhimu wa wangama pori pia naomba usihano kati hifadhi na jamii .nawasilisha
ReplyDelete