slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Thursday, September 28, 2017

MAKAMU WA RAIS, MHE. SAMIA SULUHU HASSAN KUZINDUA MAKUMBUSHO MAPYA YA OLDUVAI NA ONESHO LA CHIMBUKO LA MWANADAMU TAREHE 03 OKTOBA, 2017 MKOANI ARUSHA

Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Morogoro kuhusu uzinduzi wa Makumbusho Mapya ya Olduvai na Onesho la Chimbuko la Mwanadamu ambayo yatazinduliwa tarehe 03 Oktoba, 2017 na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika eneo la Olduvai wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha. 
 Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Morogoro kuhusu uzinduzi wa Makumbusho Mapya ya Olduvai na Onesho la Chimbuko la Mwanadamu ambayo yatazinduliwa tarehe 03 Oktoba, 2017 na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika eneo la Olduvai wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha. (Picha na Hamza Temba - WMU)

Morogoro, Septemba 28, 2017
.........................................................................
Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya imekamilisha ujenzi wa Makumbusho mapya ya Olduvai ambayo yanaonesha Chimbuko la Binadamu (The Cradle of Humankind) katika Bara la Afrika.
Makumbusho hayo mapya pamoja na Onesho la Chimbuko la Binadamu, yatafunguliwa rasmi na  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tarehe 03 Oktoba, 2017 katika eneo la Olduvai, ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Onesho hilo ni matokeo ya utafiti wa muda mrefu uliofanyika katika Bonde la Olduvai na Laetoli katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha. Wananchi, viongozi mbalimbali wa kitaifa na Mabalozi wanatarajiwa kuhudhuria kwenye hafla hiyo.
Idadi kubwa ya vioneshwa katika Makumbusho hiyo, vilipatikana katika bonde la Olduvai na Laetoli nchini Tanzania kupitia utafiti wa kisayansi wa muda mrefu na vilikuwa vimehifadhiwa katika Makumbusho ya Taifa, Jijini Dar es Salaam. Vioneshwa hivi ni pamoja na masalia ya zamadamu, zana za mawe na masalia ya wanyama walioishi takribani miaka milioni 4 iliyopita.
Makumbusho hayo yamepangwa kuonesha sehemu kuu nne zinazowiana.  Sehemu ya kwanza inahusu ushahidi wa nyayo za zamadamu zilizongunduliwa huko Laetoli mwaka 1978 na mtafiti Dr. Mary D. Leakey.  Nyayo hizi ziliachwa na zamadamu anayeiitwa Australopithecus afarensis na ndio ushaidi usiopingika wa zamadamu kutembea wima kwa miguu miwili takribani miaka milioni 3.6 iliyopita.
Sehemu ya pili inahusu hadithi ya kusisimua ya kuwa binadamu (Genus Homo); ambapo kutakuwa na masalia ya zamadamu wanaoitwa Zinjanthropus au Paranthropus boisei na Homo habilis, zana za mawe za mwanzo zilizotumika (Oldowan) katika kujipatia chakula na ushahidi wa kale wa ulaji wa nyama katika historia ya mabadiliko ya binadamu, takribani miaka million 2 iliyopita.
Sehemu ya tatu inahusu maisha ya jamii ya Homo erectus.  Jamii hii ilikuwa inafanana zaidi na binadamu wa sasa kuliko jamii zilizotangulia. Kutakuwa na masalia zamadamu Homo erectus, zana za mawe (Acheulian) na ushahidi wa ulaji wa wanyama wakubwa kama vile Nyati na tembo katika historia ya mabadiliko ya binadamu, takribani miaka million 1.7 iliyopita.
Sehemu ya nne inaonesha kipindi cha mwanzo cha binadamu wa sasa (Homo sapiens) walioanza kutokea hapa Afrika miaka laki 2 iliyopita. Sehemu hii pia itaonesha mila na utamaduni wa makabila mbalimbali kama vile Wahadzabe, wamasai na Datoga.  Kutakuwa na mavazi ya asili ya jamii hizo, zana za kuwinda na vifaa mbalimbali wanavyovitumia katika maisha yao ya kila siku.
Wizara ya Maliasili na Utalii inawakaribisha wananchi wote kuhudhuria ufunguzi huo ambapo watapata pia fursa ya kutembelea vivutio vingine vilivyopo ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ili kujifunza na kufurahia urithi huu wa asili na kiutamaduni wa Taifa letu.
Imetolewa na;

Prof. Jumanne Maghembe
Waziri wa Maliasili na Utalii

No comments:

Post a Comment