slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Monday, July 3, 2017

SHIRIKA LA KIJAMII LA UHIFADHI WA WANYAMAPORI (WCS) LATOA MSAADA WA VITENDEA KAZI KATIKA PORI LA AKIBA LA LUKWATI/ PITI.

Na: Chifuno Crispo Jembe
.......................................................................

Mapori ya akiba Lukwati  na Piti yapo katika Wilaya ya Songwe mkoani Songwe, awali kabla ya kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Songwe yalikuwa katika eneo la Mkoa wa Mbeya katika Wilaya ya Chunya, pori la akiba la Lukwati  lilianzishwa tarehe 08/08/1997 (G.N Na 459) na lina kilometa za mraba 3,146.7 na pori la akiba Piti lilianzishwa tarehe 19/04/2013 (G.N Na 75)  na lina jumla ya Km za mraba 2,972.93. Mapori yote mawili yana jumla ya  km za mraba 6,119.63.

Hifadhi ya mapori ya akiba ya Lukwati/Piti yanasisimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na ni moja ya mapori ya akiba yaliyohifadhiwa na kuwa na wanyamapori wengi kama Tembo, Simba, Chui, Mamba, Viboko, Nyati, Palahala, Kongoni, Pundamilia na wengineo.

Hifadhi ya wanyamapori ya Lukwati/Piti ni moja ya mapori ya akiba ambayo yamefanikiwa kwa asilimia kubwa kuzuia uvamizi wa mifugo na shughuli zingine za kibinamu kama uvamizi wa kilimo na uvuvi katika ufukwe wa ziwa Rukwa ambao umepakana na pori la akiba la Lukwati.

Sababu hizi zinapelekea kuwa moja ya maeneo yaliyohifadhiwa na TAWA yenye thamani kubwa za kiikolojia na kiuchumi. Shughuli za uwindaji wa kitalii zinazofanyika kila msimu wa mwaka katika maeneo haya zinaonekana kuchangia kiasi kikubwa cha pato katika makusanyo ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA). 

Pamoja na udogo wake ukilinganisha na mapori ya akiba mengine kama Selous na Rungwa utaona Lukwati/Piti ina kamata nafasi ya nne kwa makusanyo yatokanayo uwindaji wa kitalii na kuendelea kuwa moja sehemu muhimu ya kivutio cha utalii kutoka nje chini ya TAWA.

Baada ya kuona umuhimu huu wa kiikolojia basi Shirika La Kijamii La Uhifadhi Wa Wanyamapori (WCS) limeona umuhimu wa kusaidia baadhi ya vitendea kazi katika kituo cha Mapori ya Akiba ya Lukwati na Piti.

WCS kupitia programu yao ya uhifadhi wa ikolojia ya Ruaha-Katavi wametoa msaada wa vifaa vifuatavyo;

Mosi wamefanikisha ujenzi wa jengo la utawala wa zaidi ya milioni 227 na samani zake katika mapori ya Akiba ya Lukwati na Piti ambalo awali Msimamizi Mkuu (Meneja) wa mapori hayo hakuwa na ofisi za utawala ambazo angeweza kufanya baadhi ya shughuli za kiutawala kituoni hapo lakini kwa sasa tunaamini kupitia msaada huu wa WCS usisimamizi wa hifadhi hizi za Wanyamapori zitaimarika na kuwa zenye ufanisi mkubwa zaidi katika kulinda Wanyamapori. 

Shirika La Kijamii La Uhifadhi Wa Wanyamapori (WCS) wametoa msaada wa magari maalam kwa ajili ya shughuli za doria pamoja na spidi boti kwa ajili ya kuimarisha shughuli za doria katika sehemu ya ziwa Rukwa ambayo ni eneo la hifadhi hiyo ya Mapori ya Akiba ya Lukwati na Piti.

Sambamba na hayo WCS imetoa mafunzo ya utayari kwa kikosi maalum (RRT) na kwa tafrisi isiyo rasmi ni kwamba Lukwati/ Piti ina kikosi maalum kama cha F.F.U ambacho kimepewa mafunzo ya kupambana na ujangili katika eneo na muda wowote.

Wametoa vifaa kama GPS na SMART ili kusaidia doria za miguu na vifaa maalum vya kubebea maji wakati wa doria ndefu za miguu ikiwemo pia mavazi maalum wakati wa doria za masika.

WCS wamewafungia mfumo wa mawasiliano ya simu za upepo za kidigitali katika mapori haya ya Akiba katika magari yao yote kituoni hapo, vituo vidogo vyote mradini hapo pamoja na simu za upepo za mkononi ili kuleta mawasiliano ya uhakika ukizingatiwa karibu eneo lote la mapori hayo hayafikiwi na mtandao wa aina yoyote wa mawasiliano ya simu za mkononi.

Kumekuwa na changamoto ya maji ya uhakika katika vituo vidogo vya doria lakini WCS katika mipango yao ya baadae wameshaahidi kuchimba kisima kimoja kirefu cha maji katika moja ya vituo vidogo (game post) ili kurahisisha kupatikana kwa maji ya kutosha kwa askari wa ulinzi wa wanyamapori katika Mapori haya ya Lukwati na Piti.

Kama mdau wa masuala ya uhifadhi nawapongeza WCS kwa misaada hii kwani itasaidia kupunguza changamoto katika vita ya mapambano dhidi ya ujangili wa aina yoyote katika maeneo hayo.

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Katibu Mkuu Mhe. Maj. Gen. Gaudence Milanzi imepeleka shukrani zake Shirika la Wahisani la Watu wa Marekani USAID ambao ni wafadhili wa shirika hilo la kijamii la kimataifa la Uhifadhi Wanyamapori (WCS) kwa ushirikiano na juhudi zao kubwa za kuimarisha ulinzi wa Wanyamapori hasa Tembo kwenye ukanda wa ikolojia ya Ruaha-Katavi kupitia programu ya SHARPP( Southern Highlands and Ruaha-Katavi Protection Program), shukrani hizo pia zimetolewa kwenda WYSS FOUNDATION ambao wamekuwa pamoja katika kusaidia juhudi za Uhifadhi na Ulinzi wa Wanyamapori.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj Gen. Gaudence Milanzi akikata utepe kuashia uzinduzi na mapokezi ya magari hayo yaliyotolewa na WCS kwa ajili ya pori la Lukwati/Piti,  Rukwa na Rungwa. Kushoto kwake ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAWA, Martin Loibooki.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj Gen. Gaudence Milanzi (wa tatu kulia) akikagua kikosi cha RRT kutoka Lukwati/Piti kilichopewa mafunzo na jeshi la marekani kupitia ubalozi wa marekani nchini kwa ufadhili wa WCS.
Magari hayo 3 ya doria yalikabidhiwa kwa ajili ya pori la Lukwati/Piti,  Rukwa na Rungwa.
Mkurugenzi wa WCS, Aaron Nicholas (kushoto) akikabidhi jengo la milioni 227 kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kulia) kwa ajili ya shughuli za utawala kwa Mapori ya akiba ya Lukwati/Piti. Wa tatu kulia anaeshuhudia ni Kaimu kurugenzi Mkuu wa TAWA, Martin Loibooki.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kulia) akipokea maelezo kutoka kwa Askari wa Lukwati/Piti juu ya ukusanyaji wa taarifa katika eneo la tukio "Crime Scene Management".
 

1 comment:

  1. Shukrani muandishi kwa makala hii fupi. Napenda kutoa Shukrani kwa WCS kwani wamekua na jitihada na michango mikubwa ktk uhifadhi wa wanyamapori wetu.... Ikumbukwe si Lukwati /Piti pekee wamefadhili mafunzo pamoja na vitendea kazi kwani hata ktk mapori ya akiba Rukwa /Lwafi na Rungwa wamesaidia pia... No vyema taasisi zingine zikaiga jitihada za WCS na kushiriki nasi ktk uhifadhi

    ReplyDelete