slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Wednesday, June 14, 2017

WIZARA MALIASILI KUPITIA BODI YA UTALII TTB YATOA SEMINA KWA WABUNGE WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA PIC MJINI DODOMA

NA HAMZA TEMBA - WMU
.................................................................................
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania TTB, imefanya semina ya mafunzo ya siku moja kwa wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kwa lengo la kuwajengea uelewa wajumbe hao kuhusu majukumu ya taasisi hiyo ambayo imefanyika jana mjini Dodoma na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Ramo Makani na Katibu Mkuu, Meja Jenerali Gaudence Milanzi.

Akizungumza katika semina hiyo, Meneja wa Huduma za Utalii wa taasisi hiyo, Philip Chitaunga alisema bodi hiyo iliyoanzishwa mwaka 1993 ilipewa jukumu la jumla la kukuza sekta ya utalii nchini ikiwemo kutumia mbinu mbalimbali za utangazaji, kuhamasisha uendelezaji wa mazao ya utalii na miundombinu yake, kufanya tafiti za masoko na utalii kwa ujumla pamoja na kuhamasisha uelewa wa watanzania kufahamu umuhimu na faida za utalii.

Alisema taasisi hiyo imefanya juhudi mbalimbali za kutangaza utalii wa Tanzania nje ya nchi ikiwemo kuratibu ziara za waandishi wa habari za kitalii, kuweka matangazo katika magazeti ya utalii ya kimataifa, kushiriki katika maonesho ya utalii ya kimataifa na kutangaza kupitia Televisheni za kimataifa kama CNN ya Marekani.

“Jitihada zingine tulizofanya ni kutumia balozi zetu nje ya nchi na mabalozi wa utalii wa hiari yaani 'Goodwill Ambasadors', kutumia mitandao ya kijamii na matangazo kwenye vyombo vya usafiri vya umma ambapo mwaka 2008 hadi 2009 tulitangaza kwenye mabasi 124 jijini london Uingereza, taxi 100, treni mbalimbali na katika uwanja wa ndege wa Heathrow” alisema Chitaunga.

Alisema jitihada za hivi karibuni za kutangaza utalii zimefanyika kupitia michezo ya Ligi Kuu ya Uingereza ikiwemo timu za mpira wa miguu za Seattle Sounders na Sunderland, kupitia majarida, CD na filamu fupi kwa lugha mbalimbali kama Kiingereza, Kijerumani, Kifaransa na Kiswahili. Pia, kupitia tovuti maalum ya utalii ya taifa (www.tanzaniatourism.gotz), App kwenye ‘Smart Phones’ na kufanya ziara za utangazaji wa utalii yaani Roadshows katika nchi za China, Afrika ya Kusini, bara la Ulaya, Amerika na Australia.

Kwa upande wa jukumu la kuhamasisha utalii wa ndani, Chitaunga alisema bodi imetekelza jukumu hilo kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya habari nchini pamoja na mitandao ya kijamii, kushiriki katika maonesho mbalimbambali ya ndani ya nchi kama vile Sabasaba na Kili Fair, kuhamasisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo, kuendesha matangazo mbalimbali ya Radio na TV na kuweka mabango maeneo mbalimbali ikiwemo ya mpakani na kwenye viwanja vya ndege.

Aliseme katika kuhamasisha utalii wa ndani, siku za hivi karibu TTB imeingia makubaliano na chama cha wenye mabasi nchini TABOA ambapo filamu mbalimbali zinazohamasisha utalii wa ndani zitaoneshwa katika mabasi zaidi ya 300 ya mikoani.

Akizungumzia kuhusu mafanikio, alisema taasisi hiyo imechangia ongezeko la idadi ya watalii wa kimataifa nchini kutoka 230,166 mwaka 1993 na kufikia 1,284,279 mwaka 2016. Aidha, mapato yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani Milioni 146.84 na kufikia Dola za Kimarekani Milioni 2,132 huku sekta hiyo ya utalii ikichangia asilimia 17.5 ya pato la taifa.

Alisema mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na Tanzania kupata umaarufu mkubwa zaidi duniani ambapo mitandao na kampuni mbalimbali za safari za kitalii ikiwemo Safari Bookings, Fox News.com na New York Times zimeitambua kama eneo bora la utalii barani Afrika. Aidha, Mlima Kilimanjaro, Bonde la Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti zimetambuliwa kama miongoni mwa maajabu saba barani Afrika huku kampuni ya World Travel Awards ikiutambua Mlima Kilimanjaro kama kivutio bora zaidi barani Afrika.

“Baadhi ya watu maarufu duniani kutembelea Tanzania kama vile Oprah Winfrey, Bill Gates, Will Smith, Roman Abramovic, David Beckham, Moussa Sissoko na Waziri Mkuu Mstaafu wa Israel, Ehud Barak ni sehemu pia ya viashiria vya mafanikio kwa taasisi yetu kutangaza utalii wa Tanzania nje ya nchi”, alisema Chitaunga.

Aliongeza kuwa, watu maarufu kuja kuandaa filamu zao Tanzania ni sehemu ya mafanikio ya kutangaza utalii wa Tanzania nje ya nchi, “Watu mashuhuri saba kutoka China hivi karibuni wameandaa filamu itakayorushwa katika Anhui TV inayotazamwa na watu zaidi ya milioni 800 duniani” alisema.

Katika jitihada za kutangaza utalii wa Tanzania kupitia shirika la ndege la Air Tanzania Chitaunga alisema, “TTB sasa inaandaa gazeti la Air Tanzania litakalojulikana kama Safari Njema kwa ajili ya kutangaza utalii wa Tanzania na vivutio vyake pamoja na kuimarisha usafiri wa anga kupitia shirika hilo la Umma”.

Alisema pamoja na mafanikio hayo, bodi hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu hafifu katika baadhi ya maeneo ya vivutio vya utalii, changamoto ambayo imeanza kufanyiwa kazi na Serikali ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa, uimarishaji wa viwanja vya ndege na kuimarisha shirika la ndege la Air Tanzania.

Alisema changamoto nyingine ni ufinyu wa bajeti ya utangazaji, hofu ya matukio ya ugaidi na mlipuko wa magonjwa katika bara la Afrika, upungufu wa vyumba vya malazi katika baadhi ya maeneo yenye vivutio vya utalii, mtazamo hasi kuwa Tanzania ni ghali na mtazamo kuwa jukumu la utangazaji na uendelezaji utalii ni la Wizara na Taasisi zake pekee. Alisema changamoto zote hizo zinafanyiwa kazi ikiwemo kuhamasisha wawekezaji kuwekeza katika sekta ya utalii na watanzania kuona umuhimu wa utalii na kuutangaza pamoja kuwatoa hofu watalii na kuwawekea mazingira bora na rahisi ya kutembelea Tanzania.

Akizungumzia mipango ya baadaye ya taasisi hiyo, Chitaunga alisema ni pamoja na kutafsiri tovuti ya utalii ya Taifa katika lugha ya Kijerumani, Kichina na Kiswahili, kuendeleza juhudi za kufungua masoko mapya ya utalii kama vile China, Israel, Urusi na India, kuimarisha utangazaji wa utalii kupitia TEHAMA, kuongeza idadi ya mabalozi wa hiari katika masoko mahususi ya utalii, uwekaji wa mabango, tafiti za masoko mapya ya utalii na kuandaa filamu mpya za kuitambulisha Tanzania ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Albert Obama aliipongeza Wizara na TTB kwa semina hiyo pamoja na jitihada wanazozifanya za kutangaza utalii wa Tanzania ndani na nje ya nchi na kutaka juhudi zaidi ziongezwe huku baadhi ya wabunge waliochangia wakiitaka Serikali iongeze uwekezaji katika bajeti ya utangazaji ili taasisi hiyo iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Naye Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani alisema ushauri uliotolewa na wabunge hao utafanyiwa kazi na hoja zote zilizowasilishwa zitajibiwa kwa maandishi huku Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akihitimisha kwa kusema kuwa Wizara imepiga hatua kubwa ya kukabiliana na ujangili ndani na nje ya maeneo ya hifadhi nchini. 
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (kushoto) akizungumza jana mjini Dodoma katika semina iliyoandaliwa na Wizara hiyo kupitia Bodi ya Utalii Tanzania kwa ajili ya kuwajengea uelewa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu majukumu ya bodi hiyo. Kulia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Albert Obama. 
Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi (kushoto) akizungumza jana mjini Dodoma katika semina iliyoandaliwa na Wizara hiyo kupitia Bodi ya Utalii Tanzania kwa ajili ya kuwajengea uelewa wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu majukumu ya bodi hiyo. Katikati ni Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Albert Obama.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Albert Obama (kulia) akizungumza jana mjini Dodoma katika semina iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili kupitia Bodi ya Utalii Tanzania kwa ajili ya kuwajengea uelewa wajumbe wa kamati hiyo kuhusu majukumu ya bodi hiyo. Katikati ni Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi. 
Meneja wa Huduma za Utalii wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Philip Chitaunga (kushoto) akiwasilisha mada ya jumla kuhusu shughuli za taasisi hiyo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) katika semina iliyoandaliwa na Wizara hiyo kupitia bodi hiyo mjini Dodoma jana. 
Meneja wa Huduma za Utalii wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Philip Chitaunga (kushoto) akiwasilisha mada ya jumla kuhusu shughuli za taasisi hiyo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) katika semina iliyoandaliwa na Wizara hiyo kupitia bodi hiyo mjini Dodoma jana. 
 Meneja wa Huduma za Utalii wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Philip Chitaunga (kushoto) akiwasilisha mada ya jumla kuhusu shughuli za taasisi hiyo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) katika semina iliyoandaliwa na Wizara hiyo kupitia bodi hiyo mjini Dodoma jana. 
 Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) wakiangalia video zilizoandaliwa na TTB kwa ajili ya kutambulisha utalii wa Tanzania ndani na nje ya nchi katika semina iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili kupitia bodi hiyo mjini Dodoma jana.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) na Mbunge wa Viti Maalum, Riziki Lulida akichangia jana mjini Dodoma katika semina iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili kupitia Bodi ya Utalii Tanzania kwa ajili ya kuwajengea uelewa wajumbe wa kamati hiyo kuhusu majukumu ya bodi hiyo. Kulia ni Katibu Mkuu wa hiyo Meja Jenerali Gaudence Milanzi.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) wakiwa katika semina hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili kupitia Bodi ya Utalii Tanzania mjini Dodoma jana.
Meneja Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania, Geofrey Meena akifafanua jambo katika semina hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili kupitia Bodi ya Utalii kwa ajili ya kuwajengea uelewa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu majukumu ya bodi hiyo.

No comments:

Post a Comment