slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Monday, March 25, 2019

SERIKALI KUNYANG'ANYA HOTELI ILIZOZIBINAFSISHA




Serikali imeanza ukaguzi wa hoteli za Kitalii ilizozibinafsisha  kwa Wawekezaji na wale watakaobainika kuziendesha chini ya kiwango, watanyang'anywa na kupewa wawekezaji wengine walio tayari kuziendesha kwa manufaa ya kukuza utalii nchini.

Hatua hiyo inafanyika kufuatia  kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa watalii na wadau mbalimbali wa utalii juu ya  huduma  zisizoridhisha zinazotolewa na hoteli hizo.

Akizungumza mara baada ya kukagua baadhi ya hoteli za Kitalii ikiwemo ya   Soronera na Lobo, zilizo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara, Naibu Waziri wa  Maliasili na Utalii, Mhe Constantine Kanyasu  amesema lengo la kubinafsishwa kwa Hoteli hizo ilikuwa  ni kuboresha huduma.

Pia,  Hoteli ya Musoma ya mkoani Mara  pamoja na Ngorongoro Wildllife iliyopo ndani ya Mamlaka ya Eneo la Ngorongoro ni  miongoni mwa hoteli   zilizofanyiwa ukaguzi.

Amesema  Mwekezaji asiyefanya hivyo atanyang'anywa umiliki ili apewe mwekezaji   mwingine mwenye uwezo wa kutoa huduma bora.

 Aidha, amesema  kumekuwa na tuhuma kwa baadhi ya hoteli zilizobinafsishwa kukwepa kodi ya tozo ya huduma pamoja kuwalipa wafanyakazi wazawa mishahara midogo huku wale wa kigeni wakilipwa mishahara mikubwa kwa kazi ya aina moja.

Mhe. Kanyasu amesisitiza kuwa, Serikali ilizibinafsisha hoteli hizo ili zilete mapinduzi katika nyanja ya ajira, huduma bora kwa watalii, kodi pamoja kuziboresha ili zikidhi soko la watalii kwa sasa.

Akizungumza mara baada ya kukagua hoteli hizo,Mhe Kanyasu amebainisha  baadhi vitu alivyoviona ikiwemo uchakavu wa miundombinu pamoja na udanganyifu wa idadi ya watalii wanaofikia katika hoteli hizo .

Amesema Wizara  itapeleka idadi ya hoteli zitakazobainika kwenda kinyume  ili Msajiri wa Hazina  aweze kuzifutia  umiliki.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kanyasu  amewataka viongozi wa Hoteli hizo kukaa na kuona ni namna watakavyoongeza idadi ya Watanzania wanaotembelea hifadhi na kupata mapumziko katika Hoteli hizo.

 Kuhusu Tozo ya huduma ya Mapato amezielekeza Halmashauri mbalimbali ikiwemo ya Serengeti kupata taarifa sahihi kutoka  Hifadhi za Taifa ( TANAPA)

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya  Serengeti,  Victor Tonesha  amesema changamoto inayoikabili Halmashauri hiyo ni ya  kushindwa kubaini kiwango halisi cha fedha zinazotolewa na Wawekezaji hao.




Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,  Constantine Kanyasu (katikati)  akizungumza na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya y Serengeti ikiongozwa na  Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu  mara baada ya kukagua hoteli ya Soronera  iliyopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti  mkoani Mara kwa lengo la kubaini hoteli zilizobinafsishwa na serikali ambazo zimekuwa hazifanyi vizuri.

  


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,  Constantine Kanyasu (kulia) akiwa pamoja na  Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa ( TANAPA), Martin Looiboki wakiwa wameambatana kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya  Serengeti  wakiwa katika hoteli ya Soronera  iliyopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti  mkoani Mara wakiwa wanaikagua kwa lengo la kubaini hoteli zilizobinafsishwa na serikali ambazo zimekuwa hazifanyi vizuri.



Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,  Constantine Kanyasu (kulia) akizungumza na Meneja wa Hoteli ya Soronera,Asram Narwat  katika jiko la hoteli hiyo wakati Naibu Waziri huyo alipokuwa akiikagua hoteli ambayo ni miongoni mwa hoteli ambazo zilibinafsishwa na Serikali kwa Wawekezaji kwa lengo la kuboresha Huduma kwa watalii. Hoteli hiyo ipo ndani ya Hifadhi ya Serengeti mkoani Mara kwa  lengo la kukagua ili  kubaini hoteli zilizobinafsishwa na serikali ambazo zimekuwa hazifanyi vizuri.





Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,  Constantine Kanyasu (kulia) akiwa pamoja na  Mkuu wa  wa wilaya  ya Serengeti, Nurdin Babu wakiongozwa na  Meneja wa Hoteli  ya Soronera, Asram Narwat katika Hoteli ya Soronera  iliyopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti  mkoani Mara, Hoteli hiyo ipo ndani ya Hifadhi ya Serengeti mkoani Mara kwa  lengo la kukagua ili  kubaini hoteli zilizobinafsishwa na serikali ambazo zimekuwa hazifanyi vizuri



Muonekanao wa hoteli ya Soronera kwa upande wa ndani kati vyumba vya hoteli hiyo iliyopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara amabayo ni moja ya Hoteli ilyobinafsishwa na Serikali kwa Wawekezaji.


Friday, March 22, 2019

WAVAMIZI SHAMBA LA MITI BIHARAMULO WAPEWA MIEZI 3



Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ametoa muda wa miezi mitatu kwa wananchi waliovamia na kuanzisha shughuli za kibinadamu ndani ya Shamba la miti la Biharamulo kuondoka mara moja kwa hiari yao bila shuruti kabla ya mwezi Juni mwaka huu.

Ametoa muda huo ili wananchi  waliolima   mazao mbalimbali yakiwemo  mahindi na pamba  waweze kuvuna mazao yao  kabla ya kuanza kwa oparesheni maalum ya kuwaondoa, iliyopangwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi Julai mwaka huu itakayofanywa na Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania ( TFS) kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo.

Mhe.Kanyasu  ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kikazi ya   kutembelea shamba la miti Biharamulo lililopo katika wilaya ya Chato mkoani Geita.

Amesema Oparesheni hiyo haitasubiri taarifa ya Wizara tano inayoendelea kufanyiwa kazi kwa kuwa eneo hilo halihusiani na vile vijiji 366  vilivyokutwa ndani ya Hifadhi.

Amesema  haiwezekani wananchi waliovamia eneo hilo waendelee kuachwa kwa kisingizio cha Kauli ya Rais aliyoitoa Januari 15 mwaka huu kuhusiana na vijiji 366 vilivyokutwa ndani ya maeneo ya Hifadhi.

Amebainisha kuwa wananchi waliovamia eneo hilo wameitafsiri visivyo Kauli hiyo na kuongeza kuwa baada tu ya tamko la Mhe. Rais , baadhi ya wananchi hata wale waliokuwa wakiishi  katika maeneo mengine nje ya hifadhi waliendelea  kuvamia na kuanza kujimilikishia  maeneo makubwa  wakidai kuhalalishwa na tamko la Rais.

Amefafanua kuwa taarifa inayoendelea kufanyiwa kazi  na timu ya Mawaziri na Makatibu Wakuu kutoka Wizara tano imebainisha kuwa mpaka sasa zaidi ya vijiji 700 vimekutwa ndani ya Hifadhi badala 366 vilivyoripotiwa awali.

Kufuatia hali hiyo amesema baadhi ya wavamizi wa Hifadhi katika maeneo mbalimbali wataendelea kuondolewa bila kusubili kukamilika kwa zoezi linaloendelea kwa kuwa walieendelea kuvamia maeneo ya Hifadhi kwa kisingizio cha tamko la Rais huku maeneo hayo yakizidi kuharibiwa kwa miti kukatwa na shughuli nyingi za kibinadamu

Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu ameiagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) kutenga Bajeti ya kugharamia operesheni ya kuwaondoa  wavamizi ndani ya Shamba hilo.

Ameitaka TFS kuendesha oparesheni za mara kwa mara ili wavamizi hao wajue Serikali ipo kazini kulinda rasilimali za Taifa muda wote.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Chato,  Mtemi Simeoni akizungumza katika ziara hiyo  alisema kuwa  baadhi ya wananchi kutoka nje ya wilaya hiyo wamekua wakivamia na kuanzisha shughuli za kibinadamu ndani ya Shamba hilo, suala ambalo ni kinyume cha sheria.


Mkuu huyo wa wilaya amebainisha kuwa wananchi katika maenro hayo wana mahitaji makubwa ardhi na kuiomba Wizara iangalie  namna ya kuwasaidia  hekari 5000 ili wapate maeneo ya kulima na kuchungia mifugo yao.

Kwa upande wake Meneja wa Shamba hilo Bw. Thadeus Shirima  amemweleza Naibu Waziri huyo kuwa hadi sasa zaidi ya hekari 900 zimepandwa miti licha ya Shamba hilo  kukabiliwa  na changamoto ya uhaba wa watumishi pamoja na vitendea kazi.




 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu (katikati)  akizungumza   na Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhe.  Mtemi Simeoni (kushoto)   wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea Shamba la Miti la Biharamulo mara baada  ya kukagua maendeleo ya miti iliyopandwa katika shamba hilo kwa  ukubwa  wa hekari 900 katika wilaya ya Chato mkoani Geita., Kulia ni Meneja wa shamba hilo, Edward Nyondo.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akimsikiliza  Mkuu wa Wilaya ya Chato,  Mhe. Mtemi Simeoni (kushoto)  alipotembelea Shamba la Miti la Biharamulo mara baada  ya kukagua maendeleo ya miti iliyopandwa katika shamba hilo  kwa  ukubwa hekari 900 katika wilaya ya Chato mkoani Geita. Wengine ni watumishi pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo





 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu  akizungumza na  wananchi pamoja na watumishi wa shamba la miti la Biharamulo ambalo mara baada ya kukamilika kwa kupandwa miti katika eneo lote litakuwa ndio  shamba la pili kwa ukubwa kati ya mashamba  20 yanayomilikiwa na Wakala wa Hudumza Misitu Tanzania lililopo wilayani Chato mkoani Kagera.




 Mkuu wa wilaya ya Chato, Mhe. Mtemi Simeon akipanda mti wakati alipotembelea Shamba la Miti la Biharamulo mara baada  ya kukagua maendeleo ya miti iliyopandwa katika shamba hilo lenye ukubwa wa  hekari 900 katika wilaya ya Chato mkoani Geita
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa wilaya na watumishi wa Shamba la Miti la Biharamulo lililopo katika wilaya ya Chato mkoani Geita.



.Baadhi ya watumishi wa Shamba la Miti la Biharamulo wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii wakati Naibu Waziri huyo alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika shamaba hilo hukuakiwasisitizan umuhimu wa kufanya kazi kwa kushirikiana na wananchi wanaoishi karibu na shamba hilo.



















Monday, March 18, 2019

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUJA NA MKAKATI MAALUM WA KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII



Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu amesema Wizara ya Maliasili na Utalii  inatarajia kuja na mkakati maalum wa kutangaza utalii ndani na nje ya nchi kwa kunadi  maeneo ya vivutio vya utalii badala ya kuinadi nchi kwa ujumla na  vivutio vyake

Pia,Amesema  maeneo hayo yatakuwa yakinadiwa  kwa mfumo wa vifurushi (Packages) hali itakayopelekea mtalii akija nchini ataweza kutembelea maeneo ya  Hifadhi,  Misitu ya Mazingira asilia pamoja na  maeneo ya utalii wa kiutamaduni.

Amesema lengo la kuja na mkakati huo ni kusaidia maeneo hayo kuweza kujulikana pamoja na kumuwezesha mtalii kuweza kuvifahamu vivutio vinavyopatikana katika eneo hilo kwa undani badala ya kuitangaza nchi kwa kujumuisha vivutio vya utalii vilivyopo  kwa ujumla wake.

Amesema mkakati huo utasaidia  kuongeza idadi ya watalii katika maeneo yenye vivutio ya utalii lakini kwa sasa yamekuwa yakipata idadi ndodgo ya watalii kwa vile yamekuwa hayafahamiki ipasavyo.

Amesema mkakati huo utalenga zaidi katika maeneo yenye utalii wa kiutamaduni pamoja na maeneo ya Misitu asilia, Ni utalii mpya ambao kwa Tanzania haufahamiki sana unaojikita kuangaliia viumbe ambao wapo hatarini kutoweka.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri huyo mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi pamoja na Msitu Asilia wa Chome katika wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Ameeleza kuwa aina hiyo ya kutangza vivutio vya utalii katika eneo fulani badala ya nchi italeta manufaa makubwa kwa Hifadhi na maeneo yale ambayo kwa sasa yamekuwa yakipokea idadi ndogo ya watalii hasa katika ukanda wa Kusini na Magharibi.

Amesema ukizungumzia utalii kwa sasa unalenga mikoa ya Kaskazini ambako zaidi ya asilimia 80 unafanyika ukanda huko huku kanda nyingine kama vile kanda ya ziwa, Magharibi pamoja na Kusini zikiwa bado idadi ya watalii wanaotembelea ni ndogo ukilinganisha na uwingi wa vivutio vya utalii vilivyopo katika maeneo hayo.

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Shabani Shekilindi amesema Tanzania imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii lakini mapato yatokanayo na utalii hayaakisi ualisia wa vivutio vilivyopo nchini hivyo mikakati mipya ya kutangaza vivutio inahitajika.


 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii, Shabani Shekilindi (wa kwanza kushoto) akiwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ( wa pili kushoto) wakiwa pamoja na Wajumbe wa kamati hiyo wakipewa maelezo mafupi kuhusu mradi wa kuzalisha faru weusi na mbwa mwitu kutoka kwa Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) unaofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi wakati Kamati ilipofanya ziara katika Hifadhi hiyo iliyoko mkoani Kilimanjaro.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akipigiwa saluti na watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi wakati alipokuwa ameongozana na Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii ilipotembelea eneo hilo kwa ajili yamradi wa kuzalisha faru weusi na mbwa mwitu
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii kutembelea eneo la maradi wa kuzalisha faru weusi na mwitu katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi mkoani Kilimanjaro. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki.



 Baadhi ya Wajumbe wa  kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii walipotembelea ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania iliyopo katika wilaya ya  Same







SERIKALI YAPANIA UWEKEZAJI UTALII KANDA YA ZIWA



Serikali imesema kuwa itaendelea kuweka mazingira rafiki, kuwahamasisha na kuwavutia Wawekezaji watakaosaidia kuwapeleka watalii katika maeneo ya Kanda ya Ziwa ili kukuza Sekta ya Utalii Katika maeneo hayo.

Hatua hiyo inakuja baada ya kuyapandisha hadhi Mapori ya Akiba ya  ya  Burigi, Biharamulo, Kimisi,Ibanda na Rumanyika kuwa Hifadhi ya Taifa.

Akizungumza kwenye mkutano uliohusisha  Wizara Maliasili na Utalii  na Wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali nchini, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Sekta binafsi kwa kuwa sekta hiyo ni injini ya Utalii nchini.

Amesema kuwa mkutano huo una umuhimu mkubwa Katika maendeleo ya sekta hiyo kwa kuwa Serikali  inapata  nafasi ya kuwaelezea Wawekezaji fursa mbalimbali  zinazopatika katika Ukanda huo pamoja na kusikia changamoto zao.

Amesema kufuatia kufanyika kwa mkutano huo Sekta Binafsi itakuwa na kila sababu ya kuwekeza katika Ukanda huo baada ya Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa Uwekezaji

Amesema Serikali imeendelea kuweka Miundombinu wezeshi ambayo imekuwa chachu ya kurahisisha watalii na wageni mbalimbali kutembelea maeneo ya hifadhi.

Mhe.Kanyasu ameyataja maeneo yaliyoboreshwa  kuwa  ni  Barabara,   Uwanja wa ndege wa Mwanza pamoja na  Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Chato ambao umefunguliwa.

Hata hivyo, Mhe.Kanyasu amesema kuwa licha ya   kuwa Tanzania imekuwa ikifanya vizuri kwenye shughuli za Uhifadhi, lakini katika Uendelezaji Utalii bado jitihada za makusudi zinahitajika.

"Tuna vivutio vingi vya utalii lakini idadi ya watalii wanaotembelea vivutio hivyo hairidhishi, tunahitaji kuongeza juhudi katika kuwahamasisha watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea maeneo hayo" Amesisitiza

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye alikua mwenyeji wa mkutano huo, Prof.Adolf Mkenda amesema kupitia mkutano huo kutasaidia kuchagiza idadi ya watalii kuongezeka kwa kutembelea vivutio vya utalii vinavyopatikana katika ukanda huo.

Amesema kufanyika kwa mkutano huo ni muendelezo wa kutawanya fursa za uwekezaji wa sekta ya utalii nchi nzima.

Akichangia hoja kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji Watalii ( TATO)Wilbard Chamburo ameiomba Serikali iangalie uwezekano wa kutobadili  mara kwa mara sera na mipango ya kukuza masuala ya Utalii kwa kuwa kuwa hali hiyo inayochangia kuwakatisha tamaa Wawekezaji.

Amesema Wawekezaji wanataka kuwekeza mahali ambako wana uhakika wa kupata  faida itayowasaidia kujiendesha kibiashara pamoja na kulipa kodi stahiki za serikali.

Katika mkutano huo, Wakuu wa mikoa yote ya Kanda ya Ziwa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mhe.John Mongela walikua miongoni mwa Washiriki.



Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akizungumza  kwenye ufunguzi wa mkutano wa siku moja uliofanyika jana jijini Mwanza  baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii  na Wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuhamasisha Utalii Ukanda wa Ziwa




Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe.John Mongella (wa kwanza kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Hifdadhi za Taifa.Alllan Kijazi (kulia) kabla ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine  (wa pili kushoto)  Kanyasu kufungua mkutano baina ya Wizara hiyo na Wawekezaji  uliofanyika jijini Mwanza.


Baadhi ya washiriki wa mkutano baina ya Wizara ya Maliasili na  Utalii hiyo na Wawekezaji  uliofanyika jijini Mwanza'



 Baadhi ya Wawekezaji wakubwa walioshiriki mkutano wa kuhamasisha utalii kanda ya Ziwa.



Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akizungumza  kwenye  mkutano wa siku moja uliofanyika jana jijini Mwanza  baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii  na Wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali nchini ka lengo la kuhamasisha Utalii Ukanda wa Ziwa




Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu (mbele) akiwa ameongozana na Naibu waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu (wa kwanza kushoto) akiwa pamoja na Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongela(katikati)

Thursday, March 7, 2019

WAZIRI KIGWANGALA ATOA MSIMAMO VITA DHIDI YA UJANGILI,


 Waziri wa Maliasili na Utalii,  Dkt. Hamisi Kigwangala amewataka Watanzania kuondokana na dhana iliyojengeka miongoni mwao kuwa watumishi wa Wizara hiyo hususan  wahifadhi wa  wanyamapori na Misitu  ni watu katili  wanaowatesa Wananchi.


Kauli hiyo ameitoa leo wakati akifungua mkutano wa 26 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi jijini Mwanza.

Amesema watumishi hao ni watu wenye utu na weledi wa hali ya juu na wanaozingatia  sheria katika kutimiza majukumu yao na hulazimika kutumia nguvu wakati wakipambana na majangili wanaokutwa katika maeneo ya hifadhi wakifanya vitendo vya ujangili.

‘’ Ulinzi wa Rasilimali za nchi ni jukumu letu sote, wizara imepewa dhamana ya kusimamia na kuongoza kwa niaba ya watanzania, kama kuna watumishi wa Wizara hii wanaowanyanyasa wananchi naomba walete ushahidi kwetu ili tuwachukulie hatua’’ amesema Dkt. Kigwangala.

Waziri Kigwangala amesikitishwa na idadi ya watumishi walipoteza maisha kwa ajali na wengine kuuwawa na majangili wakati wakipambana nao katika maeneo yote ya hifadhi  nchini na kutoa wito kwa wananchi wote wenye taarifa au ushahidi juu ya vitendo vyovyote vya kihalifu kuziwasilisha katika mamlaka zinazohusika.

Amesema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na vitendo vya ujangili na uhalifu katika maeneo ya hifadhi na wale wote wanaoshirikiana na makundi ya watu wenye nia ovu ya kukwamisha juhudi za uhifadhi wa rasilimali za Taifa.

Ametoa wito kwa wananchi kuheshimu sheria za uhifadhi na kuepuka kuvamia maeneo ya hifadhi kwa shughuli za kijamii na ufugaji akitoa wito kwa viongozi mbalimbali wa Siasa kuunga mkono juhudi za wizara za ulinzi wa maeneo ya hifadhi kwa kuwaelimisha wananchi wanaowaongoza kujiepusha na vitendo vya uvamizi wa maeneo ya hifadhi badala ya kuwatetea.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof.Adolf Mkenda akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho amesema kuwa jumla ya watumishi 23 walifariki dunia  wakati wakitekeleza majukumu ya uhifadhi   na   5 walijeruhiwa na majangili wakiwa kazini.

Prof. Mkenda amesema kuwa waliofanya vitendo hivyo  hawaitakii mema Tanzania na ni maadui wa shughuli za uhifadhi nchini akiongeza kuwa Serikali itaendelea kusimama na kuwatetea watumishi na askari wa wanyamapori wanaotimiza majukumu yao kwa kuzingatia sheria.







 Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala akisisitiza jambo  wakati akizungumza na Watumishi wa Wizara hiyo kuhusu umuhimu wa kutekeleza maagizo kwa wakati yanayotolewa na Viongozi wa Wizara hiyo katika kikao cha Baraza la 26 la  Wafanyakazi wa Wizara hiyo  kilichofanyika leo Jijini Mwanza.

Naibu Waziri wa  Maliasili na Utalii Mhe,Constantine Kanyasu akizungumza na Watumishj wa Wizara  hiyo katika kikao cha Baraza la 26 la  Wafanyakazi kilichofanyika leo Jijini Mwanza

Katibu Mkuu wa  Maliasili na Utalii Prof, Adolf Mkenda akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo (hawapo Pichani) wakati wa ufunguzi wa baraza la 26 la Wafanyakazi wa Wizara hiyo liliofanyika  leo Jijini Mwanza.
 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, Naibu Waziri  wa Wizara, Mhe, Constantine Kanyasu wakiwa wameshikana na watumishi wengine  hukuwakiimba wimbo wa mshikamano Daima katika Kikao cha Baraza la 26 la Wafanyakazi kilichofanyika leo jijini Mwanza.


 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Constantine Kanyasu wakati akikagua gwaride la Jeshi Usu katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Pasiansi


Wafanya kazi wa  Maliasili na Utalii wakiimba wimbo wa mshikamano Daima katika Kikao cha Baraza la 26 la Wafanyakazi wa Wizara hiyo kilichofanyika leo jijini Mwanza.