slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Wednesday, May 31, 2017

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, PROF. JUMANNE MAGHEMBE AFANYA MAZUNGUMZO LEO NA BALOZI WA CHINA NCHINI, DKT. LU YOUGING, MJINI DODOMA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akizungumza na balozi wa China nchini, Dkt. LU Youqing ofisini kwake leo mjini Dodoma ambapo wamejadili na kukubaliana mambo mbali mbali ya kuimarisha uhusiano wa China na Tanzania katika sekta ya maliasili na utalii. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuwakaribisha wawekezaji katika sekta ya viwanda vya uchakataji wa mazao ya misitu na ujenzi wa hoteli katika fukwe za Tanzania na Hifadhi za Taifa.
 Balozi wa China nchini, Dkt. LU Youqing akimueleza jambo Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe alipomtembelea ofisini kwake mjini Dodoma leo. Balozi huyo amekubali ombi la Waziri Maghembe kuwaleta wadau wa mashirika ya utalii kutoka nchini China kwa ajili ya kutembelea vivutio vya utalii vya Tanzania na kuvitangaza nchi kwao.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akimfafanulia jambo balozi wa China nchini, Dkt. LU Youqing alipomtembelea ofisi kwake leo mjini Dodoma. Waziri Maghembe kupitia balozi huyo ameipongeza Serikali ya China na Wananchi wake kwa uamuzi wake wa hivi karibuni wa kufungia biashara haramu ya meno ya tembo nchini humo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akiagana na Balozi wa China nchini, Dkt. LU Youqing baada ya mazungumzo marefu ofisini kwake leo mjini Dodoma.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kulia), Balozi wa China nchini, Dkt. LU Youqing (kushoto), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili, Dkt. Aloyce Nzuki (kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Justa Nyange wakijadili jambo muda mfupi baada ya mazungumzo hayo. (PICHA ZOTE NA HAMZA TEMBA - WMU)

Monday, May 29, 2017

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, PROF. JUMANNE MAGHEMBE APONGEZA OPERESHENI YA KUONDOA MIFUGO HIFADHINI MKOANI KAGERA, ATAKA TARATIBU ZA UWAZI ZIFUATWE KWENYE ZOEZI LA MNADA WA MIFUGO ILIYOTAIFISHWA KISHERIA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kushoto) akisalimiana na Viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kagera katika ziara yake mkoani humo kuzungumzia operesheni ya kuondoa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na taratibu sahihi za kuendesha minada ya mifugo iliyotaifishwa kisheria na mahakama. Anayeongoza utambulisho huo (kushoto) ni Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu. 
Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kagera, mjini Bukoba kuhusu operesheni ya kuondoa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na taratibu sahihi za kuendesha minada ya mifugo iliyotaifishwa kisheria. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro. 

NA HAMZA TEMBA - WMU
---------------------------------------------------------

Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Kagera unaongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu kwa kufanikisha operesheni ya kuondoa mifugo katika maeneo ya hifadhi mkoani humo huku akitoa tahadhari kwa watumishi wa hifadhi hizo kupoteza ajira zao endapo wataruhusu mifugo hiyo kurudi tena katika hifadhi hizo.

Ametoa pongezi na tahadhari hiyo jana mjini Bukoba wakati akizungumza na uongozi wa mkoa huo na kusema kuwa, kazi hiyo ni ya kupongezwa sana kwakua imeleta matumaini ya uhifadhi mkoani Kagera na taifa kwa ujumla.

“Napenda niwashukuru kipekee kabisa kwa jinsi ambavyo mlifanya ile operesheni ya kuondoa mifugo kwenye hifadhi zetu, tulifanya kwa ueledi uliotukuka, hata kama umesikia watu wanalalamika lakini hakuna aliyesema kuku wangu waliuawa, walipigwa risasi, tulinyang’anywa mifugo, kazi hii ilifanywa vizuri na kwa ueledi mkubwa sana”, alisema Prof. Maghembe.

Aliongeza, “Hatutaruhusu tena mifugo hiyo irudi huko ndani ya hifadhi, hili ni jambo kubwa ambalo ni wajibu wa wahifadhi wote kuhakikisha  kwamba hakuna mifugo itakayokuwa inaingia humo ndani, Kuanzia sasa kama tutakuta mtu ameingia kwenye hifadhi yako wakati tunamuondoa tunamuondoa yeye na wewe na familia yako yote ili mbegu yako mbaya isibaki katika uhifadhi wa wanyamapori”.


“Haiwezekani kwamba kila siku Serikali yote inafunga kazi zingine zote tunahamia kuondoa wavamizi na ninyi mpo na kazi yenu ni kuhakikisha kwamba wavamizi hawaingii humo, Kwahiyo hii sio temporary na wala sio nguvu ya soda, hata kidogo, na kusema kila siku inakua hivi hivi itaisha, tutaingia tu, hakuna hiyo,  kwahiyo mfanye kazi yenu, mlinde, na wanyama wakiingia humo itakua kazi imewashinda na itakua imewashinda “permanently” ni vizuri mjue msije mkadhani kwamba hamkuambiwa, ndio maana nimekuja na wakurugenzi wenu wote ili wasikie na walisimamie jambo hili” alisema.


Waziri Maghembe katika ziara yake hiyo ya mkoani Kagera aliongozana na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexander Songorwa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi za Wanyamapori, Martin Loibooki na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo. Alitembelea pia mikoa ya Tabora na Shinyanga ambapo alitoa maelekezo muhimu ya kuondoa mifugo kwenye hifadhi.

Alisema ili kuimarisha ulinzi katika hifadhi hizo, utaratibu wa kutumia ndege maalum za doria na “drones” (ndege zisizo na rubani) utawekwa ili kuwabaini wahalifu watakaokuwa wamekaidia agizo hilo ili wachukuliwe hatua za kisheria.  

“Tutakua tunarusha ndege mara moja kila baada ya wiki tatu au wiki mbili kuhakikisha kwamba hakuna mtu anaingia na mifugo humo ndani, lakini pili tutafanya doria na ndege zile ambazo hazina marobani kuhakikisha kwamba tunaangalia kinachotokea humo ndani wakati wote.

“Najua wanaweza kubadilisha “system” (utaratibu) ikawa ya usiku na hawa askari hawa tutawapa mafunzo maalum chini ya jeshi la wananchi wa Tanzania, kuanzia miezi sita mpaka tisa, wajifunze namna ya kuhangaika na hawa ambao wanaingia kwenye hifadhi zetu”, alisema. 

Akizungumzia operesheni hiyo, alisema ulitolewa muda maalum kwa watu kutoa mifugo yao kwa hiari katika mapori ya akiba na hifadhi za misitu mkoani humo ambapo wale wote waliotii hakuna mashtaka yeyote yalifunguliwa dhidi yao ispokuwa wale waliokaidi walifikishwa mahakamani na mifugo yao ikataifishwa kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori kifungu namba 111 sehemu ya kwanza ambayo inaruhusu kutaifisha mali itakayokutwa hifadhini.

Alisema kuwa kumekuwepo na malalamiko mbalimbali juu ya utaratibu wa upigaji mnada mifugo iliyotaifishwa ikiwemo minada hiyo kufanyika ndani ya maeneo ya hifadhi, wenye mifugo kutoruhusiwa kuingia na wakati mwingine kuwepo kwa malalamiko ya idadi tofauti ya mifugo iliyotaifishwa na inayopelekwa mnadani.

Ili kuondoa malalamiko hayo alielekeza kuwa baada ya amri ya mahakama kutoka ni lazima mamlaka ya Wilaya husika ijulishwe na zoezi hilo lifanyike katika maeneo ya wazi ili kila mwananchi anayehitaji aweze kushiriki mnada husika.

“Minada hii ifanywe kwa maelekezo ya mamlaka, hukumu ikitoka mkuu wa wilaya ajulishwe, na kwamba mifugo kadhaa itapigwa mnada, na yeye ataamua mnada ufanyike wapi na lini, na iwe sehemu ambayo kila mtu anaweza kufika, minada hiyo iwe ya wazi na matangazo yatolewe ili malalamiko yasiwepo ndio maana maelekezo yametoka minada isitishwe kwa muda wa siku saba mambo haya yawekwe sawa”, alisema Maghembe.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu alishukuru kwa ushirikiano alioupata kutoka Wizara ya Maliasili katika kipindi chote cha utekelezaji wa operesheni hiyo ambayo amaeielezea kuwa na mafanikio makubwa ikiwemo wanyamapori kuanza kurudi kwenye maeneo yao katika Mapori ya Akiba ya Biharamulo Burigi na Kimisi.

“Niishukuru wizara yako mmetupa ushirikiano mzuri, kule tumesafisha tumehakikisha hakuna mifugo, hakuna kilimo, vitendo mbalimbali vya kibinadamu vilivyokuwa vikifanywa kule vya kilimo, ukataji miti hovyo, kuchoma mikaa, kulima mashamba mbalimbali ya mahindi, bangi, mirungi sasa hayapo tena, Nashukuru kwa muda huu mfupi wanyama wengi wamesharudi, wengi tuu, hadi Simba wamesharudi kwenye maeneo yao” alisema Kijuu.

Operesheni ya kuondoa mifugo na wananchi waliovamia Hifadhi ya Misitu ya Biharamulo, Nyantaka na Ruiga na Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi na Kimisi mkoani Kagera ilianza tarehe 30 Machi, 2017 ambapo jumla ya mifugo 5,939 ilikamatwa (Ng’ombe 5754, Mbuzi 140 na kondoo 45) na watuhumiwa 185 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.  
Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kagera, mjini Bukoba kuhusu operesheni ya kuondoa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na taratibu sahihi za kuendesha minada ya mifugo iliyotaifishwa kisheria. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro (kulia), Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Diwani Athuman (wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexander Songorwa. 
Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akizungumza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kagera, mjini Bukoba. 
Picha ya pamoja kati ya Waziri wa Maliasili (katikati waliokaa) na kamati ya ulinzi na usala ya Mkoa wa Kagera muda mfupi baada ya kikao cha kujadili operesheni ya kuondoa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na taratibu sahihi za kuendesha minada ya mifugo iliyotaifishwa kisheria.
 Picha ya pamoja kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii (katikati waliokaa), Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu (wa pili kulia waliokaa), Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro (wa pili kushoto waliokaa), Katibu Tawala Mkoa huo, Diwani Athuman (kulia waliokaa), Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexander Songorwa (kushoto waliokaa), Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Martin Laibooki (katikati waliosima) na maofisa wa Mamlaka hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu (kushoto) akizungumza na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Martin Laibooki (wa pili kushoto) Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa Kudhibiti ujangili, Faustine Masalu (kulia).
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexander Songorwa (kulia), Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo (katikati) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Martin Laibooki (kushoto). 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akisalimiana na uongozi wa Wilaya ya Biharamulo alipotembelea wilayani humo kwa ajili ya kutoa maelekezo ya Serikali kuhusu operesheni ya kuondoa mifugo katika maeneo ya hifadhi pamoja na taratibu sahihi za kuendesha minada ya mifugo iliyokamatwa na kutaifishwa na mahakama. Anayeongoza utambulisho huo (kulia) ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Sada Malunde.
 Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na viongozi wa Kamati ya Ulinzi na usala ya Wilaya ya Biharalamulo na watumishi wa sekta ya wanyamapori wilayani humo. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Kamati ya Ulinzi na usala ya Wilaya ya Biharalamulo na watumishi wa sekta ya wanyamapori wilayani humo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Sada Malunde na Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Diwani Athuman (kushoto). 
 Baadhi ya askari na watumishi wa Idara ya Wanyamapori wa Wilaya ya Biharamulo.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, viongozi wa mamlaka za uhifadhi, watumishi na kamati ya ulinzi na usala ya Wilaya.
Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe akiagana na Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Diwani Athuman pamoja na viongozi wengine wa chama na Serikali wa Wilaya ya Biharamulo baada ya kumaliza ziara yake Mkoani humo ya kujadili operesheni ya kuondoa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na taratibu sahihi za kuendesha minada ya mifugo iliyotaifishwa kisheria. 

Sunday, May 28, 2017

WAZIRI WA MALIASILI, PROF. JUMANNE MAGHEMBE ATEMBELEA CHUO CHA BTI TABORA, AMTAKA MKUU WA MKOA HUO KUANDAA UTARATIBU KWA WAJASIRIAMALI WA UFUGAJI NYUKI KUJIFUNZA CHUONI HAPO

Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akisaini kitabu kitabu cha wageni chuoni hapo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akizungumza na uongozi wa chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki, Tabora BTI alipotembelea chuoni hapo leo. Kulia ni Mkuu wa chuo hicho Semu Daudi na Mratibu Mkuu wa Mafunzo, Igunda John.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry (kulia) na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe wakati akitoa maelekezo mbalimbali chuoni hapo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry baada ya kutembelea Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki, Tabora, BTI leo.

NA HAMZA TEMBA - WMU
-----------------------------------------------------------
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry kutumia fursa ya uwepo wa Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki, Tabora, BTI mkoani humo kwa kuandaa utaratibu maalum utakaowawezesha wananchi hususan wafugaji wa nyuki kuhudhuria mafunzo ya muda mfupi ya ufugaji wa nyuki chuoni hapo kwa ajili ya kuboresha uzalishaji wa bidhaa hiyo na kuwaongezea kipato.

Waziri Maghembe ametoa kauli hiyo leo alipotembelea chuoni hapo wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Tabora kwa ajili kujionea changamoto mbalimbali za uhifadhi na kuona namna kukabiliana nazo ikiwa ni ahadi aliyoitoa bungeni wakati akihitimisha mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka huu wa fedha 2017/2018.

“Mkuu wa Mkoa, tafadhali andaa utaratibu maalum kwa wananchi wako, wale wafugaji wa nyuki wanaweza kuja kwenye chuo chetu hapa hata siku tatu, hata siku mbili, wafundishwe namna bora ya kufuga nyuki, yani watoke kabisa huko Skonge, waletwe hapa, walale hapa sku moja au mbili wafundishwe baadae warudi makwao wajue namna bora ya kufuga na kuvuna asali,” alisema Maghembe.

Kwa upande wake Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora alisema maelekezo hayo kwao ni faraja kwakuwa tayari kuna maelekezo ya kiserikali kusaidia makundi ya kinamama na vijana ikiwemo utoaji wa mikopo kwa vikundi vyao vya ujasiriamali.

 “Katika Mkoa wangu tuna makundi haya ya kinamama na vijana ambao tumetakiwa kuwasaidia kwa maana ya kutenga “percent” (asilimia) fulani katika “own source” (vyanzo vya ndani vya mapato), kwahiyo kwa maelekezo hayo hayo nitakachofanya mimi ni kuhakikisha kwamba tunaenda kuwaeleza katika hali ya kawaida kwamba tungeweza kuwapa mikopo lakini tungependa tuwape mikopo baada ya kupata taaluma na waweze kujua vizuri namna bora ya kufuga nyuki na kurina asali”, alisema Mwanri.

Mkuu wa Chuo hicho, Semu Daudi alisema chuo hicho kina jumla ya wanafunzi 155 na kinatoa mafunzo ya Cheti na Diploma ya Ufugaji wa Nyuki.

Naye Mkuu wa Kituo kidogo cha Utafiti wa Ufugaji Nyuki chuoni hapo, Humphrey Natali alisema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto ya vitendea kazi ikiwemo usafiria ambapo gari lililokuwepo limepelekwa matengenezo na kompyuta zilizopo nazo ni za muda mrefu.

Waziri Maghembe ameahidi kukipatia kituo hicho gari moja huku akimuagiza, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo kuona uwezekano wa kumaliza changamoto mbalimbali chuoni hapo.

TANAPA, NGORONGORO, TAWA NA TAWIRI KUUNGANISHWA KUWA TAASISI MOJA - PROF. MAGHEMBE

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akijibu hoja mbalimbali wakati akihitimisha mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2017/2018 bungeni mjini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo makani akijibu hoja mbalimbali wakati wa kuhitimisha mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2017/2018 bungeni mjini Dodoma.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, Viongozi wakuu na baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo wakiwa nje ya lango la Bunge mara baada ya kikao cha Bunge kupitisha bajeti ya Wizara hiyo.

Na Hamza Temba - WMU 
---------------------------------------------------------------------
Serikali inafikiria kuunganisha taasisi zote zinazohusika na sekta ya uhifadhi wa wanyamapori nchini kuwa chombo kimoja chenye nguvu  kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji wa taasisi hizo pamoja na kuongeza ufanisi wa kiutendaji katika sekta hiyo muhimu hapa nchini.

Akizungumza mwishoni mwa wiki bungeni mjini Dodoma wakati akihitimisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe alisema anaunga mkono ushauri uliotolewa na wabunge mbalimbali ukiwemo wa Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Atashasta Nditiye juu ya umuhimu wa kuunganisha taasisi hizo za uhifadhi.

"Wakati umefika sasa, tusiwe na makampuni (taasisi) zaidi ya manne ndani ya sekta hii ya wanyamapori, tuwe na kampuni (taasisi) moja tu ambayo itapunguza gharama katika uendeshaji, tutaunganisha jeshi la wahifadhi na jeshi hilo tutakalolitengeneza ni jeshi moja tu ambalo litakua na malezi chini ya jeshi la wananchi wa Tanzania, ili kujenga nidhamu, kuheshimu haki za binadamu na kufanya kazi kwa mujibu wa maslahi ya taifa,". alisema Maghembe. 

Aliongeza kusema "Jeshi hilo ambalo tunaliandaa kisasa, jeshi usu litakua na "chain ya comand" moja na litawajibika kijeshi kwa makosa ya haki za kibinadamu na usaliti wa taifa au usaliti wa uchumi wa nchi yetu".

Awali akiwasilisha bungeni hapo hotuba ya makadidirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake, Prof. Maghembe alizitaja taasisi hizo kuwa ni Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) na  Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI).  

Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) lilianzishwa mwaka 1959 kwa Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura 282 na kupewa dhamana ya kusimamia na kuendeleza maeneo yaliyoanzishwa kisheria kuwa Hifadhi za Taifa. Hifadhi hizo ambazo zipo 16 zina jumla ya kilometa za mraba 57,365.80. 

Kwa upande wake, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) ilianzishwa kwa Sheria Sura 284 na kupewa jukumu la kusimamia eneo la kilometa za mraba 8,292 kwa ajili ya kuhifadhi, kuendeleza utalii na wafugaji wenyeji wa eneo hilo ambapo wakati mamlaka ikianzishwa walikua takriban 8,000 mwaka 1959 na idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia zaidi ya wakazi 90,000 mwaka uliopita, 2016. 

Nayo, Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) ilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Na.135 la tarehe 9 Mei, 2014 chini ya Kifungu cha 8 cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Sura 283 ikisomwa pamoja na marekebisho yake yaliyotolewa katika Tangazo la Serikali Na.20 la tarehe 23 Januari 2015. Mamlaka hiyo ilianza kazi rasmi tarehe 1 Julai, 2016. 

Mamlaka hiyo ina jukumu la kusimamia uhifadhi wa wanyamapori kwenye Mapori ya Akiba 28, Mapori Tengefu 42  na maeneo ya wazi yenye mazalia ya wanyamapori, mtawanyiko na shoroba. Aidha, Mamlaka inashirikiana na jamii katika kusimamia maeneo 22 ya jumuiya za hifadhi za wanyamapori na maeneo manne ya ardhioevu yenye umuhimu wa kimataifa (Ramsar Sites).

Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) ilianzishwa kwa Sheria Sura 260 kwa lengo la kusimamia, kufanya na kuratibu utafiti wa wanyamapori nchini. Taasisi hiyo ina wajibu wa kutoa ushauri kuhusu uhifadhi endelevu wa wanyamapori kwa kutumia matokeo ya utafiti wa kisayansi. Aidha, TAWIRI inawajibu wa kufanya Sensa ya makundi mbalimbali ya Wanyamapori ili kushauri Wahifadhi na Serikali.

Akizungumzia umuhimu wa uhifadhi wa Wanyamapori, Prof. Maghembe alisema sekta ya maliasili kwa ujumla inachangia asilimia 21.4 ya pato lote la taifa, ambapo mchango wa wanyamapori kupitia utalii ni asilimia 17.5 na misitu asilimia 3.9. Aliongeza kuwa wanyamapori pia husaidia katika tafiti mbalimbali duniani kwa ajili ya utafutaji wa dawa za kutibu maradhi ya binadamu.

Katika mwaka huu wa fedha 2017/2018, Bunge limeidhinisha Sh. bilioni 148.597 kwa ajili ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii, ambapo Sh. bilioni 96.794 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Sh. bilioni 51.803 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. 

Thursday, May 25, 2017

SOMA HOTUBA NZIMA YA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII PROF. JUMANNE MAGHEMBE ALIPOWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA HIYO KWA MWAKA 2017/2018

Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2017/2018. Bajeti hiyo imepitishwa na Bunge tarehe 24 Mei, 2017.

Tuesday, May 23, 2017

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII PROF. JUMANNE MAGHEMBE LEO AMEWASILISHA BUNGENI HOTUBA YA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA HIYO KWA MWAKA 2017/2018

Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara hiyo kwa mwaka 2017/2018 leo  mjini Dodoma. UNAWEZA KUSOMA HOTUBA ALIYOIWASILISHA HAPO CHINI.

Sunday, May 21, 2017

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YATOA SEMINA KWA WABUNGE JUU YA UMUHIMU WA UHIFADHI WA MALIASILI, MALIKALE NA MAENDELEO YA UTALII NCHINI

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta  Ndetiye (kushoto) akizungumza wakati wa semina hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na kufanyika katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma jana. Kulia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Prof. Jumanne Maghembe. Semina hiyo ilihusu umuhimu wa uhifadhi wa Maliasili Malikale na Maendeleo ya Utalii nchini.
Baadhi ya viongozi na watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakiwa ndani ya ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania muda mfupi kabla ya kuanza kuwasilishwa kwa mada mbalimbali katika semina hiyo. Mada zilizowasilishwa katika semina hiyo ni Kwanini Watanzania tuhifadhi uoto wa asili na Wanyamapori, Athari za Muingiliano wa Mifugo na Wanyamapori, Maendeleo ya Utalii na umuhimu wake katika uchumi wa Tanzania na Umuhimu wa Uhifadhi wa Misitu Nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jeneral Gaudence Milanzi akizungumza katika semina hiyo iliyoandaliwa na Wizara kwa ajili ya wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mkurugenzi wa Idara wa Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Alexander Songorwa askiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa Watanzania kuhifadhi uoto wa asili na Wanyamapori katika semina hiyo. Kushoto waliokaa ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe na baadhi ya viongozi na wakurugenzi wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Prof. Songorwa akiwasilisha mada hiyo. 
Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Dkt. Robert Fyumagwa akiwasilisha mada juu ya Athari za Muingiliano wa Mifugo na Wanyamapori katika semina hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo akiwasilisha mada juu ya Umuhimu wa Uhifadhi wa Misitu Nchini. Alieleza kuwa umuhimu wa misitu ni sawa na hewa safi ambayo inatoa uhai kwa mwanadamu na endapo misitu hiyo itatoweka kutokana na uharibifu unaoendelea basi maisha ya binadamu nayo yatakuwa hatarini kwa kuwa hewa hiyo chanzo chake ni misitu na mimea.
Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania, Richard Rugimbana akiwasilisha mada kuhusu Maendeleo ya Utalii na umuhimu wake katika uchumi wa Tanzania kwa wabunge hao.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta  Ndetiye (kushoto) wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika semina hiyo.
Aliyekuwa MC wakati wa semina hiyo, Meneja wa Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, Paschal Shelutete akiteta jambo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zito Kabwa muda mfupi baada ya kuhitimishwa semina hiyo.
 Baadhi ya viongozi wa Wizara ya Maliasili walioshiriki semina hiyo bungeni mjini Dodoma.
Bungeni wakati wa semina hiyo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kushoto), Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya (wa pili kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Alexander Songorwa na Mkurugenzi wa Idara ya Misitu Wizara ya Maliasili, Dkt. Ezeckiel Mwakalukwa wakitoka katika ukumbi wa bunge mara baada ya semina hiyo.

Tuesday, May 9, 2017

BREAKING NEWS: TEMBO WANNE WAONEKANA CHUO KIKUU CHA DODOMA (UDOM) LEO, ASKARI WA WANYAMAPORI WAANZA KAZI KUWARUDISHA HIFADHINI

Tembo wakiwa wamejificha kwenye vichaka ndani ya eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) leo. Kwa mujibu wa taarifa za Wahifadhi wa Wanyamapori inaelezwa kuwa sehemu ya eneo hilo litakuwa ni njia ya tembo (maeneo ya mapito ya wanyamapori) ambayo ilipitika kwa miaka mingi iliyopita na kwamba tembo wana kumbukumbu hata kama walipita njia hiyo kwa zaidi ya miaka 50 iliyopita. Imeelezwa kuwa njia hiyo ya mapito ya wanyamapori itakua ilitumiwa na wanyamapori kuhama eneo moja hadi jengine ikiwemo maeneo ya hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Ruaha, Serengeti, Pori Tengefu la Rugwa na maeneo mengine ya hifadhi na kwamba maeneo hayo mengi kwa miaka ya hivi karibuni yameshaingiliwa na shughuli za kibinadamu ambazo hazisababishi tembo hao kusahau njia hizo au kutokuzitumia tena.
Tembo hao wakiwa ndani ya eneo chuo kikuu hicho cha Dodoma leo. Hakuna madhara yeyote yaliyoripotiwa kusababishwa na tembo hao na taratibu za kuwarudisha kwenye maeneo yao ya hifadhi zimeshaanza kuchukuliwa na uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo Askari wa Wanyamapori wameanza zoezi la kuwafukuza kuwarudisha kwenye maeneo yao ya hifadhi.
Prof. Julius Nyahongo wa Chuo Kikuu cha Dodoma akitoa somo kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Dodoma namna ya kuchukua tahadhari juu ya ugeni wa tembo hao chuoni hapo. Aliwaeleza wanafunzi hao kuwa mazingira ya chuoni hapo yataendelea kuwa salama kwakuwa tembo hao wapo katika njia yao ya mapito na pengine kumewahi kukucha kabla ya wao kufika mwisho wa safari yao, hivyo kwa msaada wa askari wa wanyamapori ambao wamewasili chuoni hapo itasaidia  kuwaondoa tembo hao waweze kuendelea na safari yao hadi kwenye maeneo ya hifadhi.
Wanafunzi mbalimbali wa Chuo Kikuu cha Dodoma walikusanyika wakiwa na shauku ya kuwaona tembo hao.
Msafara wa viongozi mbali mbali wa Serikali ukiambatana na Askari Polisi na Askari wa Wanyamapori ukisogelea eneo walilokuwepo tembo hao kwa ajili ya kuanza kuwafukuza kutoka katika maeneo hayo ya chuo kwenda kwenye maeneo yao ya hifadhi.
Prof. Julius Nyahongo wa Chuo Kikuu cha Dodoma (wa pili kulia), Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, Paschal Shelutete (wa tatu kulia) na maafisa wengine wa Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama wakiangalia eneo walilokuwa wamejificha tembo hao chuoni hapo.
Askari wa wanyamapori wakiingia ndani ya eneo walilokuwa wamejificha tembo hao kwa ajili ya kuanza kuwafukuza eneo hilo kuelekea kwenye maeneo yao ya hifadhi. Imeelezwa kuwa pindi tembo hao watakapofukuzwa kwa milio maalum ya risasi hutafuta njia wanazozijua wenyewe za kurudi kwenye maeneo yao ya hifadhi.
Tembo hao wakianza kuondoka katika eneo hilo baada ya askari wa wanyamapori kuanza kuwaondoa eneo hilo kwa kutumia milio maalum ya risasi.